Dar es Salaam. Wakati makali ya upandaji wa bei kwa bidhaa mbalimbali za vyakula ikianza kupoa kwenye masoko ya jijini Dar es Salaam, bei ya nyama na tangawizi imeendelea kuwa juu kwenye maeneo mengi.
Mfumuko wa bei uliibuka baada ya maandamano yaliyosababisha vurugu za Oktoba 29, 2025 zilizotokea kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo Dar es Salaam, hali iliyosababisha vyakula kuadimika huku kwenye maeneo mengi bei zikipanda na watu kulazimika kununua kwa foleni katika baadhi ya maeneo.
Wakati wa vurugu hizo jijini Dar es Salaam, kilo moja ya nyama iliuzwa Sh15,000 hadi Sh20,000.
Huku kuku wa nyama wakiuzwa hadi Sh13,000 kwa mmoja katika maeneo mengi kutoka Sh6,500 hadi Sh7,000 na bei ya unga ikifika Sh1,800 hadi Sh2,000 kwa kilo kutoka Sh1,400.
Bidhaa za viungo ikiwamo nyanya ilifika Sh12,000 kwa sado, wakati kilo moja ya hoho ilifika hadi Sh5,000 huku sado ya viazi mviringo ikifika Sh10,000.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi katika masoko ya Mabibo, Tandale, Urafiki na Ilala leo Jumatatu, Novemba 10, 2025 ikiwa imepita wiki moja tangu kurejea kwa shughuli za kiuchumi na kijamii Novemba 4, wameeleza kupoa kwa bei katika baadhi ya bidhaa licha ya nyama na tangawizi kutoshuka kama ilivyokuwa awali.
Novemba 3, 2025 Serikali ilitangaza kuanzia Novemba 4 shughuli za kijamii na uchumi ziendelee, hali iliyosaidia kurejesha unafuu katika maeneo mengi ikiwamo ya upatikanaji wa chakula.
Mwananchi imezungumza na baadhi ya wafanyabiashara ambao wameeleza bei ya bidhaa za vyakula kupoa kwa siku za karibuni tofauti na ilivyokuwa wakati wa vurugu.
Mfanyabiashara wa tangawizi katika soko la Mabibo, Rajabu Juma amesema hata baada ya maisha kuendelea kama awali, bei ya tangawizi haijashuka zaidi.
“Tangawizi ilifika hadi Sh7,000 kwa kilo, kutoka Sh3,000 wakati wa vurugu, utulivu uliporejea imeshuka hadi Sh4,500,” amesema.
Mbali na tangawizi, bei ya nyama katika mabucha mengi ya mtaani ilipanda hadi Sh 20,000 na baada ya utulivu kurejea imeshuka na kufika Sh12,000 hadi Sh14,000, ikiwa haijashuka sana.
Kabla ya vurugu mabucha mengi yaliuza Sh11,000 hadi Sh14,000 kwa kilo moja.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa nyama machinjio ya Vingunguti, Joel Meshack amesema wakati wa vurugu katika machinjio hiyo kilo moja ilifika Sh15,000.
“Hivi sasa inauzwa Sh10,000 hadi Sh11,000,” amesema Meshack. Akifafanua kabla ya vurugu za Oktoba 29, waliuza Sh10,000 kwa kilo moja.
Bei ya kuku katika soko la Urafiki hivi sasa ni Sh7,000 hadi Sh7,500, ikiwa imeshuka kutoka Sh10,000 wakati wa vurugu.
Mfanyabiashara kwenye soko hilo, Mwita Daniel amesema wakati wa vurugu bei ilifika hadi Sh10,000 kwa kuku mmoja huku mtaani akiuzwa hadi Sh13,000.
“Hivi sasa bei imeshuka, hapa sokoni kuku wa kisasa kwa sasa ni Sh7,500 mpaka Sh7,000, wakati wa vurugu gharama za usafiri zilikuwa juu, hivi sasa imerudi kawaida ndio sababu na bei imeshuka,” amesema.
Mfanyabiashara wa vitunguu kwenye soko la Ilala, Naima Mussa amesema wakati wa vurugu kiungo hicho hakikupanda bei.
“Kilisalia Sh1,500 kwa kilo, bei ambayo ndiyo tunayouza hadi sasa,” amesema.
Kwenye hoho amesema ilifika hadi Sh5,000 kwa kilo ingawa sasa imerudi kwenye bei ya kawaida ya Sh2,000 wakati wa vurugu huku karoti pia ikiuzwa Sh1,500 kutoka Sh3,000.
“Nyanya pia zimeshuka, wakati wa vurugu tuliuza hadi Sh12,000 kwa sado hivi sasa zimerudi kwenye bei ya kawaida ya Sh4,000,” amesema.
Mfanyabiashara wa viazi mviringo kwenye soko la Mabibo, Qureish Talik amesema sado hivi sasa inauzwa Sh4,000 kutoka Sh10,000 iliyouzwa wakati wa vurugu.
“Ndoo ilifika Sh35,000 kutoka Sh17,000 ingawa sasa bei ya awali imerejea.
Amesema wakati wa vurugu bidhaa zilizouzwa kwa bei nafuu katika soko hilo ilikuwa ni matunda.
“Hayakuwa na soko, haswa maparachichi ambayo wakati wa vurugu yaliuzwa Sh700 hadi Sh800 kwa moja ambapo hivi sasa ni Sh2,000.
“Vurugu vilipoanza ndicho kipindi ambacho malori yalikuwa yameleta matunda kwa wingi, hivyo yalikuwa mengi,” amesema.
Amesema bidhaa nyingine kama nyanya, hoho na karoti zilikuwa hazijaletwa, hivyo tangu vurugu za Oktoba 29, zile zilizokuwepo sokoni ndiyo ziliendelea kuuzwa kutokana na magari kutoweza kuleta bidhaa nyingine.
Katika soko la Tandale, mfanyabiashara wa mchele na unga, Rukia Shaban amesema mchele katika soko hilo uliuzwa Sh2,300 mpaka Sh3,000, kulingana na ubora.
“Hiyo ilikuwa ni kabla ya vurugu, hata wakati wa vurugu na baada bei imeendelea kusalia hivyo hivyo hadi sasa.
“Unga ndio ulipanda kufika Sh1,800 hadi 2,000 kwa kilo moja, lakini sasa umerudi hadi Sh1,400 kwa kilo,” amesema.