Dar es Salaam. Baada ya kilio cha muda mrefu cha wadau wa elimu kufuatia kukosekana kwa usimamizi wa uamuzi wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito, Serikali imekuja na mpango wa utekelezaji wa mwongozo huo.
Novemba 24, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza uamuzi wa Serikali kuruhusu kurejea shuleni kwa wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito.
Hatua hiyo ilifuatiwa na mwongozo uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Februari, 2022 ukilenga kutoa fursa ya pili kwa wanafunzi waliokatishwa masomo ili waweze kuendelea na elimu ili kufikia ndoto zao.
Hata hivyo, katika kipindi chote hicho kumekuwa na kusuasua kwa wanafunzi kurejea shuleni katika mfumo rasmi wa elimu hasa wale waliokatiza masomo kwa sababu ya ujauzito.
Kwa sababu hiyo wadau chini ya mwamvuli wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) wamekuwa wakitaka kuwepo na mpango utakaosimamia utekelezaji wa mwongozo huo ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa na ufanisi.
Tayari Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuja na mpango huo ambao umeweka bayana utaratibu na maelekezo ya utekelezaji wa mwongozo wa urejeshwaji wa wanafunzi waliokatisha masomo ili waweze kukalimisha mzunguko wao wa masomo katika mfumo rasmi.
Hili linakuja kipindi ambacho takwimu za wanafunzi wanaokatisha masomo katika ngazi za msingi na sekondari zikiendelea kuwa juu.
Kutoka Machi 2023 hadi Machi 2024 jumla ya wanafunzi 158,378 wa shule za msingi walikatisha masomo kati yao wasichana 68,341 na wavulana 91,033.
Katika kipindi hicho ni wanafunzi 3,402 pekee waliofanikiwa kurudi shuleni kati yao wasichana 1891 na wavulana 1,511.
Kwa upande wa sekondari waliokatisha masomo katika kipindi hicho ni wanafunzi 148,337 kati yao wasichana ni 72,212 na wavulana 76,125.
Waliofanikiwa kurudi shuleni katika kipindi hicho ni wanafunzi 1308 ambao kati yao wasichana ni 675 na wavulana 633.
Kupitia mpango huo imewekwa mikakati ya kina ya kuhakikisha wanafunzi wanaorudi shuleni wanapata msaada wa kisaikolojia na wakingwa dhidi ya unyanyapaa.
Zaidi ya hilo mpango huo unalenga kuhakikisha kunakuwa na maboresho ya mazingira bora ya ujifunzaji ili wanafunzi hao waweze kuendelea na masomo kwa staha na kujiamini.
Mpango huo pia umejumuisha mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na tathmini utakaowezesha kufuatilia na kuhakikisha kila mtoto aliyekatisha masomo anapata fursa ya kurejea na kukamilisha mzunguko wa elimu.
Akizungumza leo Jumatano, Novemba 12, 2025 katika uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dk Hussein Mohamed Omar amesema Serikali inakwenda kusimamia utekelezaji wa mpango huo kuhakikisha hakuna mtoto anayechwa nyuma kwenye upande wa elimu.
Dk Omar amesema wizara yake itasimamia wajibu wa kila mdau aliyetajwa kwenye mpango huo kuhakikisha anatimiza majukumu yake ya kutengeneza mazingira rafiki kwa mtoto aliyekatiza masomo kurejea shuleni.
“Tunakwenda kuunda kikundi kazi kitakachosimamia utekelezaji wa mpango huu, hii haitakuwa wizara ya elimu peke yake, tutashirikiana na wadau wengine kuhakikisha tunakuwa na tathmini katika kila robo mwaka tukiangalia kwa kiasi gani tumefanikiwa na changamoto ni zipi,” amesema.
Dk Omar amebainisha Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unakuwa na ufanisi, jumuishi na endelevu utakaenda sambamba na kampeni maalumu za kutoa elimu kwa umma kuhusu haki ya mtoto kurejea shuleni bila kujali sababu zilizomfanya akatishe masomo.
“Mfumo huu utatusaidia pia katika ukusanyaji wa takwimu sahihi, utengaji wa rasilimali na utunzaji wa taarifa muhimu zitakazowezesha kufanya uamuzi wenye tija kwa maendeleo ya elimu nchini,” amesema Dk Omar.
Akizungumzia hilo mratibu wa TenMet, Martha Makala amesema licha ya Serikali kutoa waraka na mwongozo bado watoto waliokatisha masomo walikutana na vikwazo kadha wa kadha kurudi shuleni hali iliyosababisha wengi wao kuwa nje ya mfumo wa elimu.
“Hili tuliliona, tukashauri na tukasikilizwa na kupewa jukumu la kuratibu hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Tamisemi. Kazi hii imefanyika kwa takribani mwaka mmoja na nusu na leo tunajivunia tuna mpango unaokwenda kusimamia uamuzi huu wenye tija kubwa kwa watoto.
“Ni matumaini yetu kuwa kupitia mpango huu, Serikali, wadau wa maendeleo na mashirika ya kiraia tutaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya elimu bila vikwazo vyovyote,” amesema.
Hata hivyo, Martha ameiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuboresha mfumo wa tahadhari ya mapema kuhusu uachaji wa masomo ili kuwatambua mapema watoto walio katika hatari ya kuacha shule hasa wenye changamoto za kiafya, ulemavu na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.
Amesema kuboreshwa kwa mfumo huo kutasaidia, walimu, wazazi na viongozi wa ngazi za jamii kuchukua hatua za haraka za msaada na ulinzi wa mtoto ili kupunguza wimbi kubwa la wanafunzi wanaokatisha masomo.
Sambamba na hilo amependekeza kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili kupata takwimu sahihi za wanafunzi waliokatisha masomo, waliorejea, waliomaliza na waliofanya vizuri katika mitihani ya Taifa.
Uzinduzi wa mpango huo ulienda sambamba na uwasilishaji wa taarifa ya tathmini ya sera za urejeaji.
Timu ya wataalamu ilifanya utafiti katika mikoa tisa ya Tanzania bara kuangalia utekelezaji wa mwongozo huo.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo mmoja wa watafiti ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taaluma Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Profesa Sempeho Siafu amesema bado kuna kazi kubwa katika ngazi zote kuhakikisha jamii inaelewa dhamira ya Serikali kutoa nafasi nyingine kwa watoto waliokatisha masomo.
“Tulifanikiwa kuzungumza na watu wa makundi mbalimbali wakiwamo walimu, wazazi, wanafunzi na hata hao wasichana waliokatiza masomo kwa sababu ya ujauzito, tulichobaini bado hakuna elewa wa kutosha na unyanyapaa unawafanya wengi wasirudi katika mfumo rasmi.
“Serikali iliruhusu watoto hawa warudi katika mfumo rasmi, lakini kuna urasimu, unyanyapaa na mazingira yasiyo na rafiki kwao hali inayosababisha hata hao wachache wenye shauku ya kurudi shuleni wanakimbilia kwenye mfumo usio rasmi,” amesema Profesa Siafu.