Programu ya Misitu kunufaisha wakulima wadogo 100,000

Musoma. Zaidi ya wakulima wadogo 100,000 kutoka mikoa ya Mara, Mwanza na Pwani wanatarajiwa kunufaika na programu ya kilimo misitu, ikiwa na lengo la kuboresha uzalishaji wa kilimo na kuongeza kipato cha kaya, jamii na taifa kwa ujumla.

Programu hiyo inatarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2028 na Shirika lisilo la kiserikali la Vi Agroforestry kwa ushirikiano na wabia mbalimbali wa maendeleo.

Akizungumza katika kongamano la kilimo linalofanyika Musoma leo Ijumaa, Novemba 14, 2025, Mwakilishi wa Vi Agroforestry

Kanda ya Afrika Mashariki, Dk Monica Nderuti amesema programu hiyo pia inalenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dk Nderuti amesema utekelezaji wa programu hiyo utasaidia kuimarisha kilimo biashara miongoni mwa wakulima na kuwawezesha kuachana na mbinu za zamani zilizolenga uzalishaji wa chakula kwa kujikimu.

“Wakulima watafundishwa kufanya kilimo biashara sambamba na kuzingatia usalama wa chakula na lishe bora. Tunataka kuwatoa kwenye kilimo cha mazoea na kukifanya kuwa fursa ya kiuchumi, licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Ameongeza kuwa utafiti wao umebaini kuwa wakulima wengi bado wanakumbana na changamoto kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu mpito kutoka kilimo cha mazao pekee kwenda kilimo misitu.

“Mbali na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kilimo misitu kina manufaa mengi ikiwemo utunzaji wa mazingira na bayoanuai, pamoja na kuwa chanzo muhimu cha mapato. Tunataka kuhakikisha wakulima na jamii wanaelewa faida hizi ili wengi wao wanufaike,” amesisitiza.

Akizungumzia kongamano hilo lililoandaliwa na shirika lake, Dk Nderuti amesema linatoa nafasi kwa washiriki kupata elimu kuhusu namna kilimo kinaweza kutumika kupambana na umasikini.

“Kutakuwa na mafunzo mbalimbali ya kilimo, na kwa mwaka huu tumeweka mkazo kwenye kilimo misitu ili washiriki wajifunze mbinu za kufanya mapinduzi ya kiuchumi kupitia kilimo,” amesema.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Yasintha Nzogera,akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la kilimo mjini Musoma.  Picha na Beldina Nyakeke



Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Yasintha Nzogera, ametoa rai kwa wadau kushirikiana na Serikali kutekeleza mikakati ya kitaifa na kimataifa ya kilimo misitu.

Amesema Serikali inalenga kufikia kaya 15,000 ifikapo mwaka 2031 kupitia uwekezaji katika kilimo misitu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga uchumi jumuishi na endelevu kupitia sekta ya kilimo.

Nzogera amesema kilimo misitu endelevu kitaongeza tija na kustawisha maisha ya wananchi kwa kuchochea ukuaji jumuishi na endelevu, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa elimu na teknolojia bora kwa wakulima.

Amefafanua kuwa mustakabali wa sekta ya kilimo nchini unategemea kwa kiasi kikubwa kilimo misitu, kwani kinaendana na mkondo wa Serikali wa kuongeza uzalishaji wa mazao endelevu yenye tija, thamani na ushindani wa soko la ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesema mikakati iliyopo inalenga pia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza uzalishaji wa chakula na kuinua kilimo biashara, ili kuchochea uchumi wa mwananchi mmojammoja na Taifa kwa ujumla.

Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo wamependekeza kuanzishwa kwa jukwaa la kitaifa la kilimo misitu litakaloratibu kwa ufanisi utekelezaji wa mikakati hiyo.

Juma Mbeba amesema jukwaa hilo litasaidia kuunganisha juhudi za wadau mbalimbali na Serikali, kuratibu taarifa, kubadilishana uzoefu na kufuatilia maendeleo ya programu za kilimo misitu kwa manufaa ya uchumi na mazingira.

Kwa upande wake, Maige Wambura amesema utekelezaji wa mikakati hiyo kwa pamoja utasaidia kuimarisha usalama wa chakula nchini kwa kuwajengea wakulima uwezo wa kufanya kilimo chenye ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.