Uislamu ndio dini ya mwanzo kutoa miongozo na sharia za kulinda na kutunza mazingira, kuhakikisha usalama wake, usawa wake, na ustawi wake, kwa kulinda maji, hewa, ardhi, wanyama, mimea na hata mawe. Allah Mtukufu amesema: “Yeye ndiye aliyekuumbeni kutoka ardhini na akakuamrisheni kuistawisha” (11: 61).
Aidha Allah amekataza uharibifu wa mazingira, akasema “….kuleni na kunyweni katika riziki ya Mwenyezi Mungu, wala msifanye uharibifu katika ardhi ….” (2: 60).
Mazingira katika Uislamu yanajumuisha kila kinachomzunguka mwanadamu kutoka katika maumbile ya dunia kama vile maji, hewa, ardhi, wanyama na mimea. Kuhifadhi mazingira ni miongoni mwa makusudio makuu ya Sharia ya Kiislamu. Uharibifu wa mazingira huathiri utekelezaji wa jukumu la uongozi (khilafa) na ustawi wa dunia.
Uislamu unahimiza kulinda vyanzo vya mazingira: maji, chakula, hewa na udongo. Uislamu umeyapa umuhimu maji na kuyazingatia kama chanzo cha uhai. Allah Mtukufu maesema “Na tumefanya kutokana na maji kila kitu kilicho hai (21: 30). Bila maji, hakuna maisha kwa binadamu, wanyama, au mimea. Maji yananywesha mimea, wanyama, na wanadamu, na Qur’ani imeeleza kuwa maji ni neema kutoka mbinguni.
Allah Mtukufu amesema: “Yeye ndiye anaye kuteremshieni maji kutoka mbinguni. Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa, na miti ya kulishia.” (16:10) Mtume wa Allah (rehema na amani ziwe juu yake) alikataza matumizi mabaya katika maji hata wakati wa kutekeleza ibada.
Alimwambia Sad alipokuwa anatumia maji mengi wakati wa kuchukua udhu: “Hivi unavyofanya ni israfu (matumizi mabaya), ewe Sa‘d.” Akauliza: “Je, katika uchukuaji udhu kuna israfu?” Mtume akajibu: “Ndiyo, hata kama upo kandokando ya mto unaotiririka.”
Kadhalika, Mtume wa Allah alikataza kujisadia katika maji yaliyotuama ili kulinda usafi wake na kuzuia magonjwa, na pia kuonya dhidi ya kutupa taka, mizoga au mabaki ya viwandani ndani yake. Kadhalika Uislamu unazingatia hewa safi ni sehemu ya maisha ya viumbe, kama ilivyo maji.
Kwa kuwa kila kiumbe hai kinaihitajia, Uislamu unahimiza kupanda miti na kuepuka kuikata bila sababu za dharura. Mtume wa Allah alisema: “Hakuna Muislamu anayepanda mti au mimea kisha kiumbe chochote kiwe ndege, binadamu, au mnyama kikala kutoka humo, ila itakuwa ni sadaka kwake.”
Pia Mtume wa Allah alikataza kukata miti kiholela kwa sababu ina faida nyingi, ikiwemo kupendezesha mazingira, kutoa kivuli, kustawisha wanyama, na kusafisha hewa. Akasema: “Msikate miti, kwani ni hifadhi ya wanyama wakati wa ukame.”
Aidha, Uislamu umehimiza umuhimu wa kuitunza ardhi, kuistawisha, na kukataza kuharibu au kueneza uchafuzi ndani yake. Miongoni mwa njia za kulinda ardhi ni kukataza kujisaidia haja kubwa au ndogo kwenye njia za watu au sehemu wanazopumzika. Mtume alisema:
“Jiepusheni na vitu viwili vinavyosababisha laana.” Masahaba wakauliza: “Ni vipi hivyo?” Akajibu: “Ni kwa yule anayejisaidia katika njia za watu na kwenye kivuli chao cha kupumzikia.” Kadhalika miongoni mwa njia za kulinda ardhi na uchafuzi wa mazingira ni kuainisha sehemu maalumu za kujisaidia haja, kama alivyosema Mtume: “Anapotaka mmoja wenu kujisaidia haja ndogo, achague (ainishe) sehemu maalum|”
Vile vileUislamu umehimiza kuondoa taka na uchafu barabarani na nyumba za ibada. Mtume wa Allah alisema: “Nilionyeshwa amali za umma wangu, mazuri na mabaya. Miongoni mwa mazuri niliyoyaona ni kuondoa kero njiani, na miongoni mwa mabaya niliyoyaona ni makohozi yaliyomo msikitini…..” Pia Mtume wa Allah alisema:
“Kuondoa kero njiani ni sadaka.” Aidha, Uislamu umehimiza kupambana na jangwa kwa kuihisha na kuistawisha ardhi tasa, na kupanda miti. Mtume wa Allah alisema: “Mwenye kufufua –kuistawisha- ardhi isiyo na mmiliki, yeye ndiye mwenye haki nayo.”
Kilimo na upandaji ni sehemu muhimu ya kustawisha ardhi na kulinda mazingira. Mtume alisema: “Kitakaposimama Kiama na mkononi mwa mmoja wenu ana mche wa mtende, ikiwa ataweza kuupanda (katika siku hiyo), basi na apande.” (Ahmad).
Kulindawanyama ni sehemu muhimu ya mfumo wa maisha duniani, na ِ Allah Mtukufu ameweka ndani yao manufaa mengi kwa binadamu. Uislamu umehimiza: Kuwafanyia wanyama wema Mtume wa Allah amesema: “Hakika Allah amewajibisha kufanya ihsani katika kila jambo; mnapoua (wanyama wenye madhara), fanyeni kwa wema, na mnapochinja (kwa kula), fanyeni kwa wema; na mmoja wenu ahakikishe kisu chake ni kikali (ili kuepusha maumivu makali kwa mnyama)….”
Uislamu umekataza kuwatendea wanyama ukatili. Mtume wa Allah amelaani aliyemfanya mnyama hai kuwa shabaha ya kujifunza kulenga kwa mishale au silaha nyingine, na kuwatendea ukatili wa aina yoyoteKutokana na mafunzo haya, inadhihirika wazi kuwa kulinda mazingira na rasilimali zake ni jukumu la Kisharia katika Uislamu. 0712 690811