Arusha. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) leo umezindua mahema 40 ya kisasa (semi-luxury tents) ili kuboresha huduma za malazi na kuongeza mvuto wa hifadhi zake kwa watalii. Tukio hilo limefanyika katika kiwanda cha TARPO, jijini Arusha, likihusisha wawakilishi wa vituo vya utalii vilivyopewa mahema hayo.
Mahema hayo yatasambazwa katika hifadhi za Pugu–Kazimzumbwi (10), Vikindu (4), Rau (5), Kondoa Rock Arts (2), North Kilimanjaro–Rongai (5), West Kilimanjaro (10) na Magamba (4), ambapo vituo hivyo vimechaguliwa kutokana na wingi wa watalii na umuhimu wake katika kukuza mapato ya utalii.
Afisa Utalii wa TFS Makao Makuu, Salome Letore Kivuyo, alisema mahema hayo yanalenga kuboresha huduma za malazi ndani ya hifadhi, kuongeza siku za kukaa watalii na kuongeza mapato.
“Tenti hizi ni za kisasa, zikiwa na vitanda, magodoro na vifaa bora vitakavyowezesha watalii kupata huduma bora na salama wanapolala ndani ya hifadhi. Tunataka wageni wafurahie misitu yetu wakiwa na starehe na usalama wa hali ya juu,” alisema Kivuyo.
Aliongeza kuwa kabla ya kupelekwa kwenye hifadhi husika, Wahifadhi wa TFS walipatiwa mafunzo maalumu ya namna ya kuzifunga, kuziendesha na kuzitunza tenti hizo, kuhakikisha zinadumishwa kwa kiwango cha juu na zinawahudumia watalii kwa usalama.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi wa Kituo cha Michoro ya Miamba Kondoa, Zuberi Mabie, alisema uwekezaji huo utasaidia kuongeza idadi ya wageni na kuimarisha uchumi wa jamii zinazozunguka hifadhi.
“Watalii wanapopata huduma bora, wanakaa muda mrefu zaidi, jambo linaloongeza mapato kwa jamii na serikali. Tunawakaribisha familia na makundi mbalimbali kufurahia urithi wa nchi yao katika mazingira salama na yenye utulivu,
“Wito wangu kwa makampuni ya utalii na waongoza wageni ni kuendelea kuuza vifutushi, hasa utalii wa kupiga kambi (camping), kwa sababu miundombinu wezeshi kwa watalii, hasa upande wa malazi, imeboreshwa kwa viwango vyenye ubora unaokubalika kwa watalii wa ndani na nje ya nchi,” alisema Mabie.
