Shinyanga. Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga, Yusuph Zahoro amemhukumu Mackighty Julius kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 17, kinyume na kifungu cha sheria namba 130(2)(e) cha Kanuni ya Adhabu.
Akisoma hukumu hiyo leo Jumatano, Novemba 12, 2025, Hakimu Zahoro amesema kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, mshtakiwa alimuita binti huyo kwenda kuchukua simu aliyodaiwa kuibiwa, ndipo alipombaka.
“Kifungu cha sheria namba 130(2)(e) kinaeleza kuwa mtu atahesabiwa ametenda kosa la kubaka endapo atafanya tendo la ndoa na mtoto wa kike mwenye umri chini ya miaka 18, iwe kwa ridhaa au bila ridhaa yake. Kifungu cha 131(1) kimeweka adhabu ya kifungo cha maisha gerezani kwa atakayepatikana na hatia ya kosa hilo,” amesema Hakimu Zahoro.
Kwa mujibu wa ushahidi, mshtaki ambaye ni shahidi wa kwanza, alieleza kuwa aliporwa simu na mshtakiwa pamoja na mwenzake katika maeneo ya Ngokolo, kisha akaambiwa aifuate simu hiyo eneo la Tambukareli.
Alipofika huko, badala ya kurejeshewa simu yake, alishambuliwa na kubakwa na wanaume hao wawili, mmoja baada ya mwingine.
Mhukumiwa Mackighty Johnstone Julius (17) akitolewa Mahakamani. Picha na Hellen Mdinda.
Wakili wa Serikali, Katandukila Kadata aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa vijana wengine.
“Kosa hili ni zito na linaacha maumivu makubwa kwa waathirika. Ni muhimu adhabu kali itolewe kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hii,” amesema Wakili Kadata.
Licha ya kujitetea, mshitakiwa huyo, Mackighty Julius aliiomba Mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa ana familia inayomtegemea, lakini maombi yake yalikataliwa.
“Mheshimiwa, naomba kupunguziwa adhabu. Nina familia yenye mke, mtoto, mama na bibi ambao wote wananitegemea. Baba yangu alifariki na wadogo zangu wananiangalia mimi. Naomba unisamehe,” aliomba Julius.
Tukio hilo lilitokea Juni 22, 2025, wakati mshtaki akiwa na wenzake watatu walipokuwa wakielekea mitumbani, walisimamishwa na mshtakiwa na mwenzake na kumpora simu yake aina ya TECNO POP 3.
Alipokuwa akijaribu kuifuatilia simu hiyo, alielezwa na mshtakiwa kuwa aifuate eneo la Tambukareli, alikokwenda akiwa ameandamana na rafiki yake mmoja.
Walipofika, bodaboda aliyewapeleka aliwaacha, ndipo mshtakiwa na mwenzake waliwashika kwa nguvu na kuwavuta kuelekea mtoni.
Aliieleza mahakamana kuwa rafiki yake alifanikiwa kukimbia, lakini yeye alivuliwa nguo na kubakwa kwanza na Wilson (anayesakwa), kisha na Julius.
Mhukumiwa Mackighty Johnstone Julius (17) akitolewa Mahakamani. Picha na Hellen Mdinda.
Shahidi wa pili, ambaye ni bodaboda aliyewapeleka eneo hilo, alithibitisha kuwa baada ya kuona mazingira si salama, aliondoka na kwenda kuomba watu wakatoe msaada. Waliporudi, walikuta mshtakiwa anamalizia kuvaa nguo na wakafanikiwa kumkamata, huku mwenzake Wilson akitoroka.
Daktari kutoka Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga pia alithibitisha kuwa mshtaki alifanyiwa kitendo cha kubakwa, akisema kuwa alikutwa na michubuko sehemu za siri na majimaji yenye dalili za shahawa.
Shahidi mwingine, ambaye ni mama mzazi wa mshtaki, alithibitisha kuwa binti yake ana umri wa miaka 17, jambo ambalo halikupingwa na upande wowote.
Hata hivyo, mahakama ilimwachia huru Mackighty Julius katika shtaka la pili la unyang’anyi kwa kutumia silaha, baada ya kushindwa kuthibitishwa mmiliki halali wa simu iliyodaiwa kuibwa. Hakimu alisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai hayo.
Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, Mackighty Julius atatumikia kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kubaka mtoto wa miaka 17, adhabu ambayo imeelezwa kuwa ni ya kisheria na ya kutoa fundisho kwa jamii.