Bunge la 13 na mtihani wa 50/50 majimboni

Dar es Salaam. Bunge la 13, litakuwa na wanawake 38 pekee walioshinda ubunge wa majimbo, kati ya wabunge 272 wanaowakilisha wananchi kupitia majimboni kwa mujibu wa matokeo ya kura za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

Idadi hiyo ya wanawake walioshinda ubunge wa majimbo, ni sawa na asilimia 5.23 ya wabunge wote 272 wa majimbo walioshinda uchaguzi kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Kwa maneno mengine, katika kila wastani wa wabunge sita wa majimbo, mmoja ni mwanamke.

Hatua hiyo inazidisha mtihani katika juhudi za kufikia uwiano wa asilimia 50/50 kwenye ushiriki wa jinsi zote katika siasa na hivyo, inaonyesha bado kuna safari ndefu ya kuifikia azma hiyo.

Mtihani zaidi unaongezeka pale ambapo, muhimili huo hautakuwa chini ya uongozi wa mwanamke, kwa nafasi ya Spika na Naibu Spika, baada ya Dk Tulia Ackson kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, aliyeshinda uspika ni Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu, huku Daniel Sillo akiwa Naibu Spika. Hili linakuwa moja ya mabunge machache yaliyoongoza na spika na naibu wake mwanaume.

Bunge la 9, lilikuwa na Spika mwanaume (Samwel Sitta), lakini naibu wake alikuwa mwanamke (Anna Makinda). Bunge la 10 lilikuwa na Spika mwanamke (Anna) na naibu wake mwanaume (hayati Job Ndugai).

Lilipokuja Bunge la 10, Spika alikuwa mwanaume (Ndugai) lakini naibu wake alikuwa mwanamke (Dk Tulia), vivyo hivyo kwa Bunge la 11.

Bunge la 12, liliongozwa na Spika mwanamke (Dk Tulia), huku naibu wake akiwa mwanaume (Zungu) ambaye kwa sasa ndiye aliyechaguliwa kuwa spika na naibu wake mwanaume.

Rukwa, Geita hakuna mwanamke

Ukistaajabu ombwe hilo la uwiano wa wanawake na wanaume walioshinda ubunge wa majimbo nchini, yaliyotokea katika mikoa ya Rukwa na Geita yatakushangaza. Ni mikoa pekee isiyo na mbunge hata mmoja wa jimbo.

Mkoa wa Rukwa una majimbo matano. Kati ya yote hayo, bendera za vyama vya siasa katika nafasi ya ubunge wa majimbo hayo, zilipeperushwa na wagombea wanaume.

Majimbo hayo ni Sumbawanga Mjini, Kwela, Nkasi Kaskazini, Nkasi Kusini na Kalambo.

Kwa upande wa Mkoa wa Geita, una jumla ya majimbo tisa. Katika yote hayo, wagombea wake wa ubunge kupitia vyama mbalimbali vya siasa walikuwa wanaume pekee.

Majimbo hayo ni Geita, Busanda, Geita Mjini, Mbogwe, Katoro, Bukombe, Chato Kusini, Chato Kaskazini na Nyang’wale.

Ukiacha mikoa ya Rukwa na Geita iliyokosa kabisa uwakilishi wa wanawake katika mbio za ubunge wa majimbo kutoka vyama vyote 18, mikoa ya Kagera, Katavi, Njombe na Songwe inaongoza kwa kuwa na wanawake wachache wanaogombea nafasi hizo.

Mkoa wa Kagera, ulikuwa na mgombea wa ubunge mwanamke mmoja, huku Katavi, Njombe na Songwe, ilikuwa na wagombea wawili wanawake kwa kila mmoja.

CCM, Chaumma, ACT Wazalendo wachomoza

Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichokuwa na wagombea ubunge katika majimbo yote 272, ndicho kilichoongoza kwa idadi ya wabunge wanawake wa majimbo ambao ni 36. Ni mgombea mmoja pekee ndiye aliyeshindwa (Bonna Kamoli wa Segerea).

Chama kilichoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagombea ubunge wanawake, Demokrasia Makini (wagombea 50), wote hawakufua dafu katika mbio za ubunge, walishindwa.

Kilichofuatia ni NLD wanawake 42, CCK wanawake 40. Wote hawakushinda. Kwa upande wa Chaumma wanawake 40, lakini ameshinda mmoja (Agnesta Kaiza wa Segerea).

Kwa upande wa DP kilichokuwa na wagombea wanawake 38, CUF (35) na AAFP (33) wote hawakushinda, huku ACT-Wazalendo kilichokuwa na wagombea 31 wanawake, ameshinda mmoja.

Vyama vya UPDP na NRA vilivyokuwa na wagombea 30 wanawake majimboni, wote wameangukia pua katika matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu.

Vinavyofuata ni Ada-Tadea wagombea wanawake 29, UMD (28), SAU (27), TLP (27), ADC (17), huku UDP na NCCR-Mageuzi, vikiwa na wagombea 12 kila kimoja. Katika orodha hii, wagombea wote wanawake walishindwa.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, uchaguzi wa mwaka 2010, wagombea wanawake wa ubunge wa majimbo walikuwa asilimia 12.4 pekee ya wagombea wote.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, idadi hiyo ilipanda hadi asilimia 21 na mwaka 2020 ikaongezeka tena hadi asilimia 27.6.

Hali ya mwaka huu iliyofikia asilimia 32.17 ya wagombea wote inaonyesha mwendelezo wa ongezeko, lakini bado inaleta changamoto ya kufikia lengo la usawa wa kijinsia lililoainishwa kwenye Mkataba wa Beijing (1995) na Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030 ya Umoja wa Mataifa (SDG 5).

Hata hivyo, Bunge hilo la 13, litakuwa na wabunge 115 wa viti maalumu. Kati yao wanaotokana na CCM ni 113 na wawili ni Chaumma.

Ukichanganya na wale 38 wa majimbo, bunge hilo litakuwa na jumla ya wabunge 153 wanawake kwa maana wa majimbo na wale wa viti maalumu.

Pia, Rais Samia Suluhu Hassan amemteuwa Dk Dorothy Gwajima kuwa Mbunge, hivyo ukijumlisha bunge hilo litakuwa na wabunge wanawake 154 hadi sasa.

Lakini, bado kuna nafasi nne za Rais Samia kuwateuwa wabunge wengine, huku majimbo mawili nayo uchaguzi wake umeahirishwa. Utarudiwa hivi karibuni.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Tike Mwambipile anasema idadi ndogo ya walioshinda, imechochewa na uchache wa waliojitokeza.

Anaeleza imeshuhudiwa katika michakato ya ndani ya uchukuaji fomu ndani ya vyama vya siasa, idadi ya wanawake walioonyesha nia ya kuutaka ubunge wa majimbo ni ndogo ukilinganisha na wanaume.

“Kama wamejitokeza wachache na INEC inateuwa waliopitishwa na vyama kwa kuangalia sifa na vigezo mbalimbali, ukiwachuja lazima watakaoteuliwa ni wachache. Na ukifanyika uchaguzi ndio watapungua zaidi ndicho kinachoshuhudiwa,” anaeleza.

Lawama ya wanawake wachache kwa mujibu wa Tike, imeshaondoka kwa vyama vya siasa na INEC, sasa wanaopaswa kulaumiwa ni wanawake wenyewe.

Anasema wanawake wameacha kuchangamkia fursa ya uchukuaji fomu za kugombea ubunge wa majimbo, wengi wamejikita katika nafasi za viti maalumu.

“Inaonekana bado wanawake tuna uoga wa kwenda kuchukua fomu,” anasema Tike.

Wakati Tike akieleza hayo, uchaguzi wa mwaka huu, ulikuwa na wagombea 558 wa ubunge majimboni, kati ya 1,735. Hivyo, wanawake waliojitokea kugombea ni sawa na asilimia 32.7.

Kwa sababu ya uhalisia huo, anasema inaonekana dhahiri kuna ombwe la uhamasishaji na uelimishaji wanawake kutoka kwa wadau wa jinsia.

“Sisi asasi za kiraia hii inatuonyesha bado hatujafanikiwa kuifanya kazi yetu vizuri ya kuwahamasisha wanawake wajitokeze kwenye kugombea. Bado hatujafanya vizuri na kuna umuhimu wa kuendelea kuwapa motisha wanawake ili waone umuhimu wa kushika nafasi za majimbo,” anasema.

Anasema kwa sababu hakuna visingizio vya kiuchumi wala fursa kwani zinatolewa, kilichobaki ni wanawake wenyewe kujitokeza kuchukua fomu na hatimaye kugombea.

Wachambuzi wa masuala ya kijinsia wanaeleza idadi ndogo ya wanawake wanaojitokeza kugombea ubunge wa majimbo inachochewa na sababu tatu.

Katika jamii bado kuna imani kwamba mwanaume ndiye kiongozi wa asili. Hali hii inawafanya wanawake wengi kuamini kuwa nafasi yao ya kushinda ni ndogo, hivyo hukata tamaa mapema,” anasema Pili Nyundo mdau wa masuala ya kijinsia.

Anasema ukosefu wa mtandao wa kisiasa ni sababu nyingine. Wanaume mara nyingi huanza kujijenga mapema kupitia vyama, mitandao ya kijamii, hali inayowapa nafasi ya kutambulika zaidi.

Sababu nyingine, anasema ni upendeleo unaoibuka katika mchakato wa awali wa uteuzi.

Ingawa vyama havibagui moja kwa moja, mara nyingi wanawake hukosa nguvu za kisiasa na rasilimali za kushinda kura za maoni au majimboni.

Viti maalum, baraka na changamoto

Mfumo wa viti maalumu umekuwa moja ya nyenzo muhimu katika kuongeza idadi ya wanawake bungeni. Kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya wabunge wanawake wanatokana na mfumo huo.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema mfumo huo umekuwa pia kikwazo cha kisaikolojia. Mchambuzi wa masuala ya kijinsia, Dk Elizabeth Mushi anasema wanawake wengi wanajua kuwa hata wasipojitokeza kugombea majimboni, vyama vitawapa nafasi kupitia viti maalumu.

Hali hiyo, anasema inawafanya wasipambane kwa juhudi majimboni na badala yake kusubiri nafasi hiyo ya upendeleo.

Anasisitiza umefika wakati wa kuufanya mfumo huo usiwe kimbilio, bali chachu ya kuwaandaa wanawake kwa mashindano makali zaidi ya kisiasa.

Athari za uwakilishi mdogo

Tafiti za kimataifa zinaonyesha, uwakilishi mkubwa wa wanawake bungeni una uhusiano wa moja kwa moja na kupitishwa kwa sera zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi.

Ripoti ya Inter-Parliamentary Union ya mwaka 2023, inabainisha katika nchi zenye uwakilishi mkubwa wa wanawake, bajeti ya kijamii huongezeka kwa wastani wa asilimia 15 zaidi kuliko zile zenye uwakilishi mdogo.

Kwa Tanzania, idadi ndogo ya wanawake majimboni ina maana ya sauti hafifu katika maamuzi makubwa ya kitaifa. Hii inaathiri moja kwa moja masuala kama afya ya mama na mtoto, ajira zenye mshahara mdogo na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, mambo ambayo mara nyingi wanawake wabunge huyaibua kwa nguvu bungeni.

Nafasi ya vyama vya siasa

Licha ya jitihada zilizochukuliwa na vyama vya siasa, idadi ya wanawake walioshinda majimboni bado ni ndogo.

Mtaalamu wa masuala ya jinsia, Gaudens Mpangala anaamini suluhisho la muda mfupi ni kutenga majimbo kwa ajili ya wanawake kama hatua ya mpito kuelekea usawa.

Anasema hilo siyo ubaguzi, bali ni njia ya kuleta ulinganifu kutokana na historia ya mfumo dume. Kwa mtazamo wake, tukisubiri ushindani wa kawaida pekee, huenda Tanzania ikachukua miongo kadhaa kufikia malengo ya usawa wa kijinsia.

Hali inakuwa ngumu zaidi kwa vijana wa kike. Utafiti uliofanywa na Repoa wa mwaka 2022, unaonyesha wanawake vijana wanaoingia kwenye siasa hukumbana na kebehi na dharau kutokana na jinsia na umri wao.

Utafiti huo, unaonyesha kati ya vijana 100 waliowahi kuchukua fomu za kugombea udiwani katika kipindi cha miaka mitano, wanawake walikuwa 27 pekee.

Mary John, kijana wa miaka 27 aliyegombea udiwani mwaka 2020 lakini hakufanikiwa, anakumbuka alivyokumbana na changamoto hiyo.

“Nilipojitokeza, watu waliniuliza kama si bora nianze na viti maalumu. Hii ni changamoto kubwa, maana inatuma ujumbe kuwa nafasi za ushindani ni za wanaume,” anasema.

Wadau wanaamini kuna hatua zinazoweza kusaidia. Kwanza, asasi za kiraia zinapaswa kuongeza mafunzo na uhamasishaji ili kuwaandaa wanawake kisiasa.

Mary anasema suala la gharama za kampeni linahitaji majibu kupitia ruzuku maalumu kwa wagombea wanawake, wakati huo huo mabadiliko ya kisheria yanahitajika, ikiwamo kuweka kipengele cha kikatiba kitakacholazimisha vyama kuteua idadi fulani ya wanawake majimboni.

Hatua nyingine muhimu, anasema ni kuelimisha jamii ili kubadilisha dhana kwamba siasa ni za wanaume pekee.

Kwa mujibu wa takwimu za Inter-Parliamentary Union (IPU), hadi Machi 2024, Rwanda inashikilia rekodi barani Afrika kwa kuwa na uwakilishi wa wanawake wengi bungeni kwa asilimia 61.3.

Afrika Kusini inafuatia kwa asilimia 46.5, Uganda ina asilimia 34.9. Hali hiyo inaonyesha Tanzania ipo katikati ya safari.

Imefanikiwa kupiga hatua kupitia mfumo wa viti maalumu, lakini bado ipo nyuma ikilinganishwa na majirani zake, hususan Rwanda na Afrika Kusini, katika kufikia usawa wa kijinsia kwenye siasa.