Mngazija apania kuipandisha JKU | Mwanaspoti

BAADA ya Ali Bakar Mngazija kutambulishwa kuwa kocha mkuu wa JKU, ameahidi kuipa hadhi timu hiyo kwa kufanyakazi kwa ushirikiano ili kuiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar.

Mngazija amechukua nafasi ya Seif Bausi aliyesitishiwa mkataba baada ya kuiongoza katika mechi saba za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu wa 2025-2026, kati ya hizo imeshinda moja, sare nne na kupoteza mbili, ikivuna alama saba.

Kocha huyo amesema, licha ya kukabidhiwa kikosi hicho kikiwa hakipo nafasi nzuri, lakini atatumia mbinu zake kuiweka katika nafasi inayostahili.

Mngazija amesema kwa upande wa wachezaji, wapo vizuri, kinachotakiwa ni kuwaandaa kwa kuwapa elimu ya kisaikolojia, pamoja na mbinu za kuwashinda wapinzani wanapokuwa uwanjani.

“Nahitaji wachezaji na viongozi kunipa ushirikiano kuijenga timu yetu kwani hiyo ndio sababu kubwa ya kufanikiwa kwetu,” amesema.

Mbali na hilo, Mngazija amesema mechi yao ya jana dhidi ya New King, ni kipimo kizuri katika kutambua udhaifu wao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hapo awali na Katibu Mkuu wa JKU, Khatib Shadhil, kocha huyo atakuwapo kwa muda hadi dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa.

Katibu huyo amesema, endapo akifanya vizuri, watafanya naye mazungumzo kwa lengo la kumaliza msimu huu.

Kabla ya mechi ya jana ambayo JKU ilicheza dhidi ya New King, ilikuwa nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikikusanya pointi saba katika mechi saba ilizocheza.