Sare yaipa mzuka JKT Queens CAFWCL

KOCHA wa JKT Queens, Abdallah Kessy, amesema kikosi hicho bado kina nafasi nzuri ya kufanya vizuri kwenye mchezo ujao dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast, utakaochezwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Suez Canal jijini Ismailia, Misri.

JKT Queens ambao ni wawakilishi pekee wa ukanda wa CECAFA katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake walianza kampeni zao kwa sare ya bila mabao dhidi ya Gaborone United ya Botswana kwenye mechi ya kundi B, mchezo uliochezwa saa 1 usiku nchini Misri.

Kessy amesema sare hiyo sio matokeo mabaya kwao na inawapa motisha kubwa kuelekea mchezo wao wa pili wa hatua ya makundi dhidi ya Asec utakaopigwa kesho uwanjani hapo.

“Tulikuwa na nafasi nzuri za kufunga lakini bahati haikuwa upande wetu. Tumeambulia sare ambayo si mbaya, na matokeo haya hayawezi kutukatisha tamaa,” amesema Kessy na kuongeza:

“Tumebaini makosa madogo yaliyotokea kwenye mchezo wa kwanza na tutayarekebisha. Tunaamini mechi dhidi ya ASEC itatupa nafasi nzuri ya kusonga mbele hatua ya nusu fainali ingawa haitakuwa rahisi hata kidogo.”

Kwa upande wa kipa wa timu hiyo, Naijat Abbas ambaye aliokoa penalti muhimu kwenye mechi dhidi ya Gaborone United amesema matamanio yao ilikuwa pointi tatu lakini bahati haikuwa upande kwao wakaambulia moja.

”Kila mchezaji alikuwa na morali ya kushinda mechi na kocha alituambia tutumie kila nafasi tunayopata na ikitokea hatujashinda basi tupate angalau sare,” amesema Naijat.

Jumatano hii saa 1 usiku mabingwa hao mara mbili wa michuano ya CECAFA kwa wanawake watakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya nusu fainali.

Mechi nyingine ya kundi B iliyopigwa jana mabingwa watetezi TP Mazembe walipokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Asec Mimosas ya Ivory Coast ambao ni mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo.

Dakika ya 88, Kesegofetse Mochawe wa Gaborone United alipata penalti baada ya beki wa JKT kufanya makosa ndani ya eneo la hatari na Naijat wa JKT akaokoa penalti hiyo kwa ujasiri mkubwa.

Hata hivyo refa aliamua penalti irudiwe akidai kipa huyo alitoka kwenye mstari wake kabla ya muda. Keitumetse Dithebe akarudia kupiga penalti hiyo, lakini kipa huyo akaokoa tena.