Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Novemba 11, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;
Mechi Namba 006: Young Africans SC 2-0 Mtibwa Sugar
Klabu ya Young Africans imepewa Onyo Kali kwa kosa la kushindwa kufuata ratiba ya matukio ya mchezo (match countdown) kuelekea mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa KMC Complex Oktoba 28, 2025, kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Young Africans walishindwa kuwasilisha leseni za wachezaji wao kwa wakati jambo lililochelewesha zoezi la ukaguzi, ambapo ililazimika lifanyike saa 9:44 alasiri badala ya saa 8:50 mchana kama ratiba ilivyoainisha.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 040: Pamba Jiji FC 1-1 Singida Black Stars FC
Mwamuzi wa kati, Amina Kyando kutoka Morogoro na mwamuzi msaidizi namba mbili (2), Abdalah Bakenga kutoka Kigoma waliosimamia mchezo tajwa hapo juu, wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira.
Pamoja na matukio mengine, waamuzi hao walishindwa kutafsiri sheria katika tukio la kipa wa klabu ya Singida Black Stars kudaka mpira akiwa nje ya eneo la penati, hivyo kutotoa adhabu yoyote kwa kipa huyo. Waamuzi hao pia walionekana kutetereka na kutojiamini hata katika kufanya maamuzi yaliyo sahihi katika mchezo huo.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6 & 1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Mechi Namba 017: Transit Camp FC 3-1 Songea United FC
Klabu ya Songea United imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuchelewa
Songea United iliwasili uwanjani saa 9:10 alasiri badala ya saa 8:30 mchana kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:15 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi Namba 026: Hausung FC vs Stand United FC
Klabu ya Stand United ya mkoani Shinyanga imepoteza mchezo tajwa hapo juu na timu ya Hausung FC ya Njombe imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na alama tatu (3) kwa kosa la Stand United kushindwa kufika kwenye uwanja wa Amani, Njombe bila ya sababu za msingi na zinazokubalika hivyo kusababisha mchezo huo kushindwa kufanyika.
Sambamba na adhabu hiyo, Stand United imetozwa faini ya Sh. 10,000,000 (milioni kumi), kutakiwa kulipa fidia ya maandalizi ya mchezo huo pamoja na kupokwa alama tatu (3) katika msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.
Pia Mwenyekiti wa klabu ya Stand United, Stivian Antitius amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja (1) kwa kosa la klabu yake kushindwa kufika uwanjani.
Adhabu hizi ni kwa mujibu wa Kanuni ya 31:1 (1.1, 1.2, 1.3 & 1.4) ya Championship kuhusu Kutofika Uwanjani.