Wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipolihutubia Bunge la 12, katika Mkutano wa Pili, Aprili 22, 2021, hotuba yake ilichukua takribani saa moja na dakika 30 (dakika 90).
Rais Samia alitoa hotuba hiyo wakati huo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa Job Ndugai huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) wakati huo (Aprili 2021), alikuwa George Simbachawene.
Rais Samia alikwenda kulihutubia Bunge hilo takribani mwezi mmoja tangu Tanzania iliposhuhudia kwa mara ya kwanza Rais aliyekuwa madarakani kufariki dunia.
Ni John Pombe Magufuli, ambaye Machi 17, 2021 alifariki dunia ikiwa ni takribani miezi minne na nusu alipoapishwa kuwa Rais, Novemba 5, 2020 katika muhula wake wa pili Ikulu.
Samia ambaye alikuwa Makamu wa Rais, aliapishwa na Jaji Mkuu wa wakati huo, Profesa Ibrahim Juma kuwa Rais kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.
Kwa hiyo, Rais Samia alikwenda kulihutubia kama mkuu wa nchi. Awali, alikwenda bungeni akiwa Makamu wa Rais nyuma ya Rais Magufuli.
Hotuba yake ilijikita katika kuweka bayana mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita, na ilikuwa na kaulimbiu iliyokuwa imeanza kujengeka na kutumiwa na Rais.
Maneno au kauli za vionjo (ambazo zilikamata hisia za watu na kuashiria mwelekeo mpya) ni pamoja na:
“Kazi Iendelee”: Hii ilikuwa ni kaulimbiu au salamu iliyoonyesha dhamira ya kuendeleza miradi na kazi nzuri zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, huku ikifanya marekebisho pale inapobidi.
“Tutaenzi na kuendeleza mambo yote mazuri, lakini pia tutafanya mabadiliko pale itakapobidi kwa lengo la kukuza ufanisi”: Kauli hii ilitafsiriwa na wengi kama mwelekeo wa maridhiano, maboresho, na ujenzi wa utawala wenye tija zaidi.
Pia, katika kutangaza nia ya kufanya maboresho makubwa kwenye eneo la biashara na uwekezaji: Alisisitiza kuondoa urasimu na kuimarisha mazingira ya biashara.
Rais Samia kwenye hotuba hiyo aliweka msisitizo katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa na kidiplomasia kwa kusema:
“…Tutazifanyia tathmini sera zetu zote za kisekta na kiutendaji, na kufanya marekebisho pale ambapo tunaona kuna upungufu au kuna haja ya kuongeza ufanisi zaidi.”
Hotuba ya kuvunja Bunge la 12
Rais Samia katika hotuba yake ya kulivunja Bunge la 12, Juni 27, 2025, ilielezwa kuwa “ya kihistoria” na “kubeba kila kitu.”
Hotuba hiyo ya kuvunja Bunge la 12 ilichukua takriban dakika 166 au takriban saa tatu, na Spika wa Bunge alikuwa Dk Tulia Ackson.
Kwenye hotuba hiyo ya kuvunja Buge Waziri Mkuu alikuwa Kassim Majaliwa. Kwa sasa Majaliwa ni mstaafu.
Hotuba hiyo ambayo ililenga kuorodhesha mafanikio na kuangazia mustakabali wa Taifa kabla ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, ilikuwa na vionjo kadhaa.
Baadhi ya vionjo na kauli muhimu ni: Kusisitiza maridhiano na demokrasia: Alipongeza kuongezeka kwa uhuru wa habari na uhuru wa watu kutoa maoni yao katika kipindi chake, akionesha nia ya kuendelea kusimamia uhuru wa vyombo vya habari.
Kutambua Mchango wa Spika: Alimpongeza Spika Tulia Ackson kwa uongozi shupavu, hususan kwa kuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo na kwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), akimwambia: “Hakika hujatuangusha wanawake wenzio.”
Kasi ya miradi ya maendeleo: Alisisitiza utekelezaji wa miradi mikubwa na utendaji wa Serikali, akitumia kauli yake ya kitambulisho ya “Kazi Iendelee” kuonyesha kuwa mipango mingi imekamilika au iko njiani kukamilika.
Uchumi na Haki: Alieleza mafanikio katika usimamizi wa uchumi, kuongezeka kwa mapato, na pia msisitizo katika Utawala wa Sheria na Maboresho ya Mfumo wa Utoaji Haki, akisema: “…amani na utulivu hustawi pale ambapo haki huonekana kutendeka.”
Leo, Ijumaa, Novemba 14, 2025, ndiyo siku ambayo Rais Samia ambaye katika uchaguzi mkuu ameshinda kwa asilimia 97.6 anatarajiwa kulizindua rasmi Bunge jipya la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kuanza kwa vikao vya awali vya Bunge Novemba 11, 2025.
Uzinduzi huu ni tukio la kihistoria na lenye uzito wa kikatiba.
Anakwenda kulizindua Bunge hilo ambalo sasa linaongozwa na Mussa Zungu.Aidha, anakwenda kutoa mwelekeo wa Serikali yake wakati Waziri Mkuu ni Dk Mwigulu Nchemba ambaye amemuapisha asubuhi ya leo kushika wadhifa huo huku Makamu wa Rais akiwa ni Dk Emmanuel Nchimbi.
Kumekuwa na upekee wa Rais Samia kila anapokwenda kuhutubia Bunge, miongoni ni kila anapokwenda Spika ni mwingine na sasa anakwenda Waziri Mkuu, Dk Mwigulu naye ni mpya.
Katika uzinduzi huo, Rais anatoa hotuba ya kufungua Bunge, ambayo huweka dira, mwelekeo, na vipaumbele vya Serikali kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, akianisha ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Rais Samia analizindua Bunge la 13 ambayo inasubiriwa na wananchi wa ndani na nje ya Tanzania kujua mkuu huyo wa nchi ataeleza nini hasa kile kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Pia, huenda katika hotuba hiyo akatoa mwelekeo wa baraza lake la mawaziri litakavyokuwa na bila shaka wakati wowote baada ya leo akalitangaza.