Dar/Dodoma. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akifanya uteuzi wa wabunge sita, Bunge la 13 linaanza rasmi kesho Novemba 11, 2025, likiwa limebeba mzigo wa kurejesha imani ya Watanzania.
Bunge hilo linaundwa na wabunge 272 waliochaguliwa majimboni, wabunge 115 wa viti maalumu pamoja na wabunge sita walioteuliwa na Rais Samia leo Novemba 10, 2025, kwa mujibu wa Katiba inayompa mamlaka ya kuteua wabunge 10.
Hili ni Bunge linaloshuhudia kuwa na wabunge wachache zaidi kutoka vyama vingine nje ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwa mara ya pili hakutakuwa na kambi rasmi ya upinzani kama ilivyokuwa katika Bunge la 12, hii inatokana na idadi yao kuwa ndogo.
Hadi sasa wabunge wa upinzani ni 11 na hata ikitokea upinzani wakashinda majimbo mawili ambayo hayajafanya uchaguzi na kupewa kiti kimoja kutoka viti maalumu ambacho hajateuliwa, bado hawatakidhi takwa la kisheria kuunda kambi hiyo.
Kesho wabunge wateule wataanza kwa shughuli ya kumchagua Spika wa Bunge anayetegemea kupatikana mapema na baada ya kiapo chake mbele ya Katibu wa Bunge, ataanza kuwaapisha wenzake.
Katika uchaguzi huo ambao utasimamiwa na Katibu chini ya uenyekiti wa mbunge mzoefu wa siku nyingi, mgombea wa kiti cha Spika kutoka CCM, Mussa Zungu anapewa nafasi kubwa ya kushinda.
Uzoefu unaonesha kuwa, baada ya viapo vya wabunge wote, Spika atapokea jina moja kutoka kwa Rais, la mtu atakayependekezwa kuwa Waziri Mkuu ili apigiwe kura na wabunge, ndipo siku inayofuata Rais Samia atakwenda viwanja vya Bunge kulihutubia kwa ajili ya kuzindua.
Baadhi ya wachambuzi na wananchi wamesema wabunge hao wanakabiliwa na mtihani wa kuonesha kama chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi kinaweza kujinasua kutoka katika kivuli cha Serikali na kushindwa kuisimamia.
Aidha, wamesema ni kipindi cha kuandika sura mpya ya uwajibikaji, ushirikiano na heshima baina ya mihimili ya dola huku wakirudisha sauti ya wananchi kusikika kupitia ukumbi wa Bunge.
Akizungumzia mwanzo wa safari hiyo ya Bunge, Dk Paul Loisulie, mhadhiri wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ameeleza kuwa, mzigo huo unaanza kuonekana mapema kabla hata shughuli rasmi za Bunge kuanza, kupitia mchakato wa upatikanaji wa Spika.
Mpaka sasa, Mussa Zungu, mgombea wa kiti hicho kutoka CCM, anapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho kutokana na uzoefu wa kihistoria kuwa Naibu Spika, mara kadhaa wamekuwa wakipanda kushika wadhifa huo baadaye.
Dk Loisulie amesema nafasi hiyo ndiyo dira ya mwenendo wa Bunge zima kuwa aina ya Spika atakayepatikana itatoa picha ya aina ya Bunge litakalokuwapo kwa miaka mitano ijayo.
“Bunge hili lina mzigo mkubwa wa kujitofautisha na lililopita, sasa Watanzania wanataka kuona Spika atakayechaguliwa akiwa na uwezo wa kuongoza chombo huru, kinachosikiliza hoja zote kwa uwiano na haki.
“Bunge hili linapaswa kusimama imara katika usimamizi wa Serikali kwa umakini na kuonesha kwa vitendo kwamba, linafanya kazi kwa niaba ya wananchi, si kwa matakwa ya chama au mtu mmoja,” amesema Dk Loisulie.
Amesema dhana hiyo imejengwa kutokana na historia ya muda mrefu iliyoambatana na mabadiliko kadhaa ya kimuundo na kisheria ndani ya chombo hicho, tangu kilipoanzishwa mwaka 1962, kikitambulika kama Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika.
Amesema tangu wakati huo, Bunge limepitia mageuzi makubwa, likiimarishwa zaidi baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 na baadaye Katiba ya mwaka 1977 kuweka msingi wa Bunge la kisasa.
Wakili Alloyce Komba amesema moja ya misingi muhimu ya ujenzi wa Taifa imara ni kuwa na mihimili inayoheshimiana na inayosimamia majukumu yake bila kuingiliana.
“Bunge lina wajibu wa kuishauri vema Serikali, lakini pia kuisimamia kwa kutumia mamlaka yake ya Kikatiba. Heshima ya Bunge haitapatikana kwa maneno, bali kwa vitendo vya kulinda misingi ya uwajibikaji na uwazi kwa Serikali,” amesema.
Wakili huyo amesema wabunge wanatakiwa wasiwe waoga wa kuuliza maswali magumu wala kuhoji uamuzi unaogusa masilahi ya umma.
“Mhimili huu unapaswa kuiwajibisha na kuishauri vema Serikali katika uendeshaji wa nchi,” amesisitiza Komba.
Kwa upande wa wananchi, wengi wametaka kuona Bunge likibadilika kutoka taswira ya chombo cha wanasiasa kwenda kuwa sauti halisi ya wananchi.
Kasembo Ngagi, mkazi wa Dar es Salaam, anaamini kuwa heshima ya Bunge itarejea endapo wabunge watajua kuwa, uamuzi wao unaathiri maisha ya kila Mtanzania nje ya vyama vyao walivyopitia kufika bungeni humo.
“Bunge linapaswa kuwa na meno, liwe chombo cha kuisimamia na kuiwajibisha Serikali inapokosea na liwe makini kupitisha sheria zinazolinda masilahi ya wananchi wote.
“Wabunge wajue kuwa, wanapoamua ndani ya ukumbi wa Bunge, hawafanyi hivyo kwa niaba ya vyama vyao bali kwa niaba ya Watanzania,” amesema Ngagi.
Mchambuzi wa masuala ya Katiba na siasa, Deus Kibamba amesema Bunge la 13 litakuwa la pongezi kuhusu Serikali, lakini hakutakuwa na sauti.
Kibamba amesema kitendo cha kupungua kwa idadi ya wabunge wa vyama vingine, ni kuminya demokrasia ya Watanzania.
Hata hivyo, ameomba wabunge wa vyama vingine waitwe wabunge shindani si wapinzani.
Kibamba ametaja sababu ya kuwa Bunge lenye uwakilishi hasi kwamba, makundi ya walio wengi hayapo na hivyo hakuna sauti za watu.
Amesema Bunge litakuwa la hofu na shaka kwa watu katika kipindi cha miaka mitano, huku akipendekeza kuwe na uamuzi wa haki na Bunge lidumu miaka miwili kisha waingie kwenye mfumo mwingine.
“Hili litakuwa Bunge bubu, hakuna sauti itakayotoka kwani wengi ni wa kundi la ndiyo, hatuna kambi ya upinzani bungeni wala katika Baraza la Wawakilishi, na wapinzani waliopo ni sawa na vifaranga wasiokuwa na mwangalizi,” amesema Kibamba.
Akizungumzia namna ya kuondoa mkwamo huo, amesema ni wakati wa kiongozi mkuu wa nchi kutoka hadharani na kutangaza msamaha ili viongozi wakutane na kujadiliana namna ya kumaliza hofu.
Hata hivyo, amesisitiza mapendekezo ya uhai wa Bunge kuwa ni miaka miwili ili kubadili mfumo na Taifa lianze majaribio ya matumizi ya Katiba mpya.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Gorvenance Link, Donald Kasongi amesema Bunge linapaswa kuendeshwa kwa weledi, umahiri na ubunifu kuliko ilivyokuwa kwenye mabunge yaliyopita, kwa kusimamia taasisi zote za umma ili ziweze kuwanufaisha wananchi na zionekane kufanya hivyo.
Kasongi amesema Bunge likiendeshwa kwa umahiri, rasilimali zilizopo nchini zitawanufaisha wananchi wote badala ya kuwanufaisha watu wachache hasa zinazohusu maji, madini, utawala bora na rasilimali watu.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amefanya uteuzi wa wabunge sita kwa mamlaka aliyonayo chini ya Ibara ya 66(1)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania inayompa mamlaka ya kuteua wabunge 10.
Taarifa ya uteuzi wa wabunge hao imetolewa leo, Jumatatu Novemba 10, 2025 na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.
Kwa uteuzi huo, zimesalia nafasi nne ambazo Rais anaweza kuzijaza.
Miongoni mwa walioteuliwa ni waliokuwa mawaziri, Dk Dorothy Gwajima (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum) na Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Wengine ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na alikuwa mbunge kwenye Bunge lililopita.
Dk Bashiru, Balozi Kombo na Dk Gwajima wanateuliwa kushika nafasi hizo kwa kipindi cha pili, baada ya awali kuteuliwa kabla ya nyadhifa hizo za ubunge uliokoma mwisho wa Bunge la 12.
Uteuzi huo pia, umemhusisha Dk Rhimo Nyansako ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Yumo Abdullah Ali Mwinyi aliyekuwa mbunge wa Mahonda ambaye kwenye kura za maoni ndani ya CCM alishindwa kutetea jimbo hilo. Uteuzi huo umemhusisha, pia, Balozi Khamis Mussa Omar.