BAADA ya kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Gaborone United ya Botswana kwenye mechi ya kwanza wa Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, JKT Queens sasa wana dakika 90 za jasho na damu za pointi tatu dhidi ya ASEC Mimosas.
Mechi hiyo ya kundi B inatarajiwa kupigwa Uwanja wa Suez Canal saa 12 jioni na JKT inahitaji ushindi wowote ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya nusu fainali.
Timu zote mbili zinahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi nzuri ya kuvuka nusu fainali, kwa ASEC ambao mechi ya kwanza ilishinda kwa bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe na JKT iliyotoa sare.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na presha kubwa hasa ikizingatiwa kuwa ushindi ndio unaweza kuwapa matumaini mapya mabingwa hao wa Ligi ya Wanawake Tanzania kuendelea kwenye michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Kocha wa timu hiyo amesema wachezaji wake wamechukua somo kubwa kwenye mchezo wa kwanza na sasa wamejipanga kufanya maboresho, hasa kwenye eneo la mwisho ambalo lilionekana kuwa na changamoto ya umaliziaji. “Tulicheza vizuri lakini hatukuweza kutumia nafasi tulizotengeneza, leo tunahitaji kuwa makini zaidi kila nafasi ni muhimu tunaiheshimu ASEC lakini tunajua tunapaswa kushinda,” amesema Kessy.
Kwa upande wa kocha wa Asec, Siaka Traore ‘Gigi’ amesema wanajua wana mechi ngumu leo dhidi ya JKT ambao ni wazoefu kwenye mashindano hayo.
“Kundi letu ni gumu tumewaona Gaborone na JKT walipocheza ni wazi tuna kazi ya kufanya kuhakikisha tunapata ushindi ingawa haitakuwa rahisi.”
Kabla ya mechi hiyo mapema saa 9 alasiri itapigwa mechi nyingine ya kundi B, TP Mazembe ina kibarua cha kutafuta pointi tatu mbele ya Gaborone United.