Naby Camara anavyojitofautisha Simba, mwenyewe afichua jambo

KUTOKA CS SFaxien ya Tunisia, kisha Al-Waab SC ya Qatar, Naby Camara raia wa Guinea, uwezo wake kwa sasa unaonekana ndani ya kikosi cha Simba alichojiunga nacho kipindi cha usajili wa dirisha kubwa msimu huu.

Akiwa na uwezo wa kucheza nafasi takribani tisa ndani ya uwanja kwa maana ya beki wa kushoto, beki wa kulia, beki wa kati namba nne na tano, kiungo mkabaji namba sita, kiungo wa juu namba nane, namba saba, kumi na 11, nyota huyu anayetumia zaidi mguu wa kushoto anatajwa kuwa moja kati ya sajili ya maana iliyofanywa na Simba.

Camara ni miongoni mwa wachezaji 13 wapya waliosajiliwa na Simba msimu huu, wengine ni Yakoub Suleiman (kipa), Vedastus Masinde (beki wa kati), Wilson Nangu (beki wa kati), Anthony Mligo (beki wa kushoto), Rushine De Reuck (beki wa kati), Alassane Kanté (kiungo wa kati), Morice Abraham (kiungo wa kati), Mohammed Bajaber (kiungo mshambuliaji), Hussein Semfuko (kiungo wa kati), Jonathan Sowah (mshambuliaji), Seleman Mwalimu (mshambuliaji) na Neo Maema (kiungo mshambuliaji).

Kati ya hao wote, Camara mwenye umri wa miaka 23, ndiye mchezaji pekee ambaye leo unaweza kumuona ameanzishwa beki wa kushoto, ndani ya mechi hiyohiyo akahamishwa kucheza kiungo mkabaji, kisha akamaliza akiwa kiungo mshambuliaji na nafasi zote hizo akazimudu ipasavyo.

Hilo lilidhihirika katika mechi ya kwanza ya kirafiki katika Tamasha la Simba Day ambapo Simba ilicheza dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, Septemba 10, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo, Camara alianza kucheza kiungo namba nane, kipindi cha pili alipofanyiwa mabadiliko Antony Mligo ambaye ni beki wa kushoto na kuingia Morice Abraham anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, Camara akalazimika kurudi kucheza beki wa kushoto. Katika mechi hiyohiyo, kuna wakati alikuwa anamuacha Ladack Chasambi ambaye alianzishwa kama beki wa kulia, apande juu, kisha yeye anakuja kuziba nafasi yake.


Katika mechi hiyo ambayo Simba ilishinda 2-0, Camara alicheza dakika zote tisini sambamba na beki wa kati Rushine De Reuck ambao ndiyo wachezaji wapya pekee waliosajili na Simba waliofanikiwa kufanya hivyo siku hiyo.

Septemba 16, 2025 katika mechi ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga iliichapa Simba bao 1-0, Camara alianza nafasi ya beki wa kushoto, akamaliza dakika zote tisini.

Baada ya mechi hiyo, Simba ikaenda Botswana kukabiliana na Gaborone United, ikiwa ni mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali. Wakati Simba ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini, Camara alicheza dakika zote tisini eneo la kiungo mkabaji. Hiyo ilitokana na kukosekana kwa Yusuph Kagoma aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata msimu uliopita katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba iliporudi nyumbani kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate na kushinda 3-0, Camara alicheza beki wa kushoto akitumika kwa dakika zote tisini.

Mechi mbili zilizofuata dhidi ya Gaborone United (Ligi ya Mabingwa) iliyomalizika kwa matokeo ya 1-1 na Namungo (Ligi Kuu) Simba ikishinda 3-0, Camara aliishia kukaa benchi.

Akaja kuonekana tena uwanjani Simba ilipokwenda Eswatini kukabiliana na Nsingizini Hotspurs, mechi ya hatua ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda kwa mabao 3-0.


Siku hiyo, Camara alicheza nafasi mbili tofauti kwa dakika zote tisini. Alianza kama kiungo mkabaji, kisha akawa kiungo mshambuliaji alipoingia Yusuph Kagoma kipindi cha pili.

Marudiano dhidi ya Nsingizini hakucheza, akaja kuzima dakika zote tisini Simba iliposhinda 2-1 dhidi ya JKT Tanzania katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Novemba 8, 2025 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar ambapo Camara alianza kama kiungo mshambuliaji, kisha akamaliza katika mfumo wa mabeki wa tatu.

Utulivu na kujiamini huku akiwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi ndefu zinazofika kwa walengwa, ndiyo silaha kubwa ya Camara inayomfanya awe bora ndani ya uwanja kwani anapokuwa na mpira mguuni, ni ngumu kuupoteza kutokana na umakini alionao na kujiamini kwake. Ana uwezo mkubwa wa kuhimili presha ya mpinzani.

Hata hivyo, wakati mwingine mechi ikiwa inaendelea kutokana na uhodari wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja, kocha humtumia katika mfumo wa mabeki wa tatu anapobadili mbinu zake anaposaka ushindi.

Katika mfumo huo wa mabeki wa tatu, Camara anakuwa sambamba na Rushine De Reuk na Wilson Nangu, wakati mwingine Chamou Karaboue. Mechi dhidi ya JKT Tanzania, wakati Simba ipo nyuma kwa bao 1-0, Kocha Dimitar Pantev na mwenzake Seleman Matola, walifanya mabadiliko ya wachezaji watano kwa wakati mmoja. Eneo la ushambuliaji alimtoa Steven Mukwala na kuingia Jonathan Sowah, akatolewa kiungo mkabaji Yusuph Kagoma akaingia kiungo mshambuliaji Alasane Kante. Pia eneo la kiungo mshambuliaji wakatolewa Neo Maema, Kibu Denis na Joshua Mutale, wakaingia Jean Charles Ahoua, Elie Mpanzu na Morice Abraham.


Mabadiliko hayo yakafumua mfumo wa awali, Simba ikawa inacheza mtindo wa mabeki watatu kutoka wanne ilivyokuwa ambapo Camara alirudi nyuma kabisa kuungana na mabeki wa kati Rushine De Reuck na Wilson Nangu. Antony Mligo aliyekuwa anacheza beki wa kushoto na Shomari Kapombe beki wa kulia, wakawa muda mwingi wamepanda juu kuongeza nguvu katika ushambuliaji. Hapa Camara alikuwa katikati, kushoto Nangu, kulia De Reuck.

Katika kipindi hiki cha ligi kusimama kupisha kalenda ya FIFA, Camara amejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Guinea kwa ajili ya mechi ya kirafiki ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ajiunge na Simba.

Camara ni uti wa mgongo wa Simba, huku akifanikiwa kucheza mechi tano kati ya nane za mashindano akiwa na jezi ya Simba yenye namba 30 mgongoni. Katika mechi hizo tano, ameanza zote na kumaliza, hivyo ametumika kwa dakika 450. Bado hajafanikiwa kufunga wala kuasisti.

Katika nafasi ambazo anaweza kuzicheza, pale Simba kila idara imeenea ambapo beki wa kulia kuna Shomari Kapombe na David Kameta ‘Duchu’, kushoto unamkuta Antony Mligo. Katikati wapo Rushine De Reuck, Wilson Nangu, Vedastus Masinde, Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue.

Kiungo mkabaji kuna Yusuph Kagoma na Mzamiru Yassin. Kiungo cha juu wapo Alasane Kante, Morice Abraham, Mohamed Bajaber na Semfuko Charles.

Akielezea furaha yake ya kucheza katika nafasi mbalimbali uwanjani, Naby Camara amesema uhuru aliokuwa nao umechangia kufanikisha hilo.


“Nimekuwa huru kucheza nafasi yoyote, kila nafasi na majukumu ambayo nimepewa nimekuwa huru kuyafanya,” amesema Camara.

Camara ameendelea kueleza kwamba uwezo wake wa kubadilika umeongeza thamani yake katika timu alizozitumikia.

“Kuna siku unahitaji kushiriki katika kujenga mashambulizi, siku nyingine unalinda katikati ya uwanja. Kuwa huru kucheza katika nafasi zote kunanifanya nijisikie muhimu kwa timu,” ameongeza mchezaji huyo.

Pamoja na hilo, Camara amesema changamoto za kucheza nafasi tofauti imekuwa ikimfanya kujifunza kila wakati ili kuwa bora na tayari kutumika.

“Kila nafasi ina sifa zake na changamoto, lakini pia fursa za kujifunza,” amehitimisha.