-Wananchi wampongeza kwa kuanza kutimiza ahadi yake
-Aapa kukamilisha ujenzi kwa wakati
-Wananchi wamshukuru Rais Samia kwa visima vya umwagiliaji na Umeme
Mbunge wa Jimbo la Mtumba Mh. Anthony Mavunde leo ameshiriki na mamia ya wananchi wa Mtaa wa Maseya-Kata ya Hombolo Makulu kuanzisha ujenzi wa Zahanati katika mtaa huo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa Uchaguzi Mkuu 2025.
“Nawashukuru wananchi wa Maseya kwa kumchagua Rais Samia,mimi na Diwani wa kata yetu kwa kura nyingi sana kwenye uchaguzi mkuu uliomalizika.
Kazi yetu sasa ni kufanya kazi na kutatua changamoto za wananchi,nawapongeza kwa kuitikia wito wa ujenzi wa zahanati yetu ambayo itasaidia kusogeza karibu huduma ya Afya kwa wananchi wetu.
Nitakabidhi matofali 2000 na saruji mifuko 100 ili kulifikisha juu jengo letu mpaka hatua ya upauaji,ni imani yangu kwamba serikali yetu sikivu itatuunga mkono ukamilishaji wa zahanati hii”Alisema Mavunde
Akitoa salamu za wananchi,Mwenyekiti wa Mtaa wa Maseya Ndg. Alexander Fwalu amemshukuru Rais Samia S. Hassan kwa utekelezaji wa haraka wa ahadi ya usambazaji umeme pamoja na uchimbaji wa visima vya umwagiliaji kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ambapo wananchi wengi wakulima watanufaika na kupata maji ya uhakika kwa ajili kilimo cha umwagiliaji.
Aidha pia Mwenyekiti Fwalu amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kutimiza ahadi yake ya kuanzisha ujenzi wa zahanati ya Maseya kwa uharaka na kuahidi kwamba wananchi wa Maseya watatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo inakamilika kwa wakati na hivyo kusogeza huduma ya Afya kwa wananchi.








