Dar es Salaam. Darasa moja la kidato cha kwanza lenye zaidi ya wanafunzi 600 katika Shule ya Sekondari Mtakuja Beach, lililopo Kata ya Kunduchi, Manispaa ya Kinondoni, limezua gumzo miongoni mwa wazazi, walezi na wadau wa elimu jijini Dar es Salaam.
Wazazi hao wanasema idadi hiyo kubwa inatia shaka juu ya ubora wa elimu inayotolewa shuleni hapo, huku wengine wakidai baadhi ya wanafunzi hufukuzwa au kushauri wazazi wawahamishie watoto wao shule nyingine kwa visingizio vya utoro.
“Kwa mfano, mtoto akikosa shule siku mbili tu, mzazi anaambiwa amtafutie shule nyingine. Hali hii imekuwa ikitokea mara kwa mara,” anasema Alex Jacob, mkazi wa Mtongani ambaye mtoto wake anasoma shuleni hapo.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe, anasema wingi wa wanafunzi umetokana na sifa nzuri ya shule hiyo katika matokeo ya mitihani ya taifa.
“Mtakuja ilikuwa shule ya mfano. Ilikuwa ikifaulisha sana, ndiyo maana wazazi wengi wamekuwa wakihamishia watoto wao hapa, wengine hata kwa msaada wa viongozi wa kisiasa,” anasema.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa jirani na shule hiyo wanasema pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi, hakuna anayekaa chini wakati wa masomo kwa kuwa shule ina mikondo mingi kuanzia A hadi F.
“Wanafunzi wanasoma kwa zamu kulingana na mikondo yao. Hawaingii wote 600 darasani kwa wakati mmoja,” anasema Mariam Hamisi, mkazi wa Kunduchi.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne waliozungumza na Mwananchi wanakiri kusoma wakiwa wengi darasani, lakini wanafurahia elimu wanayoipata.
“Tunagawanywa kulingana na ufaulu wetu wa mitihani ya ndani. Hata kama tuko zaidi ya 500, kila kundi linapata muda wake wa masomo,” amesema mmoja wao.
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Shule ya Mtakuja Beach, Projestus Barongo, anakanusha madai ya kuwafukuza wanafunzi, akisema hana mamlaka ya kufanya hivyo.
“Kisheria, mkuu wa shule hana mamlaka ya kumfukuza mwanafunzi. Ni bodi ya shule pekee inayoweza kufanya hivyo. Sisi kazi yetu ni kumsimamisha mwanafunzi kwa muda ili kumrekebisha, si kumfukuza,” anasema Barongo alipozungumza na Mwananchi ofisini kwake.
Barongo anakiri kuwahi kuwapa onyo wanafunzi sita ‘sugu’ kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, lakini akasisitiza hakuna aliyefukuzwa.
“Tunapambana na tabia zisizofaa kama uvutaji bangi, lakini badala ya kuwafukuza, tunawaita wazazi tuzungumze. Tatizo ni kwamba wengi wao hawafiki,” anasema kwa masikitiko.
Mkuu huyo anaongeza kuwa shule yake imekuwa ikipokea wanafunzi kutoka shule nyingine za jirani kutokana na rekodi nzuri ya ufaulu.
“Mwaka jana nilipokea wanafunzi 11 waliokuwa wamefukuzwa shule nyingine. Sasa kama nawapokea walioshindikana, nitawezaje kuwafukuza wangu?” anahoji.
Diwani wa Kunduchi afafanua
Diwani mteule wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio, anakiri kufahamu suala hilo na kusema chanzo ni idadi kubwa ya wakazi wa Mtaa wa Mtongani, unaoongoza kwa kuwa na wakazi 39,000.
“Mtongani pekee kuna shule mbili za msingi zenye idadi kubwa ya wanafunzi. Wengi wao wanajiunga Mtakuja Sekondari, hivyo shinikizo ni kubwa kuliko katika mitaa mingine kama Kondo au Pwani,” anasema Urio.
Aidha, anakanusha madai kwamba viongozi wa kisiasa wanahusishwa na uhamisho wa watoto kwa malipo, akisema wazazi wengi wanachagua shule hiyo kutokana na ukaribu na ubora wake.
“Ni kweli wazazi kutoka mitaa ya mbali kama Kondo au Pwani wanakuja kuomba watoto wao wabaki Mtakuja, jambo linaloongeza mzigo wa wanafunzi,” anasema.
Wataalamu wa elimu wapinga
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Tanzania (Tamongsco), Benjamin Mkonya, anakosoa darasa moja kuwa na wanafunzi 600, akisema linakinzana na mwongozo wa Unesco unaotaka wanafunzi wasizidi 45 kwa darasa moja.
“Mwalimu anatakiwa awafahamu wanafunzi wake, wapo wanaojifunza kwa haraka, wengine taratibu. Ukiwa na wanafunzi 600, mwalimu hawezi kufuatilia maendeleo yao vizuri,” anasema Mkonya.
Anasema idadi kubwa ya wanafunzi inachangia kuporomoka kwa ubora wa elimu katika shule nyingi za Serikali, tofauti na za binafsi zinazozingatia miongozo ya kimataifa.
Shule ya Sekondari Mtakuja Beach ni moja ya shule tatu za Serikali zilizopo Kata ya Kunduchi, pamoja na Kondo Sekondari na Godwin Gondwe High School.
Shule hiyo imejipatia umaarufu kutokana na matokeo mazuri ya wanafunzi wake katika mitihani ya kitaifa, jambo lililowafanya wazazi wengi kuamini ni shule ya kufaulisha.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Elimu ya Manispaa ya Kinondoni, ongezeko la wanafunzi limekuwa likiongezeka kila mwaka kutokana na idadi ya wakazi katika eneo la Kunduchi na upungufu wa shule za sekondari zenye miundombinu bora.
Hata hivyo, wadau wa elimu wanaonya kuwa iwapo hali hiyo haitadhibitiwa, huenda ubora wa elimu ukashuka na kuathiri kizazi kijacho.