Dar/mikoani. Dk Mwigulu Nchemba ndiye Waziri Mkuu wa 12 akivaa viatu vya Kassim Majaliwa.
Rais Samia Suluhu Hassan amempa jukumu la kuwa Msimamizi wa shughuli za Serikali.
Uteuzi wake haukutarajiwa na wananchi wameupokea kwa mitazamo tofauti.
Sehemu ya mijadala iliyopo leo Alhamisi Novemba 13, 2025 baada ya kuteuliwa ni pamoja na zile kauli zake alizowahi kuzitoa akiwa Waziri wa Fedha mathalani ya wasiotaka kulipa kodi wahamie Burundi.
Mijadala mingine ni ya kumsaidia Rais Samia kuliunganisha Taifa, kudhibiti ubadhirifu, nidhamu serikalini na kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030.
Saa chache baada ya jina lake kuwasilishwa bungeni kwa Spika wa Bunge, Mussa Zungu na Mpambe wa Rais (ADC), Brigedia Jenerali, Nyamburi Mashauri kwa ajili ya Bunge kumthibitisha, Mwananchi ilizungumza na wananchi kupata mitazamo yao.
Dk Mwigulu mwenye miaka 50, ameshika wadhidha mbalimbali ndani ya Serikali ikiwamo, mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri wa Fedha na ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu-Bara.
Mchambuzi wa siasa, Dk Onesmo Kyauke amesema kibarua kilichopo mbele ni Dk Mwigulu kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030, kwa sababu yeye ni kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni.
“Kazi kubwa iliyopo mbele ni kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa ilani na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Mambo yote yapo katika ilani, hata ukisema maridhiano au Katiba Mpya yapo huko,” amesema Dk Kyauke.
Hata hivyo, amesema ingawa uteuzi wa Dk Mwigulu haukutarajiwa, lakini ana imani na utendaji wa kiongozi huyo, akisema yupo vizuri.
Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi na Kilimo, Chuo cha Mipango ya Maendeleo, Dk Rogers Lumenyela amesema Dk Mwigulu ndiye msimamizi wa masuala yote ya Serikali, hivyo kibaru cha kwanza ni kutuliza hali iliyojitokeza ili kuwe na umoja ndani ya Taifa.
“Sasa hivi vijana wanaangalia Taifa linakwenda wapi, wakiwamo wasiokuwa na ajira, je Dk Mwigulu atasimamiaje mipango endelevu ya Serikali ili kutengeneza fursa za Kundi hilo,” amesema.
“Hayo ndio ya msingi yanayopaswa, lakini jingine ni usimamizi wa rasilimali zetu hili jambo kubwa sana. Kama rasilimali hazitasimamiwa hatutapata manufaa na Taifa litaendelea kuwa maskini, huwa nasema Taifa haliwezi kuendelea kwa kutegemea uwekezaji kutoka nje.”
Dk Lumenyela amesema pamoja na mambo mengine, Dk Mwigulu anapaswa kuhakikisha Taifa linajenga uwezo wa ndani, ili nchi isonge mbele, isipofanyika hivyo, huenda taifa likaendelea kulia njaa.
“Ninachomuombea ni kujenga uwezo wa ndani wa Taifa, si kutegemea kukusanya mirahaba, wakati ndani hatuzalishi. Haya ni mambo machache yaliyopo mbele yake na presha inakuwa kwa sababu vijana wanazaliwa na kukua, huku ajira hakuna, lazima watumie busara ya hali ya juu,” ameeleza Dk Lumenyela.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben amesema utekelezaji wa miradi iliyopo na mipya iliyopo katika Dira ya Taifa 2050 ni miongoni mwa majukumu yanayomsubiria Dk Mwigulu katika majukumu yake mapya.
“Ana kazi kubwa ya kuangalia miradi mikubwa ambayo ipo katika hali mbaya au imeharibika kutokana na kilichotokea Oktoba 29. Katika nafasi yake ahakikishe anawasaidia wananchi kuondokana na adha ya usafiri au upatikanaji wa huduma katika majengo yaliyoharibiwa,” amesema Dk Reuben.
“Hiki ni kibarua pia kwake kwa sababu hapo panahitajika, bajeti na mpango madhubuti utakaotathimini hasara ili kurejesha mazingira katika hali ya kawaida.”
‘Kuliunganisha Taifa’
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Juma Ali Khatib amesema Dk Mwigulu ana kazi ya kuliunganisha Taifa ili wananchi kuwa kitu kimoja na kubuni mbinu za kuwasaidia vijana wasiokuwa na ajira.
“Serikali ifikirie namna ya kuwasaidia vijana ili kujikwamua kimaisha na kutoa elimu ya uraia kwa kundi ambalo unaweza kusema kama vile linaanza kupoteza mwelekeo. Leo hii watu wanakwenda kuchoma miundombinu na kuharibu mali za umma na binafsi,” amesema Khatib.
“Ana kazi kubwa ya kumsaidia Rais Samia, nina uhakika ana uwezo Dk Mwigulu, kinachotakiwa ni kujitoa zaidi. Tuna kazi kubwa mbele ya kuijenga nchi yetu ili kuondokana na kadhia iliyopita, pia kuna umuhimu wa mchakato wa Katiba ukaanza mapema.”
Mchambuzi mwingine wa siasa, Said Miraj amesema kurudishwa kwa umoja wa kitaifa ni miongoni mwa mambo yanayomkabili Dk Mwigulu kwa sababu ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali.
“Anatakiwa asimamie utekelezaji wa vitendo kuhusu 4R za Rais Samia, tuanze kuona tunapata maridhiano, tunavumiliana na unajenga upya. Hiki ni kipindi kigumu, kwa sababu kuna fukuto na mvutano wa kisiasa unaoendelea kimyakimya.
“Haya yote huwezi kufanikiwa kujenga uchumi ikiwa nchi haiko imara katika siasa. Hili ni jambo muhimu linalomtazama Dk Mwigulu, sambamba na kuhakikisha uchumi unakuwa kwa haraka, kuboresha huduma na hali za wananchi,” amesema.
Mbali na hilo, Miraj amesema Dk Mwigulu ana kazi ya kusimamia maadili, nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma,jambo ambalo analopaswa kulitazama.
“Pia, kuna suala jingine la kurudisha matumaini na kutimiza ndoto za makundi tofauti hasa vijana waliokuwa na malalamiko mengine, imekuwa ndio kitu cha mambo mengi.
“Ni namna gani Dk Mwigulu ataweza ‘kudeal’ na vijana, kuwajengea matumaini mapya, sambamba na kuwahakikishia hali inaweza kubadilika. Haya anapaswa kuyaangalia Dk Mwigulu, pia aangalie zaidi utaifa siu chama katika utendaji kazi wake,” ameeleza Miraj.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Sola, Wilaya ya Maswa, Spora Kweka amesema Dk Mwigulu ni kiongozi mwenye nidhamu, uzoefu wa uongozi na mzalendo.
“Tunatarajia ataweka msisitizo mkubwa kwenye elimu, hasa maeneo ya vijijini ambako bado kuna changamoto za uhaba wa walimu na miundombinu duni,” amesema Kweka.
Mfanyabiashara wa mjini Mwanhuzi Wilaya ya Meatu, James Jisehna amesema uteuzi huo ni hatua chanya kwa maendeleo ya uchumi wa nchi, kwani kiongozi huyo anauelewa mpana wa masuala ya fedha.
“Tunategemea atapunguza urasimu kwenye utoaji wa vibali vya biashara na kuboresha mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati,” amesema Jisehna.
Rehema Mushi, mkazi wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro ambaye anaamini uzoefu wa kiongozi huyo serikalini utamuwezesha kusimamia vyema utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi, hususan maeneo ya vijijini.
James Hamis, mkazi wa Songwe amesema Dk Mwigulu kuwa Waziri Mkuu ni uamuzi sahihi uliofanywa na Rais Samia kwa kuwa, amekuwa akifanya ziara za wananchi na kusikiliza changamoto, jambo ambalo ni ishara ya uwazi na kiongozi anayejali wananchi.
“Kwa mfano, alitangaza kwa umma kwamba Serikali imepokea maoni ya wananchi kuhusu tozo za miamala ya kielektroniki na inazifanyia kazi, tuliona fedha hizohizo zimeboresha na kujenga miundombinu ya miradi ikiwepo barabara,” amesema Hamis.
Mkazi wa Mjini Babati, mkoani Manyara, Omary Haji amesema Dk Mwigulu ni kiongozi atakayemudu kuishi katika changamoto za kijamii kwa kuwa, ametoka katika familia ya kawaida, hivyo siyo kiongozi wa kujikweza.
“Atakuwa Waziri Mkuu wa vitendo siyo mtu wa kujikweza au wa kujiona ni kiongozi madhubuti wa kujishusha na mtendaji na tutarajie atakuwa hivyohivyo,” amesema Haji.
Mkazi wa Buswelu, wilayani Ilemela, Mkoa wa Mwanza, Hamis Omary amesema ni mapema kutabiri Dk Mwigulu atakuwa Waziri Mkuu wa namna gani.
“Siwezi kumweka kwenye kundi la kiongozi mbaya au kiongozi mzuri maana ukimsikiliza wakati anaongea ni mtu ambaye anaonekana ana msimamo, mfano alipotoa taarifa kuhusu ongezeko la deni la Taifa alikuwa wazi hakutaka kuficha, akiendelea hivyo ni kiongozi bora” amesema Omary.
Mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza, Joyce Jovin, amesema Serikali imeonesha mwendelezo wa kupuuza maoni na matakwa ya wananchi.
“Kama tu alikuwa Waziri wa Fedha alikuwa na kutoa majibu ambayo si ya kiungwana kwa wananchi ambao kiuhalisia maoni yao yalipaswa kusikiliwa na kutolewa majibu yanayoridhisha, yeye akawa anajibu anavyotaka, hivi amekuwa Waziri Mkuu itakuwaje? binafsi sina imani naye,” amesema Joyce.
Kauli hiyo inatokana na kipindi ambacho wananchi walilalamikia tozo za miamala inayofanywa kwa simu kuongezeka na majibu yake aliwataka wananchi kuhamia Burundi.
Baadhi ya wananchi wameweka wazi hisia zao baada ya kutangazwa jina la Waziri Mkuu Dk Mwigulu.
Kupitia maoni waliyoyatoa katika mitandao ya kijamii ya Mwananchi, wameweka matumaini yao na wengine hisia zao baada ya uteuzi huo na kuthibitishwa na Bunge.
“Tunampongeza kwa dhati Dk Mwigulu Nchemba kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni uteuzi wa kihistoria unaoonesha uthabiti wa Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha inaweka viongozi bora na wenye uwezo wa kuongoza kwa ufanisi. Dk Nchemba ni kiongozi mwenye maono, maarifa na uzoefu wa kutosha katika utawala, na ni matumaini yetu kwamba atafanya kazi nzuri katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya Taifa letu,”ameandika The_voiceless_man_07.
“Dk Mwigulu Nchemba ni kiongozi anayeweka mbele masilahi ya Taifa kuliko masilahi binafsi,” ameandika Furahinimasawe
“Tunampongeza Dk Mwigulu Nchemba kwa kuwa chanzo cha matumaini mapya kwa kizazi cha sasa,” ameandika Wclel1jy.
“Kuna wakati uteuzi wa kiongozi fulani unaweza ukawa ni kuzuiliwa kujiandaa na matajario fulani ya baadae. Akili kubwa imetumika hapa. Hii ndio siasa. Ni mtazamo wangu,” ameandika Cliff_leonardmkahala.
“Hongera sana Dk Mwigulu. Mungu akupe hekima na nguvu uweze kutimiza matarajio ya Watanzania,” ameandika Godlisten_Minja.
“Dk Mwigulu Nchemba ni kiongozi wa mfano anayethamini kazi na uwajibikaji kwa kila nafasi,” ameandika Petermwanzala.
“Mwigilu hizo ni zile sadaka unazotoa madhabahuni kila mara zimekuwa ukumbusho mbele za Mungu majibu yake ndo hayo fanya kazi umepata kibali,” ameandika Hhorkipanga8.
“Atatusikilizaje wakati kipindi kile hakutaka kutusikiliza akasema tuhamie Burundi,” ameandika Sarah_cosmetics_tz.
“Kila la kheri na Allah akusimamie katika matendo na sio maneno maana Watanzania wanataka vitendo na sio maneno,” ameandika Eden_hamad_jr.