Mahakama Yaahirisha Kesi ya Uhaini ya Lissu Hadi Ratiba Mpya – Video – Global Publishers



Kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeahirishwa kwa muda hadi Msajili wa Mahakama atakapopanga ratiba mpya, kwani kesi inasikilizwa kwa vipindi.

Kesi hiyo imeahirishwa baada ya Lissu kuwasilisha hoja mahakamani akipinga chumba kilichopewa shahidi P11, ambaye ni shahidi wa kificho, ambacho kingetumika pia na mashahidi wengine waliolindwa. Lissu alisema kuwa mashahidi waliolindwa wanapaswa kutoa ushahidi wao kwenye kizimba kilicho wazi ambapo jaji au hakimu wanaweza kuwaona, badala ya chumba kilichopo mahakamani ambacho hakiwezi kumuwezesha jaji kuona shahidi pindi kesi inapoendelea.

Aidha, Lissu alisisitiza kuwa sheria inayotumika kuwalinda mashahidi haijachapishwa rasmi katika gazeti la serikali kama inavyohitajika kisheria. Pia, ameeleza kuwa majaji hawajapewa majina ya mashahidi waliolindwa, jambo ambalo linakiuka amri iliyotolewa awali na Jaji Mtembwa. Lissu pia alibainisha kuwa Jamhuri haikuomba ruhusa ya kutumia kizimba maalum cha mashahidi, jambo ambalo linavunja taratibu za kawaida.

Upande wa Jamhuri, ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, uliomba muda wa kutosha kujibu hoja za Lissu kwani zinahitaji majibu ya kisheria na kitafiti.

Kesi sasa inatarajiwa kuendelea mara itakapopewa ratiba mpya na Msajili wa Mahakama.