TTCL YAJA NA HUDUMA TATU KWA BEI MOJA “FAIBA MLANGONI KWAKO”

::::::::::::::

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi huduma mpya iitwayo Faiba Mlangoni Kwako – T.Fibre Triple Hub, kifurushi cha kisasa kinachojumuisha huduma tatu kwa pamoja: intaneti ya kasi isiyo na kikomo, huduma ya simu ya mezani, na huduma za simu ya mkononi.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam, ukiashiria hatua kubwa ya TTCL katika kuboresha mawasiliano ya kidijitali nchini kwa gharama nafuu na urahisi wa matumizi kwa wananchi, taasisi na wafanyabiashara.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa Masoko wa TTCL, Janeth Maeda, alisema kifurushi hicho kimetengenezwa kwa kuzingatia mahitaji ya Watanzania wanaotaka huduma rahisi kutumia lakini zenye ubora wa hali ya juu.

“Kupitia kifurushi hiki, mteja atapata intaneti ya kasi kwa matumizi ya nyumbani au ofisini, dakika 300 za mawasiliano, pamoja na GB 20 za intaneti kwa simu ya mkononi kwa gharama ya shilingi elfu sabini tu kwa mwezi,” alisema Maeda.

Kwa mujibu wa Maeda, huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za TTCL kuunga mkono ajenda ya serikali ya kukuza uchumi wa kidijitali, kwa kuhakikisha kila nyumba, kila ofisi, na kila mfanyabiashara anapata huduma za mawasiliano za uhakika na za kisasa.

Aliongeza kuwa TTCL itaendelea kubuni huduma bunifu zaidi zitakazoongeza tija na kuimarisha mawasiliano nchini, sambamba na kuendeleza jitihada za kuifanya Tanzania kuwa na mfumo wa mawasiliano unaokidhi mahitaji ya dunia ya kisasa.