Na Mwandishi Wetu
TANZANIA na katika maeneo mengi ya Afrika, wanaume wengi husubiri hadi hali zao za kiafya ziwe mbaya kabla ya kwenda hospitalini. Mara nyingi, maumivu madogo huanza taratibu na kugeuka ugonjwa mkubwa, si kwa sababu huduma hazipatikani, bali kwa sababu kutafuta msaada huonekana kama jambo lisilo la lazima au linalosumbua.
Dkt. Canberth Tibihika kutoka Jubilee Health Insurance anafafanua zaidi kwamba sehemu ya tatizo inatokana na jinsi jamii inavyotafsiri maana ya “uanaume.” Tangu utotoni, wavulana hufundishwa kuwa imara, kujitegemea na wasioonyesha maumivu. Anasema kuwa ujasiri mara nyingi huonekana kama ukimya, na uwezo wa kuvumilia uchungu hupewa heshima kama ishara ya nguvu.
Matokeo yake, wanaume wengi huepuka kukiri wanapojisikia vibaya, wakiamua kuvumilia badala ya kutafuta matibabu. “Kwao, kwenda hospitalini huonekana kama kujisalimisha, ishara ya udhaifu inayopingana na imani walizojengewa tangu wakiwa wadogo. Hata hivyo, nguvu ya kweli ipo katika kuwajibika kwa afya yako, si katika kupuuza dalili za hatari.
“Sababu nyingine ni mtazamo wa huduma za afya kama jambo la kurekebisha tatizo, badala ya kuzuia. Wanaume wengi huenda hospitalini tu wanapopatwa na dharura, wakisahau umuhimu wa vipimo vya mara kwa mara na uchunguzi wa kinga. Huduma za kinga ndizo msingi wa kugundua magonjwa mapema.
Dkt. Canberth Tibihika, anaeleza wasiwasi wa kifedha pia huchangia ucheleweshaji wa kwenda hospitalini. Kwa familia nyingi, wanaume ndio watoa kipato wakuu, na kutumia fedha kwa ajili ya afya zao binafsi huonekana kama anasa.
“Jubilee Health Insurance, kila mara tunatoa elimu jinsi upatikanaji wa bima nafuu unavyobadilisha tabia ya watu kutafuta huduma za afya. Wakati mtu anapokuwa na uhakika kwamba huduma zake za afya zipo salama, anakuwa na ujasiri zaidi wa kutafuta matibabu mapema bila kusita. “Mipango yetu rahisi na inayopatikana kwa urahisi inalenga kuhamasisha huduma za kinga na kuhakikisha watu binafsi na familia wanaweka afya kipaumbele bila mzigo wa kifedha.
“Kubadilisha simulizi kuhusu afya ya wanaume kunahitaji pia mazungumzo ya wazi na mazingira yanayounga mkono. Sehemu za kazi, viongozi wa jamii na familia wanapaswa kuhimiza ufahamu wa afya na kuwatia moyo wanaume kufanyiwa vipimo mara kwa mara.”anasema. Anaongeza kuwa Wanaume wanapoona wenzao na wapendwa wao wakichukulia afya kwa uzito, nao pia huhamasika kufanya hivyo.
Anasisitiza kuhamasisha wanaume kutafuta huduma za afya mapema si suala la kuzuia magonjwa pekee, bali ni njia ya kulinda uzalishaji, uthabiti wa familia na ubora wa maisha. Dkt. Tibihika anaweka wazi afya ndiyo msingi wa nguvu, na kuilinda ni wajibu wa mtu binafsi na jamii kwa ujumla.