Vurugu zilizotokea nchini siku ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025 zimeacha alama nzito katika historia ya Tanzania.
Maisha ya watu yamepotea, wengine wamejeruhiwa, mali za umma na za binafsi zimeteketea kwa moto, huku miundombinu muhimu kama barabara, vituo vya mwendokasi, ofisi za Serikali na magari, mali za watu binafsi yakiwamo magari, vituo vya mafuta na maduka zikiharibiwa.
Ni tukio lililoitikisa nchi. Watu wengi wamebaki wakiwa na hofu, huzuni na maswali mengi wakijiuliza tumefikaje hapa na tutarudi vipi kwenye mstari wa amani na umoja wetu wa taifa?
Ili tuweze kunyanyuka, tunapaswa kwanza kutazama kwa uhalisia wapi tulijikwaa. Vurugu hazitokei bila mizizi; daima kuna chanzo, kama ni uchochezi, migawanyiko ya kisiasa, kukosekana kwa uaminifu kati ya wananchi na viongozi, au hisia za kutotendewa haki. Hatua ya kwanza ni kukubali ukweli huu bila kujitetea wala kulaumiana kupita kiasi. Kukiri kosa ni mwanzo wa kupona.
Kwanza, tulijikwaa kwenye mawasiliano na uaminifu wa kitaifa. Katika kipindi tulichokuwa tukiueleke uchaguzi mkuu, matamshi ya chuki, upotoshaji wa habari na misimamo mikali vilitawala mitandao na majukwaa ya kisiasa. Haya yalitengeneza aina fulani ya mpasuko na ili sasa tusirudie kosa hili, binafsi nashauri kwamba tunahitaji kurejesha utamaduni wa majadiliano yenye staha, kusikilizana na kuheshimu tofauti za maoni.
Maoni yanayokinzana hayapaswi kuwa chanzo cha uhasama bali fursa ya kujifunza.
Nasema hivyo kwa sababu vurugu hizi zimetuonyesha ni kwa namna gani tunapaswa kuimarisha mifumo yetu ya maisha kuanzia kwenye ngazi ya familia mpaka serikalini.
Tukubali kwamba tumejikwaa katika malezi ya kizazi kipya. Wimbi la mmomonyoko wa maadili, utandawazi usiodhibitiwa na kukosekana kwa mifano bora, imeathiri misingi ya utu na uzalendo tuliojengewa na waasisi wa Taifa hili tangu enzi na enzi.
Ili kuinuka sasa hapa tulipojikwaa na kuanguka, lazima tuwekeze katika elimu yenye maadili, inayomfundisha kijana si tu kusoma na kuandika, bali pia kupenda nchi yake, kuheshimu wengine na kutenda kwa uadilifu.
Tunapojitazama kwa uhalisia, hatuna budi kukiri kuwa bado tunayo nafasi kubwa ya kujirekebisha. Umoja wetu, amani yetu na mshikamano wetu bado ni nguzo thabiti ambazo dunia inatuonea fahari. Tusiziache ziporomoke kwa sababu ya tofauti ndogo au tamaa binafsi.
Kuanzishwa kwa vikao vya upatanisho na majadiliano ya kitaifa kutasaidia kupunguza hofu na kurejesha imani miongoni mwa Watanzania kwa hiki kilichotokea.
Lakini tumeona jinsi ukosefu wa malezi bora ulivyotugharimu. Baadhi ya vijana walijikuta wakishiriki katika matendo ya uharibifu bila kutambua athari zake kwao binafsi, familia na taifa.
Hii inatupa somo la kurejelea misingi ya elimu ya uraia na uzalendo kuanzia shuleni hadi vyuoni, ili kizazi kijacho kiwe kinathamini amani kuliko hasira za muda mfupi.
Tumejifunza kwamba amani si hali ya ukimya baada ya vurugu, bali ni matokeo ya haki, usawa na uwajibikaji. Kwa hiyo, tunapaswa kuhakikisha wale walioathiriwa wanapata haki, fidia na msaada wa kisaikolojia.
Serikali nayo inapaswa kuwatazama kwa jicho la imani wale waliopoteza ndugu na mali kwamba wanahitaji kujengewa upya imani kwa kuona kuwa Serikali yao na taifa kwa ujumla linawajali.
Pia, ni lazima tutambue kwamba vurugu hizi hazikuharibu majengo na mali pekee, bali pia udugu wetu. Hivyo basi, juhudi za upatanisho hazipaswi kuwa za maneno tu, bali ziwe za vitendo.
Viongozi wa dini, kisiasa, wa Serikali, asasi za kiraia, wanahabari na wananchi wote washiriki katika kujenga madaraja mapya ya haki amani na upendo.
Kwa sasa, tunahitaji kutumia nafasi hii kama somo la kujirekebisha. Kila sekta ichukue wajibu wake, serikali iimarisha mifumo ya ulinzi na ushirikishwaji wa wananchi, vyama vya siasa vijenge siasa za hoja na sera na wananchi wajifunze kutumia njia za amani katika kudai haki zao.
Tukumbuke kuwa Tanzania imeshinda mitihani mingi katika historia yake. Tuliweka misingi ya umoja tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alituonya kwamba amani ni tunda la haki. Hivyo basi, tusiruhusu hasira za sasa zitufanye tusahau urithi huo.
Ni vema kama kila Mtanzania akazingatia na kutambua kwamba anao wajibu wa kuiuliza nafsi yake: Ninachangia nini kuhakikisha nchi yangu inaponya majeraha haya?
Tukiweka mbele upendo na kusameheana kwa dhati, tutanyanyuka tena tukiwa wamoja ndani ya taifa moja lenye amani, mshikamano na matumaini mapya.