WAKATI Simba ikijipanga na mechi ya kwanza hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda, Kocha Mfaransa, Bruno Ferry anayeinoa Wiliete ya Angola, ametoa faili litakalorahisisha kazi.
Simba iliyopo Kundi D katika michuano hiyo, itaanzia nyumbani Novemba 23, 2025 kucheza dhidi ya Petro de Luanda kutoka Angola kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ferry ambaye aliwahi kuinoa Azam kabla ya sasa kuifundisha Wiliete inayoshiriki Ligi Kuu ya Angola, amesema anawafahamu vizuri wapinzani wa Simba huku akifichua kwamba sio timu nyepesi kabisa.
Ferry amefichua hayo akisema Petro de Luanda yenye pointi 12 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Angola msimu huu ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Wiliete (13) na vinara Clube Recreativo Desportivo do Libolo (16), ni timu ngumu.
“Simba inatakiwa ijipange kwa sababu inakwenda kukutana na timu ngumu kuanzia katikati ya kiwanja na safu ya ulinzi.
“Najua Simba ni ngumu kufungika nyumbani, hiyo ni rekodi ambayo inajulikana Afrika, lakini hawatakiwi kabisa kutoka sare katika mchezo huo muhimu kwani ni wa kwanza unaohitaji kuweka hesabu sawa.”
Ameongeza kuwa: “Kuanzia nyumbani kunaweza kuonekana kama bahati mbaya kidogo ila ni vizuri kama Simba itajipanga vyema, kwani uwanja wanaochezea ni wa bahati kwa upande wao.”
Katika kundi hilo, mbali na Petro de Luanda, pia zipo Esperance de Tunis ya Tunisia na Stade Mallen kutoka Mali.
Rekodi zinaonyesha, Petro de Luanda katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2021-2022 ilifika nusu fainali, kisha 2023-2024 ikakwamia robo fainali, huku 2024-2025 ikikwamia hatua ya pili na kushindwa kufuzu makundi.
Kocha wa kikosi hicho, Franc Artiga, ni Mhispania aliyepita Barcelona mwenye falsafa ya soka la kushambulia kupitia pembeni na pasi fupi, akipenda kutumia mfumo wa 4-3-3.
Petro de Luanda katika mechi sita za Ligi Kuu ya Angola msimu huu imeshinda nne na kupoteza mbili, imefunga mabao kumi na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.
Hatua ya awali, Petro de Luanda iliiondosha Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 6-0, ikishinda ugenini 3-0 na nyumbani ushindi kama huo, kisha ikaifungashia virago Stade d’abidjan ya Ivory Coast kwa kichapo cha jumla ya mabao 4-0.
Pia ilishinda ugenini 2-0 na nyumbani 2-0. Hivyo hadi inafuzu makundi imeshinda mechi zote nne ilizocheza, ikifunga mabao 10, bila ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa ikionesha ni timu ngumu kufungika na hatari kwa wapinzani.
Kwa upande wa Simba hadi inafuzu makundi, imefunga mabao matano na kuruhusu moja katika mechi nne ilizocheza ikishinda mbili zote ugenini na sare mbili nyumbani. Matokeo yake yalikuwa hivi: Gaborone United 1-2 Simba na Nsingizini Hotspurs 0-3 Simba.
Katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Simba imeshuka dimbani mara tatu na kushinda mechi zote ikikusanya pointi tisa, ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya vinara Yanga wenye kumi ikicheza mechi nne. Simba katika mechi hizo tatu za ligi, imefunga mabao manane na kuruhusu moja.