Panya aligundua kuwa baada ya kuharibu suti ya harusi, alitegewa kwa mitego na sumu hadi chooni. Usiku aliibuka kama kawaida yake, alipoona kuwa katayarishiwa silaha za maangamizi alikimbilia kwenye banda la kuku, akamwambia jogoo kuwa hali si shwari na kumwomba aupige teke japo mtego mmoja naye apate mlo wake. Jogoo akamkatalia.
Kadhalika mbuzi na ng’ombe walikataa kumsaidia. Akasema poa, isiwe kesi. Siku hiyo akafunga mkanda. Usiku wa manane mtegaji akausikia mtego ukifyatuka nyuma ya kabati. Akaruka kutoka kitandani, akawasha taa lakini umeme ulikuwa umekatika.
Akaona potelea mbali, akaingiza mkono nyuma ya kabati. “Chwi!” Akang’atwa katika kidole gumba. Akacheka na kusema “hata ukijitetea, leo nimekunasa”. Akarudi na kupapasa mezani, akashika kiberiti na kukiwasha. Salale! Kwenye mtego lilinasa bonge la joka jeusi! Alipaka kila alichofikiri dawa lakini wapi. Akafa usiku uleule.
Asubuhi ndugu na jamaa wachache walifika na mchana ule wakachinjiwa jogoo kama kitoweo. Kesho yake baada ya mazishi akachinjwa mbuzi. Siku ya kuanua tanga, msiba ulimalizwa na wali kwa yule ng’ombe. Naam, mtego wa panya huingia aliyemo na asiyekuwamo.
Nikirudia hadithi ya uumbaji nitachosha kwani sote tumezikuta kwenye vitabu tofauti ulimwenguni.
Kuna vingi vinavyokazia imani zetu kwamba sisi ni kitu kimoja, tumekuja kwa mtindo mmoja na tutaondoka kwa mtindo mmoja.
Tuliambiwa kuwa sote tuliumbwa kwa mfano wa Mwenyezi Mungu aliyetuumba. Kwa hiyo Mungu hakuwabagua watu kwa makabila, rangi wala hali zao za kimaisha hapa duniani.
Kila mmoja ana imani yake. Imani yangu inanisisitizia kwamba sababu ya Mwenyezi Mungu kuumba zaidi ya mtu mmoja, ni kutaka kuona ushirikiano miongoni mwa watu wake.
Kwamba haikuwezekana kila mmoja apewe kila kitu, bali kila mtu ana vipawa vyake. Hivyo kwa kuwa lengo ni kuitunza dunia, kila mmoja alichangia kipawa chake ili kufanikisha lengo hilo. Nyumba ni moja lakini ina wajenzi wengi tofauti.
Ndio maana tumejiwekea mifumo ya utawala na mifumo ya kiimani. Wapo watu waliopewa kazi maalum za ulinzi wa raia na mali zao, pia wapo wanaofundisha na kulinda imani ili kuwafanya watu wadumu kwenye amani ya mwili na roho.
Amani inapotoweka watu hukosa afya ya akili, hushindwa kuvumiliana na hivyo kuyadidimiza maendeleo yao. Ipo mifano mingi sana duniani ya watu waliofikia hatua hiyo.
Kutokana na mapungufu ya kibinadamu, sehemu moja ya watu inaweza kuondoa uaminifu baina yao na sehemu nyingine. Kwa mfano walinzi wa amani wanapowashuku wale wanaowatumikia kuwageuka, wanaweza kuwa wakali dhidi yao. Lakini pia wananchi wanaotumikiwa wakiwashuku watumishi wao, hali huweza kubadilika. Kutakuwa na kutoelewana ambako kunaweza kabisa kupelekea vita baina yao.
Pengine katika makundi haya mawili, kila moja linaweza kujiona kuwa sawa. Nitoe mfano wa ugomvi wa nyoka na binadamu: nyoka kutaga ardhini.
Binadamu huweza kupita juu ya mayai ya nyoka na kuyaharibu pasipo kukusudia. Nyoka akiwa katika kulinda watoto wake watarajiwa, anaweza kumdhuru binadamu. Kwa hali hiyo, binadamu anamwona nyoka kuwa adui yake, na humdhuru mara amwonapo.
Matokeo huja kila baada ya kitendo. Mtaalamu wetu Isaac Newton alisema “chombo kitabaki kwenye hali ya utulivu hadi itakapotokea nguvu ya nje kukisukuma.”
Uadui wa nyoka na binadamu unatokana na kila mmoja wao kuona akisukumwa na mwenzake. Uhasama wao unachukua taswira ya vita ya mafahali, ambapo nyasi huumia zaidi. Wanapodhuriana, watoto wao hubaki yatima wasio na msaidizi.
Nchi yetu imepita kwenye kipindi kigumu sana wakati wa Uchaguzi Mkuu. Kulikuwa na tishio la kutofanyika kwa uchaguzi kutokana na maandamano yaliyopangwa kufanyika katika sehemu mbalimbali za nchi. Jijini Dar es Salaam tuliipokea amri ya kutoonekana barabarani baada ya saa 12 za jioni. Lakini katika baadhi ya maeneo tulilazimika kujifungia kwa siku nzima kwani kulikuwa na kutokuelewana kwa raia na Jeshi la Polisi.
Amri ilitaka watu kutojumuika kwenye vikundi. Lakini ukweli kwenye maeneo ya masoko na vituo vya mabasi hali ilikuwa tofauti kidogo.
Ilikuwa ngumu kwa raia wanaotegemea kupata mlo kwa kuuhangaikia kwa siku hiyo hiyo.
Wale ambao ilikuwa ni lazima watoke ili waweze kukidhi mahitaji yao na watoto wao, walijikuta wakiingia hatarini zaidi. Wapo ambao hawakudhamiria kuwemo kwenye maandamano lakini wakadhurika.
Katika juma lile la ukaazi wa ndani, wananchi walijikuta wakinunua nyanya yenye ukubwa wa zabibu kwa shilingi mia tano.
Kadhalika bidhaa zingine zote za vyakula zilipandishwa bei kiasi cha mara tatu ya bei yake halisi.
Wafanyabiashara walielezea kuwa hakuna bidhaa zilizoingizwa kutoka mashambani, hivyo nao walilazimika kununua kwa bei za juu kuliko walivyozoea. Waswahili walisema “Kufa Kufaana”.
Jambo hili linatukumbusha kutoacha asili yetu ya kuondoa tofauti zetu kwa upendo.
Hakuna aliyeachwa salama katika sakata lile lililo kama mtego wa panya.
Pamoja na kila upande kuumizwa na upande mwingine, lakini itumikapo busara tunaamini mambo hayataharibika. Jukumu la kuilinda amani ni letu sote.