Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi ametaja vipaumbele na mwelekeo mpya wa Serikali katika kipindi cha pili cha utawala wake, akisema yupo tayari kutekeleza maridhiano na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pamoja na kuunda SUK, Dk Mwinyi amesema Serikali itaimarisha nidhamu, uzalendo, weledi na kudhibiti vitendo vyote vinavyoondoa utawala bora.
Dk Mwinyi amebainisha hayo leo Novemba 10, 2025 wakati akizindua Baraza la 11 la Wawakilishi Zanzibar kufuatia uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge, wawakilishi na madiwani uliofanyika Oktoba 28 na 29, 2025.
Akizungumza wakati akihutubia baraza hilo, Dk Mwinyi amesema Serikali atakayoiunda ina dhamira ya mipango mikuu ya maendeleo na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kipindi kilichopita.
Katika hotuba yake ya dakika 50, kuanzia saa 5:35 asubuhi hadi saa 6:25 mchana, Dk Mwinyi amesema kipaumbele muhimu cha Serikali ni kuendeleza na kudumisha amani na mshikamano kama msingi mkuu wa maendeleo.
“Ni dhamira yangu kuzidi kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar kuwa wamoja, bila kujali rangi, imani ya dini, jinsia, asili ya mtu au itikadi ya kisiasa,” amesema Dk Mwinyi.
Amesema jambo hilo litazingatiwa katika uteuzi wa viongozi na watendaji wa utumishi wa umma pamoja na kuwapatia fursa mbalimbali wananchi wote.
“Nitaheshimu maridhiano na nipo tayari kuyatekeleza na kutengeneza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,” amesema Dk Mwinyi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka, 1984 kupitia marekebisho ya mwaka 2010, ibara ya 39 (3), kifungu kidogo (1), Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, atateuliwa iwapo chama chake kitapa asilimia 10 au zaidi ya kura za urais.
Katika uchaguzi mkuu ulifanyika Oktoba 29, 2025, ukishindaniwa na wagombea 11, mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Mwinyi alishinda kiti hicho kwa kura 448,892 sawa asilimia 74.8 akifuatiwa na Othman aliyepata kura 139,399 (asilimia 23.22).
Kwa matokeo hayo, CCM na ACT- Wazalendo ndiyo vyama vyenye sifa ya kuunda SUK, ACT- Wazalendo kikiridhia kuingia serikalini, kitapata nafasi za makamu wa kwanza wa Rais pamoja na mawaziri kadhaa.
Alipoulizwa kuhusu msimamo wa ACT-Wazalendo yenye vigezo vya kuunda SUK, Katibu wa Itikadi, Habari na Mawasiliano kwa Umma, Salim Bimani amesema wataeleza msimamo wao katika mkutano na vyombo vya habari unaotarajiwa kufanyika kesho Novemba 11, 2025 makao makuu ya chama hicho Unguja, Zanzibar.
Akizungumzia utumishi wa umma, Dk Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya watumishi kwa kuwapatia mafunzo, vifaa vya kufanyia kazi na kuongeza masilahi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.
“Katika kipindi hiki tutaimarisha uzalendo, nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma kwa kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi wa tabia, uadilifu na utendaji,” amesema.
Pia, amesema Ofisi ya Usalama wa Shughuli za Serikali (GOS) itakuwa chombo kikuu cha uratibu na ufuatiliaji wa nidhamu serikalini, ikihakikisha kuwa, uwajibikaji na uadilifu vinakuwa na utamaduni wa kudumu katika utumishi wa umma.
Amesema Serikali itaendelea na jitihada za kukabiliana na vitendo vya vyote vinavyoathiri utekelezaji wa msingi ya utawala bora ikiwamo rushwa, uhujumu uchumi na ukiukwaji wa madili ya utumishi wa umma.
“Tutahakikisha viongozi wote katika utumishi wa umma wanazingatia sheria na maadili ya utumishi wa katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa Sheria na Maadili ya Viongozi wa Umma.
“Ni dhahiri kwamba, kufanikiwa kwa dhamira ya Serikali kuwa na utumishi wa umma bora, wenye nidhamu na uwajibikaji kunategemea mchango wa kila mmoja wetu, naomba waheshimiwa wawakilishi na wananchi wote mniunge mkono katika kufikia dhamira hii,” amesema.
Dk Mwinyi amesema katika kipindi cha pili, Serikali yake itaongeza jitihada za kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu ili kuchochea kasi ya ukuaji uchumi.
“Serikali imedhamiria kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Zanzibar kutoka watalii 800,000 hadi watalii 1.5 milioni sambamaba na kuongeza wastani wa matumizi ya siku kwa mtalii kutoka Dola za Marekani 418 hadi Dola 506 kwa siku na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Pemba kutoka 200,000 hadi 300,000 kwa mwaka,” amesema.
Amesema watajenga bandari kubwa mbili za uvuvi za eneo la Ngalawa na Unguja na Shumba Mjini Pemba na kununua meli kubwa za uvuvi.
Katika hotuba yake, Dk Mwinyi amesema kwa kuzingatia umuhimu wa sekta za kilimo kwa maendeleo na ustawi wa uchumi, upatikanaji wa chakula na kipato cha wananchi wengi wa Zanzibar hasa wanaoishi vijijini, Serikali ina dhamira ya kuongeza uzalishaji na huduma katika sekta za kilimo ikiwamo kufanya mageuzi yanayozingatia matumizi ya teknolojia ya kisasa.
“Serikali itaanzisha hifadhi ya Taifa ya chakula kwa kukarabati maghala manne na kujenga vihenge (silos) kuhifadhi tani 60,000 kwa wakati mmoja,” amesema Dk Mwinyi.
Ameongeza kuwa, Serikali itaanzisha mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha usajili na usimamizi wa vyama vya ushirika, kupata masoko ya uhakika na kuhamasisha vyama kununua hisa katika Benki ya Ushirika Tanzania.
Dk Mwinti amesema, Serikali itajenga Barabara ya Tunguu – Makunduchi yenye urefu wa kilometa 48, Fumba – Kisauni kilometa 12, Mkoani – Chake Kilometa 43.5 na barabra za utalii Nungwi, kilometa 12.
Dk Mwinyi amesema katika kipindi hicho, pia wana mipango ya kuongeza idadi ya abiria wanaotumia viwanja vya ndege kutoka 2.140 milioni hadi kufikia abiria 2.824 milioniili kuongeza kipato na ajira.
Kwa upande wa mipango miji, nyumba na makazi, amesema wataendelea kukamilisha ujenzi wa nyumba za makazi 4,715 katika maeneo ya Chumbuni.
“Tutaandaa sera maalumu ya makazi bora yenye kufuata mpangilio na kupendezesha miji yetu, tutaandaa mpango bora wa matumizi ya ardhi na kuongeza asilimia ya watu wanaoishi katika makazi yanayofuata mipango miji kutoka asilimia 18 ya mwaka 2025 hadi asilimia 40,” amesema.
Fursa za ajira kwa vijana
Kiongozi huyo amesema anatambua uwepo wa uhitaji mkubwa wa ajira kwa wananchi, hivyo Serikali itaendelea kukuza ujuzi wa vijana watakaopewa mafunzo kazini na taaluma kwa kuwajengea uwezo wa kujiajiri.
Amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Uwezehaji Wananchi kiuchumi (ZEEA) itatoa mikopo ya Sh100 bilioni pamoja na kuwapatia mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa wajasirimali.
Dk Mwinyi amesema Serikali itatilia mkazo wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kuongeza kasi ya maendeleo kiuchumi na huduma za jamii.
“Serikali itaimarisha mazingira ya uchumi wa kidijitali na kuongeza upatikanaji wa teknolojia mpya, itaimarisha uwekezaji katika miundombinu ya Tehama na kujenga vituo vya teknolojia vinavyokidhi viwango vya kimataifa na kuanzisha majukwaa ya mtandaoni,”amesema.
Pia, amesema Serikali itaimarisha uchumi wa kidijitali kwa kuzingatia thamani yake kama nyenzo muhimu kwa ustawi wa sekta nyingine, utoaji wa huduma na uendeshaji wa shughuli za Serikali.
Amesema shughuli za utafiti na ubunifu zitapewa msukumo ili kuchochea ufanisi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Kwa kuzingatia ukuaji wa uchumi ni chachu ya kuleta maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi, amesema Serikali katika kipindi chake cha pili, itahakikisha ukuaji wa uchumi unafungamana na uimara wa sekta za uzalishaji, kuwepo kwa fursa za uwekezaji, upatikanaji wa mitaji na ushirikishwaji wa sekta binafsi.
“Pamoja na mambo mengine, Serikali itachukua hatua kudhibiti mfumuko wa bei kuwa chini ya asilimia tano kwa mwaka na kuongeza ukuaji wa pato Taifa kutoka asilimia saba hadi kufika asilimia 10 kwa mwaka na kuzalisha ajira 350,000 na kuongeza kipato cha mwananchi,” amesema Dk Mwinyi.