Ujue utaratibu, historia ya uwakilishi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Bunge la Tanzania

Unguja. Wakati wengi wakijiuliza kuhusu uchaguzi wa wajumbe watano wa Baraza la Wawakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutofanyika.

Ukweli ni kwamba, wajumbe hao wanatarajiwa kuchaguliwa katika mkutano wa pili wa Baraza la 11, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano Baraza la Wawakilishi, Himid Choko amesema hayo alipozungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 12, 2025.

Mkutano wa pili wa Baraza la Wawakilishi unatarajia kuanza Februari 11, 2026. Hii ni baada ya kuzinduliwa kwa Novemba 10, kisha kuahirishwa hadi Februari, 2026.

Licha ya taratibu takribani zote kukamilika, ikiwemo kuchaguliwa kwa Spika, Naibu Spika, kuapa kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kuzinduliwa rasmi kwa baraza hilo, bado hatua hiyo itasubiri kikao kijacho.

Choko amesema uchaguzi huo upo kikanuni na wakati mwingine unachelewa kutoka na sababu kadhaa ikiwamo ya kusubiri uteuzi wa Rais wa baraza la mawaziri ambao pia wajumbe hao wanaweza kuwa miongoni mwa wateule.

“Watachaguliwa katika mkutano ujao, ni utaratibu wa kanuni za baraza,” amesema Choko.

Wabunge watano kutoka Baraza la Wawakilishi wanaowakilisha bungeni wapo kwa mujibu wa kifungu cha 66 (1) (c ) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Utaratibu wa kupatikana wajumbe wa baraza katika Bunge, kanuni za kudumu za Baraza la Wawakilishi toleo la 2020 zimeweka utaratibu wa kupatikana wajumbe watano watakaowakilisha baraza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kanuni ya 137 ya kanuni za kudumu za Baraza la Wawakilishi zimetaja masharti ya kupatikana kwa wajumbe hao.

Kanuni hiyo inaeleza kuwa; “kila chama chenye wajumbe katika Baraza la Wawakilishi kitakuwa na haki ya kupata mbunge mmoja kwa kila viti 10 ambavyo chama husika kimepata miongoni mwa wajumbe wa kuchaguliwa kwenye majimbo. Isipokuwa chama chenye haki ya kupata wabunge wawili au zaidi basi angalau nafasi moja itakuwa ya mjumbe mwanamke.”

Utaratibu wa uchaguzi wa wajumbe hao ni kwa njia ya kura za siri, kila chama kinawasilisha majina ya wagombea wa nafasi hizo kwa mujibu viti inavyostahiki.

Kila chama kinakuwa na utaratibu wake wa ndani wa kupata majina ya wagombea wa nafasi hizo. Wajumbe wa baraza wanapata nafasi ya kuwapigia kura wajumbe ambao majina yao yamewasilishwa na vyama au chama chao kugombea.

Wabunge hao mara wanapochaguliwa kwenye baraza wanatakiwa kuapishwa bungeni kwa mujibu wa Katiba, sheria na kanuni zinazoendesha Bunge, kwa kuwa wanakuwa na sifa kamili za kuwa wabunge.

Kwa mujibu wa tovuti ya Baraza la Wawakilishi, kuhusiana na suala hilo, baada ya kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964, pamoja na mambo mengine muhimu, liliundwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huo lenye sura ya Muungano, likijumuisha wajumbe wa Bunge kutoka bara na Zanzibar.

Kuanzia kipindi hicho cha mwaka 1964 mpaka mwaka 1980, wajumbe wa Bunge kutoka Zanzibar walikuwa hawachaguliwi kupitia majimbo ya uchaguzi kama ilivyo sasa.

Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi ambalo kwa wakati huo, ilikuwa ndio chombo cha kutunga sheria kwa Zanzibar, walikuwa ndio wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Wakati huo, Baraza la Mapinduzi lilikuwa na wajumbe 30 ambao ndio walikuwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Hivyo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilishiriki moja kwa moja katika shughuli zote bungeni na uamuzi wote uliokuwa ukifanyika bungeni, Serikali ya Zanzibar ilishiriki moja kwa moja.

Mwaka 1979 Zanzibar ilitunga Katiba yake ya kwanza ambayo pamoja na mambo mengine iliunda chombo cha kutunga sheria (Baraza la Wawakilishi).

Baraza la Wawakilishi liliundwa Januari 12, 1980 na mkutano wake wa kwanza wa kulizindua ulifanyika Januari 14,1980 katika Ukumbi wa Mnazimmoja ambao hivi sasa unajulikana kama ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, ambaye alikuwa Spika wa kwanza wa Baraza la Wawakilishi.

Baraza hilo la Wawakilishi lilijumuisha wajumbe kutoka Baraza la Mapinduzi, walioteuliwa na Rais na waliochaguliwa kutoka katika Jumuiya mbalimbali za chama na kamati za wilaya na mkoa.

Kufuatia mabadiliko hayo, Januari 2, 1980, Bunge la Tanzania lilipitisha sheria ya mabadiliko ya pili ya katiba ya mwaka 1977 (sheria namba moja ya 1980) ambayo yaliweka masharti mapya yaliyotokana na kutungwa kwa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979.

Miongoni mwa masharti hayo ni kuweka utaratibu wa kuchagua wabunge kutoka Zanzibar ambapo Baraza la Wawakilishi lilipewa uwezo kuchagua wajumbe wasiozidi 32 kutoka miongoni mwa wajumbe wake na kutoka nje ya baraza hilo.

Marekebisho hayo yaliendeleza ushiriki moja kwa moja wa wajumbe wa baraza kuwa wajumbe wa Bunge kwa idadi iliyoainishwa katika sheria hiyo.

Oktoba 9, 1984, Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilipitisha azimio kutunga katiba mpya ambayo ilifuta Katiba ya mwaka 1979.

Sambamba na hatua hiyo, Oktoba 30, 1984 Bunge lilitunga sheria ya marekebisho ya tano ya katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 (sheria namba 15/1984 ambayo ilifanya marekebisho makubwa katika katiba hiyo.

Mojawapo ni muundo na aina ya wa wabunge kifungu cha 13 cha sheria hiyo kilichorekebisha ibara ya 66 ya katiba  kiliweka idadi ya wabunge watano  kutoka Baraza la Wawakilishi watakaochaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wake ili kuendeleza muunganiko chanya wa vyombo hivyo viwili ulioanzishwa na waasisi wa muungano.

Vilevile, utaratibu huo unaendelea kukumbusha kizazi cha sasa kuwa Bunge la Tanzania limeasisiwa na Baraza la Mapinduzi ambalo kwa wakati huo pia lilikuwa baraza la kutunga sheria za Zanzibar, na baadaye Baraza la Wawakilishi