JKT Queens imeambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast kwenye mechi ya pili kundi B katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake.
Mechi hiyo imepigwa leo Novemba 12, 2025 kwenye Uwanja wa Suez Canal mjini Ismailia nchini Misri na inakuwa sare ya pili mfululizo baada ya mechi ya kwanza kutoa suluhu dhidi ya Gaborone United ya Botswana.
Matokeo hayo yanaifanya JKT kusalia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi B na pointi mbili, hivyo ili ifuzu nusu fainali inahitaji ushindi mechi ya mwisho dhidi ya TP Mazembe ambayo iko nafasi ya pili na pointi tatu.
JKT Queens ilikuwa na nafasi ya kumaliza mechi kipindi cha kwanza ambacho ilionekana kuwa bora kuanzia eneo la ulinzi na kutengeneza nafasi, changamoto ikionekana kwenye umaliziaji.
Wanajeshi hao walitangulia kwa bao la Ester Maseke dakika ya nane akimalizia kona iliyochongwa na kiungo fundi, Donisia Minja.
Hadi kipindi cha kwanza kinaisha, JKT ilikuwa imara ikilinda bao hilo licha ya kupelekewa presha kubwa na Asec.
Hata hivyo, mambo yalionekana kuwa magumu kipindi cha pili baada ya Asec kufanya mabadiliko ikamuingiza Brou ambaye alionekana kuwasumbua mabeki wa JKT.
Dakika ya 82, Asec wakapata penalti baada ya Erika Gnounoue kufanyiwa faulo na Christer Bahera ndani ya eneo la hatari.
Hivyo ukafanya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 1-1 ambayo ili JKT itinge nusu fainali inapaswa kushinda mechi ya mwisho dhidi ya TP Mazembe itakayopigwa Novemba 15, 2025.