Ushindi wa mchezo wa kesho, Alhamisi, Novemba 13, 2025 dhidi ya Cameroon, jijini Rabat, Morocco utakuwa na maana kubwa kwa DR Congo.
Kwanza utaifanya timu hiyo itinge katika hatua ya fainali ya mechi za mchujo za kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 huko Marekani kwa Kanda ya Afrika ambayo baadaye itawezesha kushiriki mechi za mchujo za mabara.
Lakini maana kubwa ya pili ni wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la DR Congo kila mmoja kupata kiasi cha zaidi ya Shilingi 2 bilioni kila mmoja ikiwa watapa ushindi.
Imeripotiwa kwamba serikali ya DR Congo imetoa ahadi ya Dola 1 milioni (Sh2.5 bilioni) kwa kila mtu aliyepo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo ikiwa itapata ushindi dhidi ya Cameroon.
Lengo la serikali ya DR Congo ni kuongeza hamasa kwa wachezaji wa timu hiyo ili kuhakikisha inafanya vizuri na kutinga hatua ya fainali.
Miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha DR Congo ambacho kipo Morocco kwa ajili ya mechi hiyo ya mchujo ni mshambuliaji wa zamani wa Yanga anayechezea Pyramids FC hivi sasa, Fiston Mayele
Katika fainali, mshindi wa mchezo baina ya DR Congo atakutana na mshindi wa mchezo baina ya Gabon na Nigeri ambao nao utafanyika kesho.
Mechi hizo za nusu fainali kesho zote zitachezwa jijini Rabat, Morocco na hata mchezo wa fainali utachezwa hukohuko.
Gabon na Nigeria ndio zitafungua dimba ambapo zitakutana katika Uwanja wa Moulay Hassan kuanzia saa 1:00 usiku kwa muda wa Tanzania.
Mchezo wa pili ambao utazikutanisha DR Congo na Cameroon, utachezwa kwenye Uwanja wa Al Barid kuanzia saa 4:00 usiku.
Fainali itakuwa ni Novemba 16, 2025 katika Uwanja wa Moulay Hassan kuanzia saa 4:00 usiku kwa muda wa Tanzania.