Chippo atua kuinoa Mtibwa | Mwanaspoti

UONGOZI wa Mtibwa Sugar umemshusha rasmi nchini aliyekuwa Kocha wa Pamba Jiji, Coastal Union na TRA United zamani Tabora United, Mkenya Yusuf Chippo ili kukiongoza kikosi hicho msimu wa 2025-2026, kwa kushirikiana na Awadh Juma ‘Maniche’.

Timu hiyo iliyorejea tena Ligi Kuu msimu wa 2025-2026, baada ya kushuka 2023-2024, ilianza msimu kwa kufundishwa na Awadh Juma ‘Maniche’ aliyeipandisha, ingawa hakidhi vigezo vya kuongoza benchi la ufundi kama kocha mkuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chippo amesema ni kweli amewasili nchini baada ya kutumiwa tiketi ya ndege na mabosi wa timu hiyo, hivyo kwa sasa yupo tayari kwa ajili ya kupata changamoto mpya, akiwa na kikosi hicho.

“Ni kweli nimefika Tanzania baada ya kufikia makubaliano na uongozi wangu, ni muda mzuri kwangu wa kufanya tathimini ya kina ya timu kiujumla na kuangalia pia jinsi ambavyo kwa zaidi ya wiki moja tunaweza kujipanga vizuri,” amesema Chippo.

Kwa msimu wa 2025-2026, Maniche aliiongoza Mtibwa katika mechi tano za mwanzo za Ligi Kuu na kati ya hizo alishinda moja tu, akitoa sare mbili na kupoteza mbili, ikishika nafasi ya 13, baada ya kukusanya jumla ya pointi zake tano.

CHIP 01


Mechi aliyoshinda Maniche ni ya ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Fountain Gate, Septemba 28, 2025, akitoka suluhu (0-0) na Coastal Union, Oktoba 19, 2025 na Dodoma Jiji Oktoba 22, 2025, huku akipoteza dhidi ya Mashujaa 1-0, Septemba 21, 2025.

Nyingine aliyopoteza ni ya kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya Yanga, Oktoba 28, 2025 na katika mechi hizo tano ilizocheza chini ya Maniche ilifunga mabao mawili tu, huku ikiruhusu matatu tatu.

CHIP 02


Chippo aliyeachana na Murang’a SEAL ya kwao Kenya tangu Agosti 21, 2025, anakumbukwa na mashabiki wengi hasa baada ya kukiongoza kikosi cha Ulinzi Stars kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya ‘KPL’ kati ya 2003 na 2005 na kuhudumu akiwa kocha msaidizi wa Harambee Stars kuanzia 2008 hadi 2011.

Kibarua cha kwanza kwa Chippo kitakuwa dhidi ya KMC, mechi itayopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Novemba 25, 2025.