Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameziacha wazi wizara nne kati 20 alizoziunda na kuteua mawaziri wake kwa ajili ya ACT Wazalendo endapo chama hicho kitaamua kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Chama hicho kimekidhi vigezo vya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kushirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) na sasa kitakuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na mawaziri wanne, badala ya wawili waliokuwepo awali.
Wizara walizoachiwa ACT Wazalendo ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Wizara ya Afya na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale.
“Hizi nafasi zitabaki wazi kwa mujibu wa katiba mpaka pale kipindi kitakapokwisha ambacho kikatiba ni siku 90,” amesema Dk Mwinyi.
Akizungumzia ACT Wazalendo kuachiwa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Dk Mwinyi amesema wamefanya hivyo kwa utashi mwema kuwaachia wenzao wizara hiyo inayoongoza uchumi wa Zanzibar.
“Sekta kuu ya uchumi hapa Zanzibar ni utalii, basi tumeona tuwe na good will (matashi mema), sekta kiongozi tuwape wao,” amesema Rais huyo.
Mabadiliko mengine aliyoyafanya Rais Mwinyi ni kupunguza wizara katika ofisi yake kwani katika kipindi kilichopita, kulikuwa na wizara nyingi ambazo ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais Tamisemi na Idara Maalumu, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji na Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango.
“Nimeamua kuziondoa mbili kati ya hizo, zibaki nje ya Ofisi ya Rais na mbili zitaendelea kubaki chini ya Ofisi ya Rais. Itakayobaki chini ya ofisi ya Rais ni Ofisi ya Rais Ikulu na Ofisi ya Rais, Tamisemi na Idara Maalumu.
“Zitakazotoka na kuwa wizara zinazojitegemea ni Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kazi na Uwekezaji,” amesema kiongozi huyo.