Tume kuchunguza vurugu za Oktoba 29

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu amesema Serikali yake itaunda tume maalumu ya kuchunguza vurugu zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 ili kujua kiini cha tatizo hilo.

Vurugu hizo zilizosababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa miundombinu mali za umma na binafsi pia zilisababisha kusimamishwa kwa shughuli mbalimbali.

Samia ametoa msimamo huo  leo Novemba 14, 2025 wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa Bunge hilo la 13.

Rais huyo ameeleza kusikitishwa kwake na kilichotokea siku hiyo huku akiwataka wabunge na wageni waliokusanyika bungeni hapo kusimama kwa dakika moja kuwaombea waliopoteza maisha.

“Tumuombe Mungu azipokee roho za marehemu walipoteza maisha katika vurugu zilizotokea Oktoba 29. Binafsi nimehuzunishwa sana na tukio lile natoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao, Mungu awapumzisha na majeruhi tunawaombea wapone haraka.”

“Kwa wale waliopoteza mali zao, tunawaombea wawe na ustahimilivu na uvumilivu. Serikali imechukua hatua ya kuunda tume ya kuchunguza yaliyotokea ili tujue kiini cha tatizo, taarifa hiyo itatuelekeza kwenye mazungumzo ya kuleta maelewano na amani” amesema Samia.