Moshi. Kama ilivyo kawaida kwa baadhi ya watu wa makabila wakiwamo Wachaga kurejea makwao wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka, tayari dalili za msimu huo zimeanza kushuhudiwa katikati ya mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Miongoni mwa ishara hizo ni maua yenye rangi ya zambarau yanayoanguka kandokando ya barabara na kuupa mji huo mandhari ya kupendeza, yakitoa taswira ya maandalizi ya sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.
Mwananchi Digital imetembelea maeneo mbalimbali ya mji huo wa Moshi, ikiwamo ya Shanty Town, sehemu za Soweto, KCMC, Rengua na Majengo na kushuhudia maua hayo yakiwa yameenea chini na kupamba mandhari ya barabara za maeneo hayo.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Moshi wamesema kuwa maua hayo huamsha hisia na kuwapa taswira ya kuukaribisha msimu wa sherehe za mwisho wa mwaka, hususan Krismasi na Mwaka Mpya.
Mwalimu Elisaria Mrema kutoka Kijiji cha Korini Kusini, Kata ya Mbokomu akizungumza na Mwananchi Digital kuhusiana na msimu huo, amesema maua hayo yana maana ya kipekee kwa watu wa jamii ya Wachaga.
“Kuna miti ambayo kipindi hiki huanza kutoa maua ya zambarau tunapokaribia siku ya kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwetu sisi huu ni ujumbe kwamba msimu wa sikukuu umefika,” amesema Mrema.
Amesema rangi ya maua hayo huleta furaha na hamasa ya kuanza maandalizi ya sherehe hizo, ambazo huwakutanisha ndugu, jamaa na marafiki.
“Miti hii ndiyo ishara kwamba sherehe hizi ni za kweli, zinatupatanisha na kutupambia miji yetu na kututia moyo wa kusherehekea kwa furaha,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Angel Uwoya mkazi wa Marangu, amesema msimu huu huwa ni fursa ya familia kuandaa mambo mbalimbali kwa ajili ya sherehe ambazo huwakutanisha ndugu ambao hawakuonana kwa mwaka mzima.
“Karibuni Kilimanjaro. Moshi inapopambwa na maua kama haya, tunajua wakati wa kurudi nyumbani umefika. Ndipo tunapokutana na ndugu, tunafanya sherehe, tunachinja na kufurahia pamoja,” amesema.
Ameongeza: “Wageni wote tunawakaribisha waje wajionee vivutio vyetu kama ndizi, mbege na mandhari yetu mazuri.”
Akizungumzia maandalizi ya sikukuu hizo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amewahakikishia wananchi na wageni kuwa hali ya usalama ni shwari, na Moshi ipo tayari kupokea wageni katika msimu huu wa mwisho wa mwaka.
“Nawahakikishia wananchi wa Moshi kwamba mji wetu ni salama na shughuli zinaendelea vizuri. Tunashukuru kwa kudumisha amani na mshikamano, hali ambayo inafanya tuendelee kuwa sehemu salama,” amesema.
Mnzava amesema kila mwaka, kuanzia Novemba kuelekea Desemba, mabadiliko ya mazingira ya mji huashiria utamaduni wa watu kurejea nyumbani kwa ajili ya sikukuu.
“Hata ukipita barabarani unaona jinsi miti ya maua inavyobadilika na kutupa taswira ya mwisho wa mwaka. Nawaalika wote, wenyeji na wageni, kuja kusherehekea hapa Moshi,” amesema.
Amesisitiza kuwa Serikali imeweka utulivu wa kutosha ili familia ziweze kukutana, kubadilishana mawazo na kuimarisha umoja.
“Karibuni Moshi. Mji upo salama. Tuna vivutio vizuri kama Mlima Kilimanjaro, Msitu wa Rau na maeneo mengine tulivu ya kupumzikia,” amesema.