Usichofahamu wanaume wanaopata kichefuchefu, uchovu kisa mimba za wenza wao

Dar es Salaam. Kuna wanaume ambao, bila wao wenyewe kuelewa vizuri, huanza kupata dalili zinazofanana na za wake zao wanaotarajia mtoto, kama vile usingizi mwingi, kichefuchefu, kutapika, hata kuongezeka uzito.

Hali hii imekuwa ikionekana kama mzaha katika jamii, wengi wakijiuliza, “Mume naye ana mimba?”

Katika baadhi ya jamii huiona hali hiyo kama ishara ya upendo wa dhati au kiunganishi cha kiroho kati ya mume na mke, wakiamini ni ishara ya mwanaume mwenye huruma au anayebeba mzigo wa ndoa kwa pamoja pale wanapotarajia kupata mtoto.

Lakini wapo pia ambao hucheka au kuona kama ushirikina au “mapepo ya mimba” hasa pale dalili zinapokuwa kali zaidi kuliko za mke wake.

Simulizi ya Josephat Gwamaka wa Temeke, Dar es Salaam ambaye ni baba wa watoto wawili amesema, katika kipindi chote cha ujauzito wa mkewe yeye ndiye alikuwa kwenye hali ya uchovu.

“Kuna muda nilihisi kama nimerogwa, ilifikia hatua kuna aina ya vyakula sikutaka hata kusikia harufu yake, nilipata kichefuchefu na mara nyingi nilikuwa mchovu na mwenye usingizi kupitiliza.

“Ilifikia hatua hadi ufanisi wangu kazini ulipungua, ajabu mke wangu aliyekuwa mjamzito ndiye alikuwa akinisaidia mimi, hali ile ilinitesa hadi alipojifunguka, ilinitokea tena alipobeba mimba ya mtoto wa pili,” amesema Gwamaka baba wa watoto wawili.

Nelson Peter yeye pia ni miongoni mwa waliokutana na changamoto hiyo, anasema wakati wa ujauzito wa mkewe, kuna vyakula alipenda kula, ambavyo hakuwahi japo kuvifikiria kabla.

“Nakumbuka kuna nyakati nilikuwa natembea na limao au ndimu n kula, wafanyakazi wenzangu walikuwa wakinitania, naishia kutabasamu tu lakini niliyoyapitia anajua Mungu, hivi sasa naogopa mke wangu akibeba mimba ya pili nini kitatokea,” amesema.

Baadhi ya kina mama wakieleza hali hiyo wamesema wenza wao walijikuta wakifanya matukio yasiyo ya kawaida, wao walipokuwa na ujauzito.

Elizabeth Jonas amesema mumewe alikumbana na changamoto ya kupoteza kumbukumbu yeye alipokuwa mjamzito.

“Nilipojifungua hali yake ikarudi kawaida,” amesema Elizabeth akitolea mfano wa moja ya matukio ambayo hawezi kusahau ni mumewe kusahau kitu gani alitaka kufanya au ni eneo gani alitaka kwenda.

“Kuna siku alisahau ni wapi alikuwa akienda, hadi akanipigia simu, hali hiyo ilikwisha nilipojifungua,” amesema huku akitabasamu.

Hulda Mussa yeye anakumbuka mumewe alivyoanza kula udongo, alipokuwa mjamzito.

“Niliona ajabu sana, kuna muda hadi nilimuonea huruma kutokana na aliyokuwa akipitia. Kama haitoshi, kila mara alikuwa akilalamika kuumwa, alikuwa sawa nilipojifunga,” amesema.

Inaelezwa hali ya mwanaume kupata dalili za ujauzito wa mwenzi wake kwa kitaalamu sio ugonjwa ni tabia inayojulikana kitaalamu kama “Couvade Syndrome”.

Wakieleza dalili zinazoweza kumpata mwanaume ambaye mwenza wake ana mimba ni kichefuchefu, kutapika au kukosa hamu ya kula.

Dalili nyingine ni usingizi mwingi au uchovu usioelezeka na wengine kupata maumivu ya kichwa au mgongo, huku baadhi yao wakiwashwa na wengine kupata mabadiliko ya hisia na baadhi yao kuongezeka uzito kadiri mimba inavyokuwa.

Jarida la American Journal of Men’s Health (2019) liliripoti kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wanaume huonyesha dalili fulani za aina hiyo wakati wa ujauzito wa wenzi wao.

Lilibainisha mabadiliko hayo mara nyingi hutokea katika kipindi cha kati cha ujauzito, na hupungua mtoto anapozaliwa.

Mwaka 2007, katika utafiti wa “A Critical Review of the Couvade Syndrome:The Pregnant Male”, mhadhiri mwandamizi wa vyuo vikuu vya Kingston na St George’s vya nchini Uingereza, Dk Arthur Brennan alieleza juu ya Couvade Syndrome.

Alisema huo si ugonjwa, bali ni jibu la kisaikolojia na kihisia linalohusiana na mabadiliko yanayotokea katika maisha ya mwanaume anapokaribia kuwa baba.

Katika utafiti wake, uliochapishwa kwenye jarida Journal of Reproductive and Infant Psychology, Toleo 25, ulieleza hali ya ajabu ambayo baadhi ya wanaume huanza kupata dalili zinazofanana na za ujauzito wakati wenzi wao wakiwa na mimba.

Dk Brennan alieleza, dalili kama kichefuchefu, maumivu ya mgongo, kuongezeka uzito, mabadiliko ya usingizi, na wasiwasi hutokea kwa baadhi ya wanaume kwa kipindi fulani cha ujauzito wa wenzi wao, hasa miezi ya kati na ya mwisho.

Alisema Couvade Syndrome ni alama ya ushirikiano wa kihisia na mabadiliko ya kijamii katika safari ya uzazi, akifafanua kwamba mwanaume anayepitia dalili hizo anaonyesha kiwango cha juu cha kuhusika na uhusiano wa karibu na mwenzi wake, hivyo si ugonjwa au udhaifu.

Akifafanua hilo, Rais wa Chama cha madaktari wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Ali Said amesema hiyo ipo kisaikolojia zaidi na si kitaalamu.

Amesema hakuna sayansi inayothibitisha hilo kitaalamu, akifafanua kwamba hali ya mwanaume kupata dalili za ujauzito wa mwenzi wake au “Couvade Syndrome” ni ya kisaikolojia zaidi na si kitabibu.

Daktari mwingine wa masuala ya uzazi kwa wanaume, Isaka Hamis anasema hakuna uhusiano wa moja kwa moja wa kitabibu wa hali hiyo.

“Japo kuna dhana kwa baadhi ikihusishwa na na bond ya wenza waliyonayo katika mahusiano, hivyo ni masuala ya kisaikolojia, lakini sio kitabibu,” amesema.

Mwanasaikolojia, Deogratius Sukambi anasema hakuna ushahidi wa kitaalamu wa moja kwa moja kuhusu mwanaume kupata dalili za ujauzito wa mwenzi wake, japo kisaikolojia kuna tatizo la trauma bond ambalo linasababisha hisia kupitiliza katika misingi yamajeraha au maumivu.

Akitolea mfano hilo, anasema wapo baadhi ya watu, mtu mwingine anapata msiba yeye ndiye anakuwa kana kwamba amefiwa au mwingine mtu anapoomba amkopeshe pesa akashindwa kumsaidia basi huwa unaumia kupitiliza.

“Isivyo bahati wenye tatizo hili huwa wanajiona kuwa na moyo mzuri, kumbe sivyo bali ni tatizo la kisaikoloji linalohitaji tiba,” amesema.

Amesema kuna wanaume ambao kihisia huwa hawana stamina na ustahimilivu hasa anapokuwa anashuhudia mtu mwingine akiteseka.

“Si wanaume pekee, hadi wanawake wapo, mfano hawezi kustahimili kuona mtoto akilia, hivyo kwa hilo la mume kupata dalili za ujauzito wa mwenza wake, huenda wakawepo lakini ni wale wenye changamoto ya traoma bond lakini kitaalamu hakuna kinachothibitisha hilo la mimba ya mwenza wake.

“Hivyo basi wale wenye tatizo la traoma bond ndiyo huenda miongoni wakajikuta wanaingia huko, kwa kuwa tatizo hilo linahusisha kuwa na hisia kupitiliza katika maumivu ya mtu mwingine,” amesema.

Akitolea mfano aina ya watu wenye tatizo la Traoma Bond, Sukambi amesema miongoni mwao ni wale inatokea mtu mwingine amefiwa, basi msiba anaubeba yeye kana kwamba ndiye amefiwa.

“Katika mazingira kama hayo ya ujauzito wa mwenza, ikitokea mtu mwenye tatizo la traoma bond basi anaweza kuingia huko, lakini hakuna muktadha wa saikolojia unaothibitisha hilo.

“Hivyo yule mwenye tatizo la hisia kupitiliza anaweza kuibeba straggle ambayo mwenza wake anapitia wakati wa ujauzito, lakini kitaalamu hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuhusu mume kupata dalili za mimba ya mwenza wake,” amesema.

Mwanasaikolojia mwingine, Mchungaji Daniel Sendero hajatofautiana sana na mtangulizi wake, amesema wapo baadhi ya wanaume wana changamoto hiyo akibainisha kwamba haliko moja kwa moja ya mimba, bali ni wale wenye tatizo la traoma bond.

“Kijamii hilo la ujauzito halina maelezo ya kitaalamu ya saikolojia, japo wapo wale wenye tatizo la traoma bond ambao wanakuwa anabeba maumivu ya mtu mwingine na kuzama ndani ya hilo tatizo kama lake,” amesema.