Mastaa Yanga wamchambua Kocha Pedro Goncalves

MASHABIKI wa Yanga kidogo wameshusha presha juu ya ubora wa kikosi chao wakiona mambo yameaanza kubadilika lakini wachezaji wao nao wamefunguka namna walivyompokea kocha wao, Pedro Goncalves raia wa Ureno.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, wamesema kocha huyo ana vitu vyake ambavyo vimeanza kuingia kwenye timu na vitakuwa na matokeo chanya zaidi siku zinavyozidi kwenda.

Nahodha Msaidizi wa Yanga, Dickson Job, amesema mwanzo umekuwa mzuri kwa Goncalves ndani ya kikosi chao ambapo haraka wameanza kushika falsafa zake.

Job amesema kuwa kocha huyo anataka wachezaji wake wacheze soka la pasi na mipango ambalo sio jipya ndani ya kikosi chao, ikiwapa nafasi ya kurudisha ubora wa timu na kushinda kirahisi.

YANG 02


“Kocha tumempokea vizuri kama ambavyo umeona, tumeshinda vizuri hizi mechi mbili za kwanza lakini muhimu sana hii wa pili (dhidi ya KMC), nadhani na baadhi ya mambo anayoyataka yameanza kuonekana.

“Kocha anataka kuona wachezaji wake wanajiamini, wanatengeneza mipango ya kutafuta nafasi na kufunga mabao, nadhani tukiendelea kuimarika zaidi itatuongezea vitu vingi bora,” amesema Job.

Wakati Job akiyasema hayo, kiungo Pacome Zouzoua amefunguka kwamba kitu muhimu kwenye kikosi hicho ni namna wanavyohamasishana kuhakikisha wanaendelea kubadilika kabla ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, kitu ambacho kocha huyo anahitaji.

YANG 03


Zouzoua amesema alilazimika kumuachia penalti mshambuliaji wa kikosi hicho, Andy Boyeli ili imsaidie kurudisha hali ya kujiamini kwa lengo la kuhakikisha wanakuwa kwenye mstari mmoja wa ubora.

“Wakati ule nilikuwa nimeshafunga nikaona umuhimu wa wenzangu nao kufunga hasa washambuliaji ili tuimarike wote kabla ya mechi zijazo,” amesema Zouzoua.

“Sio kwa Boyeli tu hata Dube (Prince) angekuwa uwanjani naye ningempa, najua nini inamaanisha pale mchezaji anapokosa kufunga muda mrefu, nafurahi kuona baada ya penalti ile akafunga tena.

“Tunatakiwa wote kuwa kwenye mstari mmoja wa ubora kabla ya kuanza hizo mechi muhimu za Ligi ya Mabingwa, naamini tutafanya vizuri zaidi.”

Katika mechi hiyo iliyochezwa Novemba 9, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar, Yanga ilishinda kwa mabao 4-1, yakifungwa na Maxi Nzengeli, Pacome na Boyeli aliyetupia mawili, moja likiwa la penalti. Lile la KMC lilifungwa na Darueshi Saliboko.

YANG 04


Yanga baada ya kumalizana na KMC ikiwa imeshuka dimbani mara nne kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu na kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 10, Novemba 22, 2025 itaikaribisha AS FAR ya Morocco katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi B, itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Hiyo itakuwa ni mechi ya tatu kwa Goncalves tangu atambulishwe ndani ya kikosi cha Yanga Oktoba 25, 2025 akichukua nafasi ya Romain Folz. 

Mechi ya kwanza alishinda 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, kisha 4-1 dhidi ya KMC, zote za Ligi Kuu Bara. Dhidi ya AS FAR ni ya kwanza ya kimataifa.