Maaskofu walilia amani inayozingatia haki

Dar es Salaam. Viongozi wa Kanisa Katoliki nchini wametoa wito wa kuendelea kufanywa maombi, kujitathmini kama taifa, na kusisitiza amani itakayozingatia haki, ili kuepuka kujeruhi na kupoteza heshima ya Taifa kutokana na vurugu na machafuko.

Msisitizo wa viongozi hao wa kiroho ni kuwepo hali ya kukubali ukweli kwamba zipo sababu za msingi zilizoifikisha hatua hiyo, hivyo lazima watafutwe wadhamini wenye uelekeo na utayari wa toba ili kujua kiini cha tatizo na kutoruhusu baadhi ya watu kutumia fursa za machafuko hayo.

Wito wa viongozi hao unakuja siku chache baada ya matukio ya vurugu yaliyotokana na maandamano katika mikoa mbalimbali nchini, yaliyosababisha uharibifu wa mali za umma na binafsi, kujeruhi, na kupoteza uhai wa watu.

Kauli hizo zimetolewa katika misa za kuwaombea walioathirika na vurugu hizo, wakiwamo waliopoteza maisha, hasa ukizingatia kwamba katika kalenda ya Kikatoliki, huu ni mwezi wa kuwaombea marehemu wote.

Katika misa ya kuwaombea marehemu iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu Dar es Salaam leo, Jumatatu Novemba 10, 2025, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Juda Thadeus Ruwa’ichi, amesema yaliyotokea wakati wa uchaguzi Oktoba 29, 2025, yamelijeruhi na kupoteza heshima ya Taifa.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Juda Thadeus Ruwa’ichi



Amesema sio tu taifa limepoteza heshima, bali pia raia waliouawa kiholela.

“Katika simulizi zinazoendelea, wapo watu waliouawa wakiandamana, lakini adhabu ya kuandamana sio kifo cha risasi.

“Wapo waliouawa wakiwa majumbani mwao, hilo halionyeshi sura ya Tanzania hata kidogo, na halina maelezo. Msamaha ni chukizo mbele za Mungu,” amesema.

Katika mahubiri yake, Askofu Ruwa’ichi amesema Tanzania imepoteza muono wa haki na mara nyingi, katika mazungumzo aidha kwa makusudi au ujinga, watu wamekuwa wakizungumza kuhusu amani na kuiacha haki.

Amesema hakuna amani bila haki, na watu wanapaswa kufahamu kuwa haki ni msingi wa lazima wa amani.

Kuhusu heshima, Askofu Ruwa’ichi amesema ni wasifu wa Mungu, na binadamu mwadilifu anatazamiwa kuwa na hekima akihoji kama Watanzania wana hekima.

Akinukuu kitabu cha Injili, amesema, “Yesu anafundisha juu ya makwazo, na atakayemkwaza mmoja wa wadogo ni afadhali afungwe jiwe kiunoni na kutumbukizwa baharini.

“Hivyo, kwa maneno mengine, anayejiruhusu kushabikia au kufanya makwazo ni chukizo mbele za Mungu.

“Kwa hiyo ndugu zangu, tunapoadhimisha misa ya kuwaombea ndugu, jamaa, marafiki, na raia wenzetu waliouawa wiki ya uchaguzi, tuombe Mungu atuhurumie na atujalie hekima na utayari wa kutenda haki na kuwa wakweli,” amesema askofu huyo.

Askofu Mkuu wa kanisa Katoliki Jimbo kuu Mbeya, Gervas Nyaisonga akizungumza wakati wa ibada maalumu ya kuwaombea waliopoteza maisha na kujeruhiwa wakati na baada ya uchaguzi mkuu



Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga, amesema uamuzi wa kufanya ibada hiyo umebebwa na dhamira sita zinazohusiana na matukio ya wakati na baada ya uchaguzi.

Amezitaja dhamira hizo ni kuwaombea marehemu, kuwaombea majeruhi, kumuomba Mungu asaidie jitihada kuwapata waliopotea, wawe hai au wamekufa, kuwapa pole waliopoteza mali zao, kutoa rai ya kujitathimini, na kuomba uponyaji kutoka kwa Mungu.

Ameeleza matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi yaliposababisha vurugu, mauaji, majeruhi, na uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Amesema miongoni mwa maeneo yaliyoathirika ni Mkoa wa Mbeya na Songwe, ndio maana kanisa hilo limeamua kuwaombea waliopoteza maisha, kujeruhiwa, na walioathirika na matukio hayo.

“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kumetokea vifo vya wenye hatia na wasio na hatia, wamo watoto, vijana na wazee, wanawake na wanaume, raia na askari. Novemba 4, nimeshuhudia wingi wa watu waliokuwa wakinunua majeneza, misafara ya magari ikisafirisha misiba kwenda nje ya Mbeya,” amesema Nyaisonga.

Kutokana na matukio hayo kuwa mengi kwa wakati mmoja na haijulikani nani apewe pole au nani aachwe, amesema misa hiyo imelenga kutoa pole kwa ujumla kwa waliofikwa na madhila yoyote.

Akitumia maneno ya wasanii wa kundi la Msondo Ngoma, walioimba, “Ukiona mtu mzima analia jua kuna jambo” na “Tunatoana roho kwa mali alizoacha baba,” amesema wimbo huo uwekwe kwa muktadha wa Taifa.

Amesema kabla na wakati wa uchaguzi mkuu, watu kadhaa waliripotiwa kupotea kwa mazingira ya kutatanisha na yasiyojulikana, akieleza kuwa wanaomba Mungu asaidie wapatikane kwa mazingira yoyote.

“Tumeshuhudia upotevu na uharibifu wa mali za umma na binafsi, tunawapa pole kwa hasara mbalimbali. Mungu ameleta hili ili tugutuke kutoka usingizini, kutusahaulisha mambo ya msingi.

“Tunatoa mwaliko wa kujitathimini, nchi yetu ilionekanaje wakati moto ukiwaka maeneo mbalimbali… hata mbinguni walishangaa, barabara na madaraja yanajengwa, huduma zinatolewa, lakini unajiuliza kwa nini tufikie hatua hii mbaya?” amehoji.

Katika mahubiri yake, ameongeza: “Lakini yote hayo unaweza kusema labda wanaofanya hivi hawaoni mazuri, labda ni maadui, chuki binafsi, au wanatoka nje, labda labda zitakuwa nyingi, ila ukitafakari, sidhani kama wahuni wanaweza kujitokeza kwa wingi wakati mmoja, hata wahuni hawawezi kufa kwa sababu za kijinga.”

Amesema lazima kukubali kuwa zipo sababu za msingi hadi kufikia hatua hiyo, na kwamba lazima kutafuta wadhamini safi wenye uelekeo na utayari wa toba ili kujua kiini cha tatizo na kutoruhusu baadhi ya watu kutumia fursa za machafuko nchini.

“Tunaomba Mungu aliponye Taifa letu na kuliepusha na migogoro, atuponye sote. Kwa unyenyekevu niwaombe wafiwa wasamehe na wawe tayari kuanza upya kama wajasiri kujenga upya, kwa faida ya waliopo na wajao,” amesema askofu huyo.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Amani



Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Amani, ametoa wito kwa Watanzania kuungana katika maombi, kufunga, na kutafakari kwa kina, kufuatia vurugu zilizoshuhudiwa nchini wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kupitia waraka maalumu alioutoa Novemba 7, 2025, Askofu Amani ameeleza masikitiko yake kutokana na vifo, majeruhi, na uharibifu uliotokea katika miji mbalimbali, akisema hali hiyo imetikisa taswira ya taifa ambalo kwa muda mrefu limekuwa mfano wa amani barani Afrika.

“Yaliyotokea siku hiyo yametushangaza na kushangaza ulimwengu, Tanzania ilizaliwa upya kwa huzuni. Nawaalika waamini wote tusali tukiwaombea waliopoteza maisha, waliojeruhiwa, na wale waliopoteza wapendwa wao,” amesema.

Askofu huyo amesema vurugu hizo zimeacha majeraha ya kimwili na kisaikolojia kwa waathiriwa wengi, wakiwamo watoto walioshuhudia vitendo vya kikatili majumbani mwao.

Ameeleza kuwa taifa linapaswa sasa kuomba uponyaji na faraja ya Mungu, huku likijitafakari kama jamii yenye heshima kwa uhai na utu wa mtu.

“Watoto waliokuwa mashahidi wa umwagikaji wa damu watahitaji uponyaji wa rohoni; tuwaombee, maana Tanzania inaomboleza, kama alivyolia Nabii Yeremia akisema, ‘Sauti imesikiwa Rama, kilio na maombolezo mengi,’” amesema akirejea Yeremia 31:15.

Askofu Amani ametumia maandiko ya Biblia kumkumbusha kila Mtanzania kuhusu onyo alilompa Mungu Kaini, akisema vurugu za uchaguzi zimeonesha jinsi ghadhabu na uhasama vinavyoweza kuangamiza udugu wa taifa.

“Tumeacha udugu, tukaangamizana. Kaini hakumsikiliza Mungu, bali alimwinukia nduguye akamuua. Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka ardhini,” amenukuliwa akisema.

Katika waraka wake huo, Askofu huyo amewataka viongozi wa dini na wananchi wote kuendeleza sala ya “Tanzania Haki na Amani,” akiwasihi wasichoke kuomba hadi Mungu ajibu kwa wakati wake.

Pia ameomba Watanzania kujitafakari upya kuhusu wajibu wao wa kulinda utu, haki, na thamani ya uhai, akisema:

“Hakuna mwenye haki ya kumwumiza au kumuua mwingine, uhai wa mwanadamu ni mtakatifu na unapaswa kulindwa kwa gharama yoyote,” amesema.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila



Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila, amesema binadamu wote wameumbwa kwa sura ya Mungu, kwa hivyo wauaji na waliouawa wote wana sura hiyo ya uumbaji.

“Ni lazima tuwapate watetezi, watetezi wazuri kabisa ni ninyi makatekista. Waeleze watu maana ya uhai, kazi kuu ya uhai ni kumtukuza Mungu na kumtetea. Tumeumbwa kwa sura na mfano wake,” amesema.

Aidha, Askofu Msonganzila amesema matukio ya mauaji vinavyoripotiwa wakati wa uchaguzi yapo sehemu mbalimbali nchini.

“Ingawa mkoa wa Kagera hakukumbwa na shida kubwa, kuna maeneo mengine ambapo watu wameuawa kwa wingi,” amesema.

Ameongeza kuwa kuonekana kwa vitendo hivyo ni matokeo ya dhambi na kupuuza thamani ya uhai, zawadi ni kila mtu anayoipata bila kuomba au kuulizwa.

“Hatuna silaha, yetu ni neno la Mungu. Usiue tena, usiue. Naomba mtafsiri andiko hili kwa watu,” amesema.

Imeandikwa na Baraka Loshilaa, Juma Issihaka (Dar), Janeth Mushi (Arusha), na Saddam Sadick (Mbeya).