TMA yataja sababu mvua za wastani, ikieleza uwepo wa upepo mkali

Mbeya. Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imesema moja ya sababu za kutokea kwa msimu wa mvua za wastani na chini ya wastani ni ongezeko la joto katika uso wa Bahari ya Pasifiki.

Kwa mujibu wa TMA, mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya pili au ya tatu ya Novemba, 2025 na kuendelea hadi Mei 2026 na zinaweza kusababisha athari mbalimbali ikiwamo maji kuingia kwenye makazi, mito, mifereji na vijito.

Meneja wa TMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elius Lipiki ametoa ufafanuzi huo leo Ijumaa, Novemba 14, 2025, alipozungumza na Mwananchi Digital kuhusu utabiri wa msimu na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa na wananchi, hasa wakulima.

“Utabiri unaonyesha uwepo wa mvua za wastani na chini ya wastani, na moja ya sababu ni joto lililoko kwenye uso wa Bahari ya Pasifiki,” amesema.

Lipiki ametaja baadhi ya athari zinazoweza kujitokeza kuwa ni pamoja na upepo mkali na maji kujaa kwenye makazi na maeneo ya mkusanyiko kama mito, mifereji na vijito. Amehimiza wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa mara kwa mara ili kuchukua tahadhari mapema.

Ameongeza kuwa, pamoja na athari hizo, mvua zinazotarajiwa zinatoa fursa kwa wakulima kuanza maandalizi ya mashamba kwa ajili ya kupanda mazao kama maharage na mahindi.

“Tunashauri wadau wa sekta ya kilimo, wakulima na wataalamu kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa ili waweze kuchukua hatua stahiki mapema,” amesema.

Ameeleza kuwa kwa kawaida, joto likiwa juu ya wastani huashiria msimu wenye mvua nyingi, na kwamba TMA inaendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa msimu.

“Tunashauri jamii na wadau kufuatilia taarifa za utabiri wa saa tano, kumi hadi mwezi mzima ili kuweka sawa kalenda za uzalishaji wa mazao katika msimu ujao,” amesema.

Lipiki pia amezitaka mamlaka za sekta ya kilimo na huduma ya maji, pamoja na wataalamu wa kilimo, kutumia utabiri wa hali ya hewa kama nyenzo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkulima wa mazao ya chakula na biashara, Oriva Sanga, amesema msimu wa kilimo wa mwaka huu unawatia wasiwasi kutokana na kuchelewa kwa mvua.

“Kipindi kama hiki mwaka jana tulikuwa tumeandaa mashamba na kupanda mbegu, lakini sasa tuna mashaka kuwa uzalishaji unaweza kuwa mdogo na kutuletea hasara,” amesema.

Naye Witness Kamwela amesema mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa changamoto kubwa katika uzalishaji, na hivyo inapaswa wataalamu wa kilimo wawe karibu na wakulima ili kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na hali hiyo kuanzia hatua za awali.

“Mabadiliko ya tabianchi ni mwiba mkali unaowapa ugumu wakulima kuzalisha kwa tija, jambo ambalo mara nyingi husababisha kupanda kwa gharama za vyakula na kuwaumiza wananchi wa kipato cha chini,” amesema.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa mazao ya nafaka katika soko la Machinjioni, Rehema Noel, ameziomba mamlaka husika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuhakikisha maofisa ugani wanawafikia wakulima ili waweze kutumia vyema msimu huu wa mvua za wastani na chini ya wastani katika kuongeza uzalishaji.