Unguja. Wakati Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, akitangaza Baraza jipya la Mawaziri, amesema dhamira yake ni kuacha alama itakayokumbukwa katika historia ya uongozi wake, huku akiwatahadharisha wanaomwona kuwa ni mpole kwamba safari hii atakuwa mkali zaidi kuliko awamu iliyopita.
Akizungumza leo Alhamisi, Novemba 13, 2025, Ikulu Zanzibar, mbele ya waandishi wa habari wakati akitangaza uteuzi huo, Rais Mwinyi amesema kipindi hiki ni cha mwisho katika uongozi wake, hivyo anataka akimaliza muda wake madarakani, utawala wa Serikali ya Awamu ya Nane uache alama zinazotambulika kwa utendaji na mafanikio makubwa kwa Zanzibar.
Akiwa ameongeza wizara mpya mbili na kufanya jumla kuwa 20 kutoka 18 za awali, Rais Mwinyi amesema lengo la mabadiliko hayo ni kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, akisisitiza kuwa katika kipindi hiki anataka kasi ya utendaji na utekelezaji wa yote waliyoahidi kwenye Ilani kwa wananchi wakati wa kampeni iwe kubwa.
“Kasi ya kipindi hiki cha pili, ambacho ndicho cha mwisho katika uongozi wangu, lazima iwe kubwa zaidi. Tunataka kuacha alama ya kudumu (legacy). Kama kuna wanaodhani mimi ni mpole, basi safari hii nitakuwa mkali zaidi,” amesema Rais Mwinyi alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Rais huyo amesema Serikali yake imejipanga kutekeleza kwa kasi ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni, akieleza kuwa baadhi ya sekta zilipokuwa chini ya wizara moja zilikuwa na mzigo mkubwa wa majukumu, hali iliyohitaji mgawanyo mpya ili kuongeza ufanisi wa utendaji.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma, akibainisha kuwa changamoto hizo bado zipo na zinahitaji kushughulikiwa kwa umakini.
Miongoni mwa walioteuliwa katika baraza hilo la mawaziri, wanawake wako saba huku wanaume wakiwa 14.
Hata hivyo, hadi sasa wizara nne hazijapatiwa mawaziri ambazo ni Afya, Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Utalii na Mambo ya Kale, pamoja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Akitaja vigezo vilivyotumika katika uteuzi wa mawaziri, Rais Mwinyi amesema vilijikita katika kuzingatia usawa wa kijinsia, uwiano wa kikanda, kiwango cha elimu, uzoefu wa kazi pamoja na sifa binafsi za kila mteuliwa.
“Tunapanga na kupanga upya, lakini kila uamuzi unazingatia vigezo hivi pamoja na sifa maalumu alizonazo mhusika mwenyewe,” amefafanua.
Rais Mwinyi amesema ameahirisha uteuzi wa mawaziri na manaibu wao katika wizara nne, akisubiri upande wa chama cha ACT-Wazalendo kupendekeza majina ya watu wanaoona wanastahili kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kama inavyotakiwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Kwa mujibu wa katiba hiyo, chama kinachostahili kuunda SUK hutakiwa ndani ya siku 90 kupendekeza majina ya Makamu wa Kwanza wa Rais na wale watakaoteuliwa kuwa mawaziri ndani ya Baraza.
Endapo muda huo utapita bila uteuzi kufanyika, Rais anakuwa na mamlaka ya kuunda Serikali ya chama kimoja, hali inayomaanisha kuwa upande wa upinzani unapoteza sifa za kushiriki serikalini.
Katika baraza jipya la mawaziri, watano waliokuwa mawaziri katika Serikali iliyopita hawajateuliwa. Wawili miongoni mwao wameachwa, huku watatu waliondolewa katika mchakato wa vikao vya Chama cha Mapinduzi (CCM) vya kupata wagombea wa nafasi za uwakilishi kwenye majimbo yao.
Waliokosa uteuzi ni pamoja na Tabia Maulid Mwita (Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo) na Ali Mrembo, (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Ikulu).
Wengine ni Shamata Shaame Khamis (Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo), Shaib Hassan Kaduara (Maji, Nishati na Madini), na Juma Makungu Juma, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha.
Katika mchakato wa CCM pia aliachwa Masoud Ali Mohamed, aliyekuwa Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, ambaye hata hivyo, Rais Mwinyi amemteua kuwa Mwakilishi na leo amemteua kuwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi.
Rais Mwinyi pia amefanya marekebisho katika muundo wa Serikali kwa kupunguza wizara zilizokuwa chini ya Ofisi ya Rais kutoka nne hadi mbili. Zilizobaki ni Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Rais – Ikulu.
Wizara za Kazi na Uwekezaji pamoja na ile ya Fedha na Mipango zimeondolewa chini ya ofisi hiyo.
Aidha, wizara mpya alizoziunda ni pamoja na Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, inayoongozwa na Mudrick Ramadhani Soraga, na Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji, inayoongozwa na Shaaban Ali Othman.
Rais Mwinyi pia amemteua Dk Saada Mkuya kuwa Mwakilishi na Waziri, Ofisi ya Rais (Ikulu), huku Haroun Ali Suleiman akirudishwa katika Wizara ya Katiba, Utumishi na Utawala Bora.
Idrissa Kitwana ameteuliwa kuwa Waziri wa Ofisi ya Rais, Tamisemi, akitokea nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma ameendelea na wadhifa wake. Wizara ya Fedha na Mipango sasa itaongozwa na Dk Juma Ali Akil, aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, huku Naibu wake akiwa Dk Hamad Omar Bakar.
Waziri wa Kazi na Uwekezaji ni Shariff Ali Shariff, wakati Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaendelea kuongozwa na Rahma Kassim Ali, akisaidiwa na Naibu Waziri Salha Mwinjuma.
Lela Mohamed Mussa anaendelea kuongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, akisaidiwa na Khadija Salum Ali. Riziki Pembe Juma amehamishiwa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, akisaidiwa na Ali Abdugulam Hussein.
Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo itaongozwa na Masoud Suleiman Makame, akisaidiwa na Dk Salum Soud Mohamed, huku Wizara ya Maji, Nishati na Madini ikienda kwa Nadir Abdulatif, ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. Naibu wake ni Seif Kombo Pandu.
Masoud Ali Mohamed ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, akisaidiwa na Mboja Ramadhan Mshenga. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itaongozwa na Dk Khalid Salum Mohamed, akisaidiwa na Badria Natai Masoud.
Anna Athanas Paul, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, sasa ni Waziri kamili wa wizara hiyo, akisaidiwa na Zawad Amour Nassor.
Mudrick Ramadhani Soraga ataongoza Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, akisaidiwa na Mohamed Sijiamin Mohamed, huku Wizara mpya ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji ikiongozwa na Shaaban Ali Othman, akisaidiwa na Hassan Khamis Hafidh.
Baadhi ya wananchi wamepokea uteuzi huo kwa maoni tofauti. Wengine wamepongeza hatua hiyo wakisema inalenga kuongeza ufanisi, huku wengine wakiona hakuna mabadiliko makubwa zaidi ya kubadilishana wizara.
“Ukiangalia safu ni ileile, huenda Rais ameona utendaji wao ni mzuri, hivyo akaona ni vyema kuendelea nao. Wakati mwingine unapoweka watu wengi wapya, ni kama kuanza upya,” amesema mdau wa siasa, Othman Said Ali.