Wawili wahukumiwa kunyongwa kwa mauaji baada ya kupora pochi

Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, imewahukumu kunyongwa hadi kufa Sharifu Rajabu na Muumin Tembo baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya Edes Chami. Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Thadeo Mwenempazi Novemba 10, 2025 na nakala yake inapatikana katika tovuti ya Mahakama.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Mahakama imebaini bila kuacha shaka kuwa washtakiwa hao walimvamia marehemu, wakampiga kwa kitu kizito kichwani, kisha kumuibia pochi iliyokuwa na fedha taslimu Sh240,000, simu ya mkononi aina ya Infinix Hot 9 yenye thamani ya Sh400,000 pamoja na kadi za benki.

Tukio hilo lilitokea Julai 5, 2023 katika eneo la Kashato wilayani Mpanda, Edes alifariki dunia Julai 23, 2023 katika Hospitali ya Bugando kufuatia majeraha makubwa aliyoyapata kichwani.

Aidha, Mahakama ilimuachia huru aliyekuwa mshtakiwa wa tatu, Charles Antipass baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha ushiriki wake katika mauaji hayo.

Jaji Mwenempazi alisema, “Nimeridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha bila shaka kwamba washtakiwa wa kwanza na wa pili walitenda mauaji haya kwa nia ovu. Kwa mujibu wa sheria, ninawahukumu kunyongwa hadi kufa.”

Ushahidi ulivyowasilishwa mahakamani

Baba wa marehemu, Emmanuel Chami (shahidi wa nne), alieleza mwanawe alimjulisha kuwa alivamiwa na kuibiwa pochi yenye fedha na simu.

Baada ya kutoa taarifa polisi, marehemu alilazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda kabla ya hali yake kuzorota na kuhamishiwa Katavi, kisha Bugando ambako alifariki dunia.

Dk Alex Mremi (shahidi wa sita), aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, alisema kifo kilisababishwa na jeraha kubwa la kichwa lililosababisha kuvuja damu ndani ya fuvu kutokana na kupigwa kwa kitu kizito butu.

Upelelezi wa tukio hilo uliongozwa na Inspekta Godfrey Leka (shahidi wa kwanza), ambaye alifuatilia simu ya marehemu hadi ilipopatikana kwa Matilda Festo (shahidi wa pili) katika eneo la Nsemulwa.

Matilda alidai alinunua simu hiyo kutoka kwa mtu aliyejulikana kama Japhet Abel kwa Sh140,000.

Baada ya kukamatwa, Japhet alikiri kuhusika na kuwataja washirika wake. Hata hivyo, aliuawa na wananchi wenye hasira muda mfupi baada ya kukamatwa. Polisi walitumia maelezo yake kuwakamata Sharifu na Muumin Novemba 15, 2023 katika Mtaa wa Fisi, Mpanda.

Maelezo ya onyo ya washtakiwa hao, yaliyopokelewa mahakamani kama vielelezo, yalionesha kukiri kwao kushiriki katika tukio la kumpiga na kumuibia marehemu.

Sharifu alidai kukamatwa kwa tuhuma za wizi wa runinga na siyo mauaji, huku akikana kumfahamu marehemu au washtakiwa wenzake.

Muumin naye alidai kukamatwa kwa tuhuma za kuvunja duka na kuiba na kwamba, alijulishwa baadaye kuwa anatuhumiwa kwa mauaji.
Charles, mshtakiwa wa tatu, alieleza kuwa alikamatwa kwa madai ya kuwaweka wahalifu dukani kwake ambako hufanya kazi ya DJ na kuingiza nyimbo kwenye flash drive, akikanusha kuhusika na mauaji hayo.

Jaji Mwenempazi alisema katika kesi za mauaji, ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha bila kuacha shaka kwamba washtakiwa walitenda kosa kwa nia ovu.

Aliongeza kuwa maelezo ya onyo ya washtakiwa wa kwanza na wa pili yalithibitishwa kuwa yalitolewa kwa hiari yao na yalionyesha wazi ushiriki wao katika shambulio lililosababisha kifo cha Edes.

Alisema baada ya kupitia ushahidi wote, Mahakama iliwatia hatiani Sharifu Rajabu na Muumin Tembo kwa kosa la mauaji na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa kama sheria inavyotaka.

Kwa upande mwingine, Charles Antipass aliachiliwa huru baada ya Mahakama kubaini kuwa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja wala wa kimazingira unaomuunganisha na kosa hilo.