Faili kamili la uwaziri mkuu wa Mwigulu Nchemba

Rais Samia Suluhu Hassan, ametimiza wajibu wake wa kikatiba. Ndani ya siku 14 baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia alipaswa kuwasilisha bungeni jina la mtu anayempendekeza kuwa Waziri Mkuu, ili wabunge wamthibitishe.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 51 (1) na (2), inatoa mwongozo huo wa lazima. Novemba 13, 2025, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amepokea jina la Mwigulu Nchemba. Kisha wabunge kwa wingi wao, wakamwidhinisha kwa kura za ndiyo.

Ni Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu wa 13 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya kufanya kazi kwa miaka minne na miezi saba, akiwa Waziri wa Fedha, katika muhula wa kwanza wa urais wa Dk Samia, amependa ngazi. Imempendeza Rais Samia kumpandisha daraja.

Kijana aliyekuwa na umri wa miaka 35 mwaka 2010, akawa mbunge wa Iramba Magharibi.

Chama chake ni CCM. Aliyekunywa maji ya bendera, akawa na kukuru-kakara nyingi na wapinzani. Shingoni alining’iniza skafu ya CCM au Bendera ya Taifa, tai zake daima zina rangi za Bendera ya Taifa.

Hupati shida kung’amua mahaba yake kwa Tanzania na chama chake, CCM. Mwaka 2011, akiwa mbunge, aliteuliwa kisha kuidhinishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), CCM, kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha (Mweka hazina).

Mwaka 2012, Mwigulu alipanda ngazi hadi kuwa Naibu Katibu Mkuu CCM, Tanzania Bara, nafasi ambayo aliishikilia mpaka mwaka 2015.

Mwaka 2013, Mwigulu akiwa Naibu Katibu Mkuu CCM, aliteuliwa pia kuwa Naibu Waziri wa Fedha. Ni kipindi cha urais wa Jakaya Kikwete, ambaye pia alikuwa ndiye Mwenyekiti wa CCM.

Desemba 2015, Mwigulu aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Ulikuwa uteuzi wa Baraza la Mawaziri la kwanza, la Rais wa tano, Dk John Magufuli.

Juni 2016, Mwigulu alihamishiwa na kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Alitumikia wizara hiyo kwa miaka miwili, kabla ya kuwekwa kando, kutokana na kukithiri kwa ajali za barabarani. Baada ya benchi la miaka miwili, Mei 2020, Mwigulu alirejea Baraza la Mawaziri, akiwa Waziri wa Sheria na Katiba.

Machi 19, 2021, Tanzania ilipata Rais mpya. Ni Dk Samia, kufuatia kifo cha Dk Magufuli. Baada ya kula kiapo kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia alimteua aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, kuwa Makamu wa Rais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kisha, akamteua Mwigulu kuwa Waziri wa Fedha.

Miaka minne ya kufanya kazi pamoja. Mafanikio ambayo Rais Samia ameyatengeneza, bila shaka imemridhisha na ikampendeza kumpandisha ngazi awe Waziri Mkuu. Ni kipimo kwamba Rais Samia anakoshwa na utendaji kazi wa Mwigulu, nidhamu na uwajibikaji wake, vinginevyo asingemteua nafasi hiyo kubwa.

Ripoti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Septemba 2025, ilionyesha kuwa makusanyo ya mwezi, yamefikia Sh3.47 trilioni. Hiyo ni karibu mara mbili ya Sh1.8 trilioni, ambayo yalikuwa makusanyo ya mwezi, kipindi Rais Samia alipomteua Mwigulu kuwa Waziri wa Fedha.

Ripoti za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), zinaonyesha afya ya kifedha ya Tanzania imeimarika kwa kiasi kikubwa, kipindi cha uwaziri wa fedha wa Mwigulu. Ukuaji wa pato la ndani la Taifa (GDP), kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ulivuka makisio ya asilimia 5.5 hadi kuwa asilimia 5.6. Ukuaji GDP ulikuwa chini ya asilimia 4, wakati Mwigulu anakula kiapo kuwa Waziri wa Fedha.

Sera za kifedha za Serikali ya Tanzania, zimewezesha mfumuko wa bei kugota kwenye asilimia ndogo ya 3.1. Sarafu ya Tanzania imeimarika.

Dola ya Marekani inauzwa kwa Sh 2,400 kutoka Sh 2,800. Hayo ni mafanikio kipindi cha Rais Samia, na bila shaka anatambua Mwigulu ni askari wake wa mwavuli, ambaye amempa matokeo hayo.

Oktoba 2025, Umoja wa Afrika, ulichapisha ripoti ya Uhusiano wa Kikanda Afrika (ARI) kwa mwaka 2025. ARI ni ripoti ambayo hutolewa na Umoja wa Afrika, kuonyesha maendeleo ya kanda kiuchumi.

ARI ni ripoti ambayo huandaliwa kwa ushirikiano wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Kamisheni ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika (ECA), Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), vilevile Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs). Ripoti hiyo ilionyesha kuwa Tanzania ina mwendo wa kasi na mzuri wa uzalishaji na uongezaji thamani bidhaa badala ya uuzaji wa malighafi nje ya nchi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania inashika nafasi ya kwanza kwa mwendo mzuri wa ukuaji uchumi katika Afrika Mashariki.

Burundi inashika nafasi ya pili, ikifuatiwa na Kenya. Nchi za Uganda, Rwanda na Sudan Kusini zipo chini. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia, zipo mkiani. Hayo ni matokeo chini ya Rais Samia na Waziri wa Fedha ni Mwigulu.

Miaka minne na miezi saba ya urais wa Dk Samia katika muhula wake wa kwanza, eneo la uchumi limechanua vema. Miradi mikubwa na ya kimkakati, ambayo imegharimu fedha nyingi, Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), Reli ya Standard Gauge (SGR), Daraja la Kigongo-Busisi, kwa pamoja ilikuwa chini ya asilimi 40 kukamilika kwake.

Ndani ya miaka minne na miezi saba, Rais Samia amekamilisha miradi hiyo na kuanza mingine kwa kasi, zikiwemo barabara za mabasi ya mwendokasi Dar es Salaam. Miradi hiyo imekuwa ikihitaji fedha na Mwigulu ndiye Waziri wa Fedha.

Pitia aya kwa aya kuanzia kwenye kichwa kidogo, “kwa nini Mwigulu”, ukiweza rejea tena, utaweza kuona kwamba ni kwa nini Rais Samia ameamua Mwigulu na siyo mbunge mwingine.

Kwa yanayofahamika waziwazi, utakuwa umepatia sana kama utapitisha jibu kwamba uwaziri wa fedha, ndiyo umempa Mwigulu uwaziri mkuu.

Katika moja ya vikao vya Bunge mwaka 2013, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, alizungumza bungeni akiwataka mawaziri wafanye kazi, wasijibu vijembe vya wapinzani kwa sababu yeye (Livingstone) na Mwigulu peke yao walikuwa wanatosha kuwakabili na kuwanyamazisha.

Kauli hiyo ya Livingstone, ilikuwa inajenga picha kuwa yeye na Mwigulu ndiyo wataalamu wa siasa za kushambuliana, kujibizana na kuchafuana.

Na huyo ndiye Mwigulu, ambaye hakukanusha matamshi ya Lusinde, na ambaye alipojitokeza kuomba tiketi ya kuwa mgombea urais wa CCM mwaka 2015, jina lake liliandikwa kwenye mawe nchi nzima, mpaka akaitwa rais wa mawe.

Kipindi cha urais wa Kikwete, Mwigulu akiwa kijana wa moto na mgeni bungeni, alifahamika kwa kutema maneno ya shombo dhidi ya wapinzani. Bungeni ‘alikinukisha’. Hoja zake mara kadhaa zilisababisha vikao vya bunge kusimama, pale wapinzani waliposimama na kutaka muongozo wa kiti, juu ya maneno au matamshi yake.

Kipindi cha urais wa Magufuli, Mwigulu alijipambanua kwa mtindo wake wa kuchukua hoja za wapinzani na kuzipiga mkazi, kuonyesha kwamba ni za hovyo na hazikubaliki.

Hilo lilimfanya Mwigulu aonekane siyo mwanademokrasia, na hufanya yanayowapendeza mabosi wake kwa kujipendekeza.

Wakati wa urais wa Samia, Mwigulu ameonyesha ukomavu. Haonekani kubishana, badala yake hutoa ufafanuzi pale inapolazimu.

Je, mabadiliko hayo ya Mwigulu ni ishara ya kukomaa kwake kisiasa na kiuongozi? Amebanwa na mtindo wa uongozi wa Rais Samia? Wizara ya Fedha inamshughulisha sana, kwa hiyo anakosa muda wa kutumia mkasi kama zamani au kutoleana maneno ya shombo na wapinzani?

Uteuzi wa Mwigulu kuwa Waziri Mkuu ni tafsiri kuwa ndoto ya waasisi wa Tanzania bado ipo hai. Yule mtoto aliyetumia kanga ya dada yake kama shuka ya kujifunika, aliyekua akichunga ng’ombe. Akapambana na elimu. Matokeo ya elimu yake yakampandisha ngazi hadi uwaziri mkuu.

Ni Tanzania ya yeyote anaweza kuwa yeyote. Kisa umezaliwa familia maskini isiyo na muunganiko na jamii za matajiri na viongozi, haimaanishi huwezi kuwa tajiri au kiongozi.

Mwigulu anabakisha hai ndoto ya wasisi wa Tanzania, sawasawa na Rais Samia. Tanzania ni nchi yenye fursa, na masilahi sawa kwa wote.

Mzawa wa kijijini, maisha ya kijijini, ambaye elimu ilimwezesha kusafiri miji kwa miji, hadi kuizunguka dunia. Mwigulu alizaliwa Januari 7, 1975. Alisoma Shule ya Msingi Makunda, Singida, akafaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari ya Ilboru, Arusha, ambayo wakati huo walipelekwa wanafunzi vipanga. Kisha, kidato cha tano na sita, Mwigulu alisoma Shule ya Juu ya Mazengo, Dodoma.

Mwigulu ni mhitimu wa shashada ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mwaka 2004. Mwaka 2006, alitunukiwa shahada ya uzamili ya Uchumi, UDSM.

Na kupitia chuo hichohicho, Mwigulu alifuzu shahada ya uzamivu (PhD) ya Uchumi. Kabla ya siasa, Mwigulu alikuwa mchumi daraja la kwanza, Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Alipokuwa Naibu Waziri wa Fedha, kuna wakati watu walimwita Sokoine wa Pili (Sokoine II), kwa kufananishwa na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu mara mbili, hayati Edward Moringe Sokoine. Mwigulu alipigana kwa vitendo kuhusu uwepo watumishi hewa ambao walikuwa wanalipwa mishahara kila mwezi.

Kauli ya Mwigulu aliyoitoa wakati wa mapambano yake ya watumishi hewa, ni kwamba Tanzania inaweza kujiendesha yenyewe kama mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali itazibwa pamoja na kukata minyororo yake yote.

Mwigulu alivalia njuga vitendo vya ukwepaji kodi ambavyo vinafanywa na wafanyabiashara wengi wakubwa.

Alisuka mipango na kuvamia ofisi kadhaa ambazo alikuwa amepenyezewa taarifa ya kuwepo kwa mashine feki za risiti. Hakika ni mpambanaji.

Ongeza mafanikio yake akiwa Waziri wa Fedha. Chukua na ahadi yake kwamba atawakabili wavivu serikalini baada ya kiapo cha Waziri Mkuu.

Inawezekana akawa Waziri Mkuu atakayemsaidia hasa Rais Samia. Hata hivyo, Rais Samia anahitaji Waziri Mkuu atakayefanya kazi kwa kujitoa asilimia 100 kusaidia kazi, na siyo yule anayeuwaza urais.

Mwigulu anafahamika kuwa ana ndoto za urais. Kwa ndoto yake hiyo, anakabiliwa na vita mbili. Mosi ni yake binafsi, anapaswa afanye kazi ya uwaziri mkuu bila kuufikiria urais.

Pili, wanaotamani urais, wanafahamu Mwigulu ni mshindani wao, wanaweza kumuundia majungu hadi kumharibia hata kwenye uwaziri mkuu.