Yanga yafanya kweli, Pedro aongezewa mtu

PALE Yanga kama kuna mtu hajui hatma ya kesho yake basi ni kocha wa viungo wa timu hiyo, Mokaila Tsephang ambaye kwa sasa yuko kwao Botswana akimalizia msiba wa mama mzazi aliyekwenda kumuuguza kabla ya kupatwa na tatizo hilo.

Hii ni kwa sababu, majaaliwa yake ndani ya klabu hiyo inayojiandaa na mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni ndogo, kutokana na ukweli kuwa, hata kabla ya kuondoka kwake kwenda kuuguza na kisha kufiwa, Mokaila alikuwa amekalia kuti kavu na kuwa kwenye presha kubwa kuanzia mashabiki hadi mabosi, wakiona kama jamaa hatoshi kuifanya timu hiyo iwe fiti uwanjani.

Mabosi wa Yanga wanaungana na mashabiki wa klabu hiyo juu ya kumuhitaji mtu mwingine katika eneo hilo la kuwarudishia utimamu wa mwili wachezaji wa kikosi hicho kama ambavyo ilikuwa kabla ya ujio wa raia huyo wa Botswana.

Baada ya kuondolewa kwa kocha Romain Folz na wasaidizi wake, ni Mokaila pekee aliyekuwa amesalia benchini, lakini mabosi wa Yanga walitaka jamaa pia afuate nyuma katika panga hilo, hata hivyo kocha mpya Pedro Goncalves alizuia mpango huo akitaka kumsoma kwanza kocha huyo wa mazoezi ya viungo.

Hata hivyo, wakati Pedro akizuia Mokaila asiondoke, Mwanaspoti limejulishwa kuwa Yanga inapiga hesabu za kumrudisha Adnan Behlulovic ambaye aliletwa nchini na kocha Sead Ramovic walioifanya Yanga icheze soka la Gusa, Achia, Twende Kwao na kutamba ndani na nje ya nchi.

Behlulovic, raia wa Bosnia & Herzegovina, wakati akitua Yanga katikati ya msimu uliopita kuchukua nafasi ya Taibi Lagrouni, aliwafanya wachezaji wa Yanga kuwa fiti uwanjani wakati wa soka la  Ramovic ambaye alikuwa na ile gusa achia twende kwao na kugawa vipigo vya maana kabla ya kuondoka kwenda Algeria.

Behlulovic (44) akakoleza hesabu hizo za Yanga baada ya juzi kubadili wasifu wake katika ukurasa wa mtandao wa Instagram akiandika kuwa ni kocha wa viungo wa Yanga, huku akiposti picha akiwa na fulana ya timu hiyo kisha akiweka bendera ya Tanzania.

“Tunataka kufanya mabadiliko kweli kwa yule kocha bahati mbaya tu ni huu msiba uliomfika lakini acha tutajua, hatufurahii sana kazi yake, kwasasa wachezaji wetu hawako fiti kama ilivyokuwa kabla,” amesema bosi mmoja wa juu wa Yanga na kuongeza;

“Unaweza kusema labda ni sisi viongozi lakini hata mashabiki wanaona na kitu kibaya zaidi kocha mpya naye amefika ameona vilevile, kwahiyo sijui kama atabaki hapa kwa muda mrefu.

“Tulifikiria kumrudisha Lagrouni lakini ameingia mkataba mgumu, kuna yule Adnan (Behlulovic) tunaendelea kupambana naye kumrudisha angalau naye tuliona ubora wa kazi yake.”

Yanga inajiandaa kuikaribisha AS FAR Rabat ya Morocco katika mechi ya kwanza ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa itakayopigwa Novemba 22, 2025 kuanzia saa 10:00 jioni, kabla ya kuifuata JS Kabylie ya Algeria wiki moja baadaye na mapema mwakani 2026 itavaana na Al Ahly katika mechi mbili mfululizo.