KINACHOFANYWA na madaktari wa Azam hivi sasa ni kumpambania kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ awepo kwenye mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Maniema.
Hiyo inatokana na Fei Toto kuumia nyonga katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kuumia kwake kumezua hofu ya kukosekana katika mechi hiyo ya kwanza itakayochezwa Novemba 23, 2025 nchini DR Congo ikiwa ni ya Kundi B.
Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Azam FC, Mbaruku Mlinga, amesema Fei amepata shida ya nyonga ambapo leo mchana walitarajia kumfanyia vipimo kwa kina kufahamu anaweza kuwa nje kwa muda gani.
“Leo mchana ndio tulikuwa na mpango wa kumfanyia vipimo ambavyo vitatoa majibu tutamkosa kwa muda gani kutokana na shida aliyoipata kwa sasa siwezi kuweka wazi ni muda gani tutamkosa hadi hapo vipimo vitakapofanyika,” amesema na kuongeza;
“Ukiachana na Fei Toto pia Azam FC ilikuwa na majeruhi mwingine ambaye ni Yahya Zayd ambaye tayari alifanyiwa vipimo na kubaini ana maumivu kwenye mguu, tayari ameshafanyiwa uchunguzi, nafikiri kabla ya mchezo wetu wa kimataifa atakuwa amerudi mazoezini na ataweza kutumika kama kocha ataona ina ulazima.”
Akizungumzia kuhusu kipa wa timu hiyo, Aishi Manula, alisema alikuwa na matatizo ya kiafya ambayo tayari ametibiwa na anarudi mazoezini kama kawaida tayari kwa maandalizi ya michuano ya kimataifa.
“Kwa ujumla upande wa majeruhi tumebakiza ripoti moja tu ya Fei Toto ambayo itatolewa muda mchache baada ya vipimo ili tujue jeraha lake la nyonga litamuweka nje kwa muda gani,” amesema Mlinga.