Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imetoa Onyo Kali kwa Klabu ya Young Africans SC kutokana na kushindwa kufuata ratiba ya matukio ya mchezo (match countdown) kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar FC, uliochezwa Oktoba 28, 2025 katika Uwanja wa KMC Complex, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2–0.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Bodi ya Ligi iliyotolewa Novemba 11, 2025, klabu hiyo ilikiuka Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu Tanzania Bara, inayohusu utaratibu na muda wa maandalizi ya kabla ya mchezo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Young Africans walishindwa kuwasilisha leseni za wachezaji wao kwa wakati, hali iliyosababisha ucheleweshaji wa zoezi la ukaguzi wa wachezaji. Badala ya ukaguzi kuanza saa 8:50 mchana kama ilivyopangwa, ulianza saa 9:44 alasiri, kinyume na taratibu za mashindano.
Bodi ya Ligi imesisitiza kuwa ucheleweshaji wa aina hiyo unavuruga ratiba rasmi ya mechi na maandalizi ya timu zote mbili, hivyo onjo hilo kali litumike kama tahadhari kwa klabu kuhakikisha inazingatia kanuni zote za ligi katika michezo ijayo.
Related
