Cheche ataja tatizo Chama la Wana

BAADA ya kucheza dakika 270 bila ushindi, kocha mkuu wa Stand United, Idd Nassor ‘Cheche’ amesema tatizo lililowatesa amepata mwarobaini wake sasa kazi inaanza rasmi akiivimbia Kagera Sugar.

Stand United iliyowahi kutamba Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja misimu mitano nyuma, msimu uliopita wa Ligi ya Championship ilicheza playoff ya kupanda daraja lakini hesabu ziligoma dakika za mwisho.

Msimu huu timu hiyo yenye mashabiki wengi mjini Shinyanga, imeonekana kutokuwa na mwanzo mzuri baada ya kucheza mechi tatu bila ushindi wala sare na kujikuta nafasi ya 13.

Akizungumza na Mwanaspoti, Cheche amesema kilichowapa ugumu katika mechi tatu za mwanzo ni kutoanza nao mapema maandalizi hali iliyompa ugumu kutengeneza mfumo, muunganiko na masuala mengine ya kifundi.

Amesema pamoja na kutoanza vizuri, lakini dakika 270 zimewapa utimamu wachezaji hivyo kuanzia mechi ya kesho dhidi ya Kagera Sugar, huko Kaitaba, mjini Bukoba wataanza kuamka upya.

“Nilifika kikosini wiki moja kabla ya ligi kuanza, sikupata muda mzuri na wa kutosha kuijenga timu na ndio sababu ya matokeo hayo, lakini kwa sasa vijana wameimarika kiasi fulani na matarajio yangu mchezo ujao tutakuwa imara,” amesema Cheche beki wa zamani wa Sigara.

Kocha huyo aliyewahi kuzinoa timu kadhaa ikiwamo Azam FC, aliongeza kinachompa matumaini ni jinsi wachezaji wanavyojituma, kwani mbali na kupoteza mechi tatu, lakini wamefunga bao.

Aliongeza upungufu uliopo katika timu hiyo ataufanyia kazi wakati wa dirisha dogo, akitoa matumaini kwa mashabiki kuwa Chama la Wana litafanya vizuri akiomba sapoti yao.