WAKATI New Stone Town ikishikilia rekodi ya kupoteza mechi zote saba ilizocheza katika Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), Chipukizi imepata ushindi wa kwanza msimu huu.
New Stone ni miongoni mwa timu nne zilizopanda daraja kutokea Pemba sambamba na Fufuni. Nyingine ni New King na Polisi.
Katika msimamo wa ligi, New Stone ndiyo timu pekee isiyokuwa na pointi ikishika mkia kati ya timu 16.
Novemba 9, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, New Stone ilifunga bao la kwanza ilipopoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Chipukizi na kabla ya hapo ilicheza mechi sita bila kutikisa nyavu za wapinzani ikiwa imeruhusu kufungwa mabao 18.
Katika hatua nyingine, Malindi imeendelea kuwa timu pekee ambayo haijapoteza mechi hata moja tangu kuanza kwa msimu huu Septemba 25, 2025.
Kichapo ilichopokea KVZ Oktoba 25, 2025 kutoka kwa Malindi katika Uwanja wa Mao A uliopo Unguja cha mabao 3-0 yaliyofungwa na Ramadhan Mponda, Shafii Lumambo na Ajib Mohammed, kilikuwa cha kwanza kwao msimu huu.
Kwa upande mwingine, mabingwa wa FA msimu uliopita na waliokuwa wawakilishi wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, KMKM imeshuka dimbani mara nne bila kuonja ladha ya ushindi ikiambulia sare tatu na kupoteza moja.
Timu nyingine ambayo haijashinda mbali na New Stone Town ni Junguni United yenye sare tatu na kupoteza nne katika mechi saba.
Kabla ya jana Jumanne haijachezwa mechi ya Uhamiaji na Kipanga, vinara wa ligi walikuwa KVZ waliokusanya pointi 16 wakifuatiwa na Malindi (15) na Zimamoto (14) zote zikishuka dimbani mara saba.