KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi ya kwanza ya makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola, lakini kuna taarifa moja inayoshtua baada ya kipa namba moja wa timu hiyo ya Msimbazi, Moussa Camara kuamua kuwagomea mabosi wake kama utani.
Huenda unajua, kwa sasa kipa huyo raia wa Guinea hajaonekana uwanjani kutokana na kuwa majeruhi na nafasi yake kwa sasa imezibwa na Yakoub Suleiman akisaidiwa na Hussein Abel.
Mabosi wa Simba katika kuhakikisha kipa huyo anarudi mapema uwanjani walipanga wampelekea nje ya nchi ili afanyiwe upasuaji, lakini bila kutarajiwa Camara amegomea upasuaji huo na tayari vigogo wa Msimbazi wameanza hesabu mpya za mapema za kutafuta kipa mwingine wa kuokoa jahazi.
Camara aliyetua Simba msimu uliopita na mwishoni mwa msimu huo kuongeza mkataba wa mwaka mmoja utakaomalizika mwisho wa msimu huu, alipata majeraha katika mechi ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana iliyomalizika kwa sare ya 1-1 na kuwafanya Wekundu hao kutinga raundi ya pili na mechi zote zikidakwa na Yakoub Suleiman.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezinasa ni kwamba, Camara bado hajakubaliana na uamuzi wa kwenda kufanyiwa upasuaji.
“Mgomo wa Camara umeifanya Simba kukaa njia panda, kwani bado haijajulikana ni lini atarejea tena kujiunga na kikosi,” kimesema chanzo hicho na kuongeza;
“Baada ya kufanyiwa vipimo madaktari wamemshauri kipa huyo akubali kufanyiwa upasuaji ambao utafanyika kwa njia ya kisasa, lakini Camara ameshindwa kukubaliana na uamuzi huo.”
Chanzo hicho kimeongeza kutokana na msimamo huo wa Camara, mabosi wa Simba wamefikiria njia nyingine ya kutafuta jembe lingine la kuja kuziba nafasi ya kipa huyo ikielezwa anaweza kuwa nje kwa muda wa miezi sita hadi kumi mara atakapofanyiwa upasuaji huo.
“Simba bado inasubiri uamuzi wake, lakini hapo hapo iko kwenye harakati za kusaka mbadala, kwani huenda jeraha hilo litamuweka nje muda mrefu, hicho ndicho kinachomtesa Camara.”
Licha ya Camara kukosekana katika milingoti mitatu ya Simba, lakini lango hilo lipo katika mikono salama ya Yakoub Suleiman aliyesajiliwa msimu huu akitokea JKT Tanzania, akionekana kuziba pengo vyema kwa kiwango alichoonyesha chini ya kocha Dimitar Pantev na Seleman Matola.
Iwapo Camara atafanyiwa upasuaji na kukaa nje ya uwanja itakuwa na maana mkataba alionao na Simba unaweza kuisha kwa kujiuguza kwa muda huo unaokadiriwa wa miezi sita hadi kumi, kwani hii iliwahi pia kumtokea nyota wa zamani wa Yanga, Yacouba Songne na alipopona aliibukia Ihefu (sasa Singida Black Stars) kabla ya kutua Tabora United (TRA United) ambako aliishia pia njiani.