CUF yaivaa INEC yaitaka ijiuzulu, INEC yajibu

Dar es Salaam. Wakati Chama cha Wananchi (CUF), kikiitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kujitathmini na, ikiwezekana, watendaji wake kujiuzulu, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jacobs Mwambegele amesema malalamiko yoyote dhidi ya chama hicho kama yana hoja zenye mashiko kipeleke mahakamani.

CUF miongoni mwa vyama 18 vyenye usajili wa kudumu vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu 2025, kimeishutumu tume hiyo kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo katika kusimamia uchaguzi huo, uliofanyika Oktoba 29, 2025. Huku kikieleza mawakala wengi wa vyama vya upinzani walizuiliwa kuingia vituoni kushuhudia shughuli hiyo.

Malalamiko ya CUF yametolewa leo Alhamisi, Novemba 13, 2025 Makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wake-bara, Othuman Dunga.

Amesema kilichotokea siku ya uchaguzi ni fedheha na msimamo wa chama hicho unabaki kama ulivyotolewa Novemba 11, mwaka huu na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba hawautambui kwa kuwa ulikuwa na ukiukwaji wa taratibu.

“Natoa wito kwa INEC ijitathmini, na ikiwezekana wajiuzulu ili kuepuka aibu hii iliyotokea na kulisababishia Taifa hasara kubwa. Leo watu wamepoteza maisha, miundombinu imeharibiwa, halafu wao wanaendelea kufurahia maisha,” amesema Dunga.

Kiongozi huyo aliyekuwa mgombea ubunge Kondoa Vijijini, amesema malalamiko dhidi ya baadhi ya makamishna wa INEC kuwa na uhusiano wa karibu na chama tawala yamekuwa yakipuuzwa kwa muda mrefu, hali aliyoitaja kama kiini cha kasoro nyingi zilizojitokeza katika uchaguzi huo.

Makamu Mwenyekiti wa chama Cha Wananchi (CUF) Othuman Dunga



“Tulilalamika muda mrefu kwamba baadhi ya makamishna wana nasaba na chama fulani. Ukiweka watu wa aina hiyo kwenye tume, unategemea nini kitokee,” amehoji.

Othuman anayedai alishikiliwa na Jeshi la Polisi na hakushuhudia matokeo yake amesema, CUF iliingia kushiriki uchaguzi huo si kwa sababu ilikuwa imeridhishwa na maandalizi ya tume, bali kuonyesha dunia namna chaguzi nchini zinavyoendeshwa.

“Tusingeshiriki, wangeiba nini sasa? Lazima ushiriki ili uone namna wanavyofanya. Wenzetu waliotabiri mapema walikataa kushiriki wakisema mfumo haujabadilika, lakini sisi tulitaka kuona kwa macho yetu,” amesema.

Amesema baada ya matokeo kutangazwa, chama chake kimebaini kuwa INEC imeshindwa kabisa kutenda haki, hivyo haistahili hata kuitwa tume huru.

“Wito wangu ni kwamba wajiuzulu mara moja. Na kama hawatafanya hivyo, nitapeleka hoja binafsi Baraza Kuu la CUF kuomba kuitishwa maandamano ya nchi nzima kushinikiza tume hii ivunjwe na kuundwe serikali ya mpito itakayotuandalia katiba mpya,” amesema.

Akizungumzia hali aliyoishuhudia wakati wa uchaguzi, akiwa Kuondoa Vijijini amesema mawakala wa vyama vya upinzani walitishwa na kulazimika kukaa kimya licha ya kuona wazi ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.

“Niliona vituo vingi vya kupigia kura masanduku yakiwa yamejaa mapema asubuhi kabla hata wapigakura hawajafika. Watu walihofia kuitiwa polisi, wakaamua kukaa kimya,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu madai hayo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mwambegele amejibu malalamiko yake akisema anaona hayana msingi, na kama kiongozi huyo wa CUF ana hoja zenye mashiko aende mahakamani kwakuwa ni chombo kinachotoa uamuzi.

“Sioni maana katika madai yake kama kweli ana hoja basi aende mahakamani, INEC tulifanya kazi yetu kwa mujibu wa sheria. Ingawa kweli kuna baadhi ya changamoto zilijitokeza kama za mawakala kuzuiwa kuingia kwa baadhi ya maeneo lakini tulizifanyia kazi na waliingia,” amesema Mwambegele.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ndani ya chama hicho, Yusuph Mbungilo amesema msimamo wa chama hicho uko sawa kama nchi inatambua umuhimu wa demokrasia basi lazima izingatiwe ili kuleta umoja wa Kitaifa.