KWA sasa habari ya mjini ni kiungo mpya wa Simba, Moruice Abraham ambaye ameonyesha kiwango kilichowakuna wengi na mmoja ya walioshindwa kujiuzuia kwa nyota huyo chipukizi ni kiungo wa Mbeya City, Omary Chibada.
Chibada amesema miongoni mwa mastaa wanaomkosha Ligi Kuu Bara ya msimu huu ni dogo huyo wa Msimbazi ambaye amekuwa gumzo msimu huu.
Morice, aliyetua Simba akitokea RFK Novi ya Serbia, ni kati ya mastaa chipukizi anayefanya vizuri akiwa ni mchezaji pia wa timu ya taifa, Taifa Stars.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chibada amesema hadi sasa hakuna mchezaji ambaye anamkosha kwa upande wa ligi ya ndani kama Morice.
Amesema Morice ni mchezaji mwenye nidhamu na juhudi kubwa ambayo kama utani yamewafikisha mbali kwani kuchezea timu kama Simba kwa umri wake ni mafanikio.
“Wapo wengi ila kwa unyenyekevu ni Morice Abraham, namwangalia sana, zaidi ni heshima anayotoa kwa wachezaji wenzake na shauku ya kujifunza aliyonayo kila siku,” amesema Chibada na kuongeza;
“Kila mchezaji anatakiwa kumwona kama kielelezo cha kujifunza hasa hawa ambao wanaanza kuchipukia kutokana na shauku walizonazo za kuonekana. Napenda sana anavyocheza nidhamu yake na utulivu itamfikisha mbali katua Simba msimu huu lakini uwezo wake unampa nafasi ya kucheza mbele ya wachezaji wakubwa tena wageni.”
Morice hadi sasa amecheza mechi mbili kati ya tatu ambazo Simba imecheza, huku akifikisha jumla ya dakika 114 na kuiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili katika msimamo na ikiwa ni moja kati ya timu nne za Tanzania zilizotinga makundi ya michuano ya CAF.