Andabwile, Yanga kuna kitu, Kigogo TFF afafanua

KUNA pande tatu zimetoa kauli mbili tofauti zilizoibua utata wa madai ya fedha za usajili yanayomuhusu kiungo wa Yanga, Aziz Andabwile dhidi ya klabu hiyo ambapo kesi hiyo imefikishwa kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Upande wa kwanza ni wa mtu wa karibu na mchezaji huyo ambapo taarifa za madai zikathibitishwa na TFF, kisha upande mwingine wa Andabwile, mwenyewe akiibuka na kukanusha.

Hayo yote yanafanyika wakati Andabwile ambaye amewahi kuchezea Mbeya City na Fountain Gate kabla ya kutua Yanga, huu ni msimu wake wa pili ndani ya klabu hiyo.

Mwanaspoti linafahamu kwamba, msimu wa 2024-2025, Andabwile alitua Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja, kisha mwanzoni mwa msimu huu akasaini mkataba mwingine utakaomuweka hapo hadi 2027 kwa makubaliano ya kulipwa fedha zake kwa awamu tatu.

Mtoa taarifa amesema: “Andabwile amefungua kesi TFF ya madai ya fedha za usajili na kesi itasikilizwa Alhamisi (kesho) kwenye ofisi za TFF. Madai yake ni kwamba hajalipwa fedha zozote za usajili ambazo zilitakiwa zilipwe Agosti 31, 2025 kwa mujibu wa mkataba wake.”

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura, amesema, ni kweli kesi ya kiungo huyo imefika katika ofisi zao.

“Kamati ina kesi nyingi na kesho tutakuwa tukisikiliza baadhi ikiwemo hiyo ya Andabwile, baada ya kikao hicho maamuzi yatatolewa,” amesema Wambura.

Wakati sakata likiwa linaendelea, Andabwile aliutumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akiandika: “Habari Wananchi. Nipende kuchukua nafasi hii kuliweka sawa jambo linaloendelea mtandaoni kuhusu mimi na Klabu yangu ya Yanga.

“Mimi ni mchezaji wa Young Africans Sports Club na haki zangu za kimkataba tayari nilishalipwa. Niwaombe ndugu waandishi wa habari kuwa na vyanzo sahihi vya taarifa ili kutoleta taharuki kwa wachezaji kwenye Timu zao.

“Mwisho, niwaombe radhi wote ambao wamekwazika na sintofahamu iliyojitokeza. Asanteni.”

Andabwile ambaye kiwango chake msimu huu kimewavutia wengi baada ya kuonyesha uwezo mzuri wakati kikosi hicho kikinolewa na Romain Folz kabla ya ujio wa Pedro Goncalves, amefanikwia kufunga mabao mawili katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu huu akiwa ameuanza vizuri, msimu uliopita 2024-2025, Andabwile alicheza mechi tano pekee kwa dakika 125, akiwa hajafunga wala kuasisti.