‎Watuhumiwa 227 Ilemela, Arusha washtakiwa kwa uhaini, Jamhuri yabanwa kwa hoja nne

‎Mwanza/Arusha. Watuhumiwa 227 waliokamatwa wilayani Ilemela mkoani Mwanza na Arusha kutokana na vurugu zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, wameshtakiwa kwa makosa ya kula njama na uhaini.

Mawakili 37 kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Mwanza wamejitolea kuwatetea washtakiwa wote wenye kesi za namna hiyo.

Washtakiwa hao wamesomewa hati ya mashtaka yanayowakabili leo Jumatatu Novemba 10, 2025 kwa nyakati tofauti kuanzia saa 7 mchana hadi saa 10 jioni katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela iliyopo kwenye Kituo Jumuishi cha utoaji haki, Buswelu.‎

‎Kati ya watuhumiwa hao 114 ni wa Ilemela Mwanza na 113 ni wa Arusha. Washtakiwa wa Mwanza wamesomewa mshtakiwa yao katika kesi tatu tofauti, ambapo kesi ya kwanza inawahusu watuhumiwa 22, kesi ya pili watuhumiwa 64 na kesi ya tatu watuhumiwa 28.

Kesi hizo zimesomwa kwa nyakati tofauti mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Christian Mwalimu na Stella Kiama wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela. ‎

‎Katika kesi hizo, upande wa Jamhuri umeongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwanahawa Changale na Safi Amani wakisaidiwa na Adam Murusuli.

Upande wa utetezi umewakilishwa na mawakili tisa kutoka TLS wakiongozwa na Erick Mutta, Angelo Nyahoro, Deborah Marwa, Lugano Kitangalala, Stella Sangawe, Benson Bernad, Said Juma Said, Sijaona Revocatus, na Justine Kadaraja.‎

‎Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote juu ya mashtaka yao kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri lao. Pia, makosa yote hayana dhamana hivyo watakuwa rumande wakati upelelezi ukiendelea mpaka itakapoitwa tena.‎

‎Kesi hizo zimeahirishwa hadi Novemba 24, 2025 zitakapotajwa tena.‎

‎Katika shauri la kwanza namba 26565/2025 ambalo limesomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Christian Mwalimu likiwahusisha watuhumiwa 22, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwanahawa Changale amesema washtakiwa wote wanashtakiwa kwa kosa la kula njama za kutenda kosa (uhaini) kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 urekebu wa mwaka 2023.‎

‎Ambapo kati ya Oktoba 28 na 29, 2025 katika maeneo tofauti mkoani Mwanza, washtakiwa walikula njama na kutenda kosa la uhaini.‎

‎Wakili Changale amesema katika shtaka la pili linalowakabili washtakiwa wa kwanza hadi 17 (Said Hamza na wenzake) wanaoshtakiwa kwa kosa la uhaini kinyume na kifungu cha 39 (2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 urekebu wa mwaka 2023. ‎

‎Amesema Oktoba 29, 2025 katika eneo la Nyasaka Buzuruga wakiwa na nia ovu ya kuvuruga uchaguzi mkuu na kusudi la kutishia mamlaka waliharibu mali za Jamhuri zinazotoa huduma hizo.‎

‎Katika shtaka la tatu linalowakabili mshtakiwa wa 18 hadi 22, watuhumiwa wanashtakiwa kwa kosa la uhaini kinyume na kifungu cha 39 (2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 urekebu wa mwaka 2023.‎

‎Kesi ya pili namba 26641/2025 inayowahusisha watuhumiwa 64 (Fredy Malebele na wenzake 63) ambayo imesomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Stella Kiama wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, upande wa Jamhuri umeongozwa na mawakili wa Serikali waandamizi, Safi Amani na Mwanahawa Changale wakisaidiwa na wakili wa Serikali, Adamu Murusuli.‎

‎Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Adamu Murusuli amesema washtakiwa wote 64 wanakabiliwa na makosa mawili ya kula njama kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 urekebu wa mwaka 2023 ambapo Oktoba 28, 2025 katika maeneo tofauti mkoani Mwanza waliunda genge la uhalifu kwa nia ya kutenda uhalifu wa uhaini.‎

‎Katika shtaka la pili, watuhumiwa wote 64 wanashtakiwa kwa kosa la uhaini ambalo walilifanya kinyume na kifungu cha 39 (2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 urekebu wa mwaka 2023.‎

‎Ambapo Oktoba 29, 2025 katika maeneo ya Pasiansi, Kona ya Bwiru, Kitangiri, na Kirumba wilayani Ilemela, Mwanza watuhumiwa waliunda nia ya kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa nia ya kuitisha Serikali na kuunda nia ya kutaka kutekeleza kwa kuharibu mali za Serikali.‎

Hata hivyo, ‎katika mashauri yote, upande wa utetezi umeibuka na hoja nne ambazo imeomba Mahakama ielekeze Jamhuri izifanyie kazi kwa haraka kabla ya tarehe nyingine itakayopangwa ya kutajwa kwa shauri hilo.‎

‎Wakili wa utetezi, Lugano Kitangalala ameiomba Mahakama iwaelekeze Jamhuri na wanaosimamia mahabusu kwa watuhumiwa wenye mahitaji ya matibabu, Jeshi la Magereza liwapatie matibabu na wale ambao hawana nguo na viatu pia wapatiwe.‎

‎”Watuhumiwa tisa wana majeraha ya vidonda vibichi ambayo wanalalamika kuwa walipigwa na polisi wakati wa kuandika maelezo, wengine sita hawana viatu wameletwa wakiwa kwenye mavazi ambayo tunaona siyo sahihi, tunaomba Mahakama iamuru wapatiwe vitu hivyo,” amesema Kitangalala.‎

‎”Pia ambao hawana vidonda lakini wanalalamika kuwa na maumivu ambayo yametokana na kupigwa, waruhusiwe kumuona daktari na ripoti iletwe mahakamani.”‎

‎Naye Wakili wa utetezi, Justine Kadaraja amesisitiza kwa kuiomba Mahakama itoe maelekezo kwa Jeshi la Magereza kuwachukulia washtakiwa kama binadamu kwa mujibu wa Katiba kwa sababu bado ni watuhumiwa, pia liwaruhusu ndugu zao wawapelekee vitu mbalimbali.‎

‎”Tunaomba wapewe haki zao za msingi ambazo ziko kikatiba kwa sababu bado hawajathibitishwa kutenda kosa,” amesema Kadaraja.‎

‎Ameomba Mahakama iwaelekeze mawakili wa Serikali (Jamhuri) kuharakisha upelelezi ili ukamilike kwa wakati kwa sababu washtakiwa wamekaa ndani kwa takribani siku 13 tangu Oktoba 29, 2025 bila ya kujua hatima yao, jambo ambalo kwa mujibu wa Sheria za kimataifa ni unyanyasaji wa kisaikolojia (Psychological torture).‎

‎”Tunaomba kutokana na unyeti wa kesi hii na ilivyokuwa na mashiko kwa umma wasicheleweshe kutafuta ushahidi na tutakapokutana tena hapa tuwe tumepiga hatua kubwa,” amesema Kadaraja.

‎‎Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili katika kesi ya kwanza, Hakimu Mkazi Mkuu, Christian Mkuu amemuagiza Mkuu wa Gereza la Butimba kuhakikisha washtakiwa tisa wanapelekwa hospitalini na ripoti za kitabibu ziwasilishwe mahakamani siku ya kutajwa kesi.‎

‎Pia aweke utaratibu utakaowawezesha washtakiwa kupata haki ya kupewa mavazi na viatu.‎

‎”Washtakiwa wakiwa Magereza wana haki ya kutembelewa na ndugu na mawakili wao kwa taratibu za gereza. Pia, Jamhuri inaagizwa kuharakisha uchunguzi na kutoa taarifa ya mwenendo kila shauri litakapokuwa linatajwa,” amesema Mwalimu.‎

‎Naye, Hakimu Mkazi Mkuu, Stella Kiama katika kesi ya pili katika uamuzi wake amesisitiza watuhumiwa wanapaswa kupata haki zao wakiwa chini ya uangalizi wa vyombo vya usalama, huku akiliagiza Jeshi la Magereza kusimamia utaratibu wa watuhumiwa kuonana na ndugu zao chini ya utaratibu uliowekwa.‎

‎”Mahakama imeelekeza kwamba taratibu za kukagua afya za watuhumiwa ufanywe chini ya utaratibu wa magereza. Taratibu za Magereza zifuatwe ili kuhakikisha watuhumiwa wanapata haki za,” amesema Hakimu Kiama.‎

‎‎Makamu Mwenyekiti wa TLS chapta ya Mwanza, Erick Mutta amesema mawakili 37 kutoka kwenye chama hicho mkoani humo wamejitolea kuwatetea watuhumiwa wote waliofunguliwa kesi kwa makosa yaliyotokana na matukio yaliyotokea kati ya Oktoba 29, 30, na 31 baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.‎

‎Mutta ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 10, 2025 baada ya kuwaongoza mawakili tisa kuwawakilisha watuhumiwa 114 waliosomewa mashtaka ya uhaini leo katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.‎

113 Arusha kizimbani kwa uhaini

Huko mkoani Arusha, watuhumiwa 113 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakikabiliwa na makosa ya kula njama ya kutenda kosa na uhaini.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani Novemba 7, 2025 katika Mahakama hiyo katika kesi tatu tofauti.

Kesi ya kwanza inawakabili washtakiwa 21, kesi ya pili washtakiwa 39 na kesi ya tatu washtakiwa 53.

Katika kesi ya kwanza namba, 26514/2025, washtakiwa 21, wameshtakiwa kwa kosa la kula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Ilidaiwa mahakamani hapo kwa tarehe tofauti kati ya Oktoba 1 hadi 29, 2025, walifanya njama mbalimbali za kutenda kosa la uhaini.

Katika kesi ya pili namba 26534/ 2025 inayowakabili washtakiwa 39 ni kula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Ilidaiwa kwa tarehe tofauti kati ya Oktoba mosi hadi 29, 2025, walifanya njama mbalimbali za kutenda kosa la uhaini.

Katika kesi hiyo, kosa la pili linalowakabili washtakiwa hao ni uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Wanadaiwa Oktoba 29, 2025 wakiwa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Arusha wakiwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikusudia kuzuia au kuharibu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa nia ya kuitisha Serikali na walidhihirisha nia hiyo kwa kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.

Kesi ya tatu namba 26512/2025 inayowakabili washtakiwa 53 ambao wanakabiliwa na makosa mawili la kwanza likiwa ni kula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Wanadaiwa katika kwa tarehe tofauti kati ya Oktoba mosi hadi 29, 2025, walifanya njama mbalimbali za kutenda kosa la uhaini.

Katika kesi hiyo, kosa la pili linalowakabili washtakiwa hao ni uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Washtakiwa hao wanadaiwa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, walikusudia kuzuia au kuharibu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kwa nia ya kuitisha Serikali na kwa kudhihirisha nia hiyo walifanya vitendo vya vurugu vilivyosababisha uharibifu mkubwa mali za Serikali, zilizokuwa zikitoa huduma muhimu kwa wananchi.

Kesi zote zimeahirishwa hadi Novemba 19, 2025 zitakapotajwa tena mahakamani hapo.