Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limewaachia kwa dhamana viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwemo John Heche ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara.
Kwa mujibu wa wakili wao, Hekima Mwasipu, dhamana hiyo inawataka viongozi hao walioachiwa jioni ya leo Jumatatu, Novemba 10, 2025 kuripoti kesho Jumanne saa tano asubuhi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.
“Ni kweli wameachiwa kwa dhamana viongozi hao na wanapaswa kuripoti kesho ya saa tano asubuhi Kituo cha Polisi cha Kati,” amesema Mwasipu alipokuwa akizungumza na Mwananchi.
Mbali na Heche, wengine ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa, Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema na Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai.
Lema, Golugwa na Boni Yai ni miongoni mwa waliokamatwa hivi karibuni na Polisi ambalo lilidai wanahusika dhidi ya maandamano yaliyozaa vurugu kabla na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Songwe, Kilimanjaro, Dodoma, Mara na Ruvuma.
Heche alikuwa anashikiliwa na Polisi tangu Oktoba 22, 2025, alipokamatwa nje ya geti la Mahakama Kuu Dar es Salaam, alipokuwa akienda mahakamani, kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini.