Straika Yanga autamani ubingwa | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Yanga Princess, Jeaninne Mukandayisenga amesema kama wachezaji wana kiu ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake na kuandika historia kwa mara ya kwanza.

Tangu Ligi ya Wanawake ianzishwe mwaka 2017 ni timu tatu tu zimenyakua ubingwa, Mlandizi Queens walioweka historia ya kuchukua kwa mara ya kwanza huku Simba Queens na JKT Queens zikibeba mara nne kila moja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mukandayisenga amesema huu unaweza ukawa msimu wao bora kutokana na aina ya kikosi na morali ya kila mchezaji kuutaka ubingwa huo. Aliongeza kuwa wachezaji wamejipanga kuhakikisha wanapambana kila mechi ili kuhakikisha wanatimiza malengo ya timu msimu huu.

“Tunajua ligi ni ngumu, kila timu imejipanga lakini sisi tumeweka malengo pia tunataka ubingwa. Kila mchezaji ana morali kubwa naamini huu unaweza kuwa msimu wetu wa kipekee,” amesema Mukandayisenga

Straika huyo raia wa Rwanda amesema mbali na malengo ya timu lakini binafsi anaitamani tuzo ya kiatu cha ufungaji akiamini uwezo wa kufikisha mabao 20 ndani ya msimu upo kutokana na kuzungukwa na viungo bora wa ushambuliaji.

“Ukiangalia timu yetu imesajili nyota wenye uzoefu na wana ubora mkubwa naamini kwa kushirikiana na wenzangu ndoto yangu ya kuchukua kiatu inaweza kutimia.”

Mukandayisenga alijiunga na Yanga dirisha dogo la usajili uliopita akitokea Rayon Sports ya kwao Rwanda ambako alionyesha kiwango kikubwa.

Ndani ya muda mchache aliocheza Yanga alifunga mabao 12 na kuisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.